Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba, Yanga ukubwa wenu uko wapi?

LIVE Simba Vs Yanga Simba, Yanga ukubwa wenu uko wapi?

Mon, 6 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati fulani napata tabu sana kukubali na kuuthibitisha ukubwa wa hizi klabu zetu pendwa hapa nchini Simba na Yanga unaozungumzwa ni upi. Simba na Yanga zinajinadi na kutamba kwamba ni timu kubwa Tanzania na pengine ukubwa wake huo unatambulika Afrika. Ni miongoni mwa timu kubwa katika Bara la Afrika.

Inawezekana vipo vigezo ambavyo wanavyo na wanavitumia vinavyohalalisha ukubwa wao Tanzania na Afrika ambavyo sijui havijaniingia akilini.

Wakati fulani nawaza, lakini nashindwa kuwazua kwamba klabu kama Simba na Yanga ndizo kubwa, ila wanachama, mashabiki, wapenzi na wadau wake ni wachanga, hawajakua bado hivyo kuwaza na kutenda kwao kwa kupo chini. Nawaza tu ukubwa wa hii miamba.

Kwa nini mpapaso wa Jumamosi ya leo unajikita kutaka kujua ukubwa wa Simba na Yanga ni upi ni kutokana na kutoiona tofauti ya kimantiki ya hao wanaojinadi ni wakubwa na hao wengine wanaodaiwa wadogo, katika mambo fulani hivi. Unajua ukikua, ukawa mkubwa, umepevuka mwili na akili, huliilii hovyo kama enzi zile za utoto mawazo na mazungumzo na hata matendo yanakuwa tofauti na yale uliyoyafanya ukiwa mtoto.

Mtoto akijisikia haja huweza kujisaidia popote. Hujisaidia hadharani, kwenye nguo, hutembea uchi, huchezea na hata kula kinyesi chake. Hii ni kawaida kwa mtoto mdogo. Hakuna atakayeshangaa mtoto mdogo kuyafanya hayo, lakini mkubwa akiyafanya lazima atiliwe shaka utasikia mwezi mchanga huyo hii yote ni kuonyesha kwamba ipo tofauti kubwa kati ya mtoto na mkubwa.

Simba na Yanga ukubwa wenu ni upi hasa unaowatofautisha na udogo wa wengine kama kina Ruvu Shooting, Azam, Biashara, KMC, Geita Gold, Kagera Sugar, Coastal Union, Mtibwa na wengine wote mnaowaita wadogo.

Ukubwa wenu ni kuanzishwa na kuwepo kwenu miaka mingi. Huenda mashabiki wengi wa kurithi mlionao au kipato tegemezi mlichonacho ni hivi kweli vinatosha kuwafanya mjipige kifua kwamba ninyi ni wakubwa katika soka la Tanzania na Afrika au ni nini hasa utambulisho wa ukubwa wenu.

Au inatosha ninyi kuitwa wakubwa mkisajili wachezaji wa kigeni ambao wengi uwezo wao ni sawa au chini ya uwezo wa Watanzania. Mnaowalipa vizuri kidogo kuliko wa hapa ambao ni bora pengine kuliko hao wageni, lakini malipo yao kidogo yakilinganishwa na ya hao wageni au kuajiri baadhi ya watendaji, wafanyakazi wa kigeni na makocha wazungu huu n-dio ukubwa wenu?

Inawezekana, labda kwa fikra zangu ambazo ni sahihi kwangu, lakini kwako ikawa kinyume ila kwa upotofu ukubwa wenu ni uwezo mlionao wa kupanda ndege kwenda mikoani kucheza ligi na timu za huko ambao timu nyingine hawana.

Labda ukubwa wenu ni kutwaa ubingwa wa soka nchini mara nyingi zaidi kuliko klabu nyingine - ubingwa ambao baadhi ya Watanzania wakiwemo viongozi wa Serikali na wastaafu wa ngazi ya juu kabisa serikalini wanauhoji na kuutilia shaka kwamba huenda ni wa hila na mazungumzo na ndio maana mkienda kimataifa mapema tu mmeng’olewa. Hii kweli ni moja ya alama ya ukubwa wenu mnaojidai nao na mmeridhika kabisa inatosha kuwatambulisha na kuwathibitisha ninyi ni wakubwa?

Pengine ukubwa wenu ni ile hali ya kutotaka kufungwa hata kama mnazidiwa uwezo na hizo timu nyingine mnazoziita ndogo. Ni kuzua mgogoro kati yenu kwenye timu zenu wakati mwingine kushambuliana ninyi kwa ninyi na kutimuana madarakani timu zinapokosa ubingwa. Huo ndio ukubwa wenu.

Au kuwasifia wachezaji na benchi la ufundi wanapopata ushindi hata wa kubahatisha, kiwango kibovu katika mechi fulani na kuwaona wa hovyo wasio na uwezo, wasiofaa wanapofungwa kwenye mchezo mwingine kwa isivyo bahati kwa kuwa kiwango kilionekana bora japo walifungwa kiasi cha kutaka watimuliwe, labda huo ndio ukubwa wenu mnaotamba nao.

Inawezekana ukubwa wenu ni pale mnapokutana ninyi wenyewe katika mechi yoyote, yeyote atakayefungwa anaingia kwenye mgogoro, malumbano, viongozi kulaumiana, kushambuliana kwa maneno, kutimuana na kufuta benchi la ufundi hata kama limekuwepo kwa muda mfupi tu, kwenu hiyo imetosha na mnafurahi kuitwa timu kubwa.

Yaani, mpapaso wa leo unapapasa huku na kule, kujaribu kuona ukubwa wenu hasa ni upi au kule kucheza michezo yenu yote ya ligi saa za jioni wakati timu nyingine, baadhi ya michezo inachezwa saa 8 mchana - jua kali ndio ukubwa wenyewe huo.

Inawezekana wengi wasinielewe nini namaanisha katika mpapaso wa leo, hasa watoto ambao ni wakubwa, wanaopenda ukubwa, japo ni watoto, lakini wakubwa waliouacha utoto, japo wanaweza kuwa wachache, hao naamini watanielewa.

Inawezekana kabisa Simba na Yanga ni wakubwa na wanastahili kujiita au kuitwa wakubwa, lakini muonekano na matendo yao kweli yanaakisi ukubwa huo?

Mkubwa anacho ambacho mtoto anapaswa kujifunza ambacho ni chema, cha maendeleo,na kwa ukubwa wake yuko tayari kumuonyesha njia na kumsaidia mtoto ili naye kwa kiasi fulani apige hatua za maendeleo.

Kwa muktadha wa mpira wa miguu, lipi hasa la kimaendeleo ambalo wadogo katika soka la nchi yetu wanaweza kujifunza na kuiga kutoka kwa wakubwa hao ili na wao kwa kiasi fulani wapige hatua za maendeleo sawa na wakubwa hao.

Miundombinu ikoje kwa wakubwa hao? Viwanja wanavyo vya mazoezi na mechi? Wanavyo japo vituo vya michezo vyenye huduma zote cha kuwaandaa kikamilifu vijana kwa ajili ya timu imara ya baadaye?

Wamejiwekezaje hasa katika masuala mazima ya soka? Wanavyo vitega uchumi vinavyowawezesha kujitegemea na kujiendesha wenyewe? Muundo wao wa uongozi ukoje? Viongozi wanaheshimiana, wanatambua na kutekeleza majukumu yao ipasavyo? Hawaingiliani katika kufanya kazi kwao? Ni vipi wanashirikishana katika kutatua changamoto kwenye timu na kupanga mikakati ya maendeleo?

Ifike wakati sasa Simba na Yanga wauonyeshe ukubwa wao kwa vitendo. Kila mtu akiona akubali kweli kwamba hao ni wakubwa katika soka la Tanzania na Afrika, wadogo wawe na cha kujifunza kutoka kwao, cha maendeleo.

Hivi kweli Kamati ya Saa 72 inatoa adhabu ya labda kushiriki vitendo vya kishirikina na uchawi hadharani wanaoadhibiwa ni Simba na Yanga yaani wakubwa, lakini mnatafuta ushindi kwa ndumba. Vitendo vya aibu hivi, wakubwa hawapaswi kuvifanya.

Kuna wakati minong’ono ya mashabiki na kauli mitandaoni iliwahi kusema na kuwapachika jina la ‘wazee wa tiGo pesa’ wakimaanisha kwamba kuna ushawishi fulani wa ushindi kwa kutumia miamala mnaoufanya ama kwa waamuzi au wachezaji wa timu pinzani ili ushindi upatikane. Rais mstaafu wa awamu ya nne aliwahi kuligusia hilo.

Kwa namna Simba na Yanga zilivyojijengea heshima katika soka la Tanzania na Afrika hazipaswi kujiingiza kwenye kashfa ya aina yoyote ile ya kisoka, hiyo inaweza kuwa moja ya sifa ya kuuelekea ukubwa ziandae timu zenye ushindani, zishinde kwa uwezo halali na wa haki.

Kuna mambo yakimtokea mtoto lazima alie hovyo, lakini yakimkuta mkubwa ni kawaida tu. Itakuwa ajabu mtoto analia, mkubwa analia, ajabu sana wakati fulani. Mkubwa analia anamtafuta mtoto amnyamazishe. Nyieeee Simba na Yanga ukubwa wenu ni upi, uonyesheni kwa vitendo isiwe tu porojo.

Columnist: Mwanaspoti