Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba Yanga, kuteleza si kuanguka

Simba SC Saa 10 Kikosi cha Simba

Sat, 18 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashindano ya klabu barani Afrika kwenye ngazi ya makundi yalitimua vumbi mwishoni mwa juma lililopita. Mashindano haya ambayo yana udhamini mnono wa Kampuni ya Nishati ya Total Energies yamekuwa na msisimko na kufuatiliwa sana kote Afrika na zaidi hapa kwetu nchini.

Ushiriki wa klabu wapinzani wa jadi Simba na Yanga zinayafanya mashindano haya yafuatiliwe kwa karibu na wapenzi wa mpira nchini.

Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku Yanga ikishiriki yanayofuata kwa ukubwa ambayo ni kombe la shirikisho.

Matokeo ya mwishoni mwa juma hayakuwa mazuri kwa timu zinazoiwakilisha Tanzania kwani Simba ilipoteza mchezo kwa kufungwa 1-0 na timu ya Horoya FC ya Guinea katika mchezo uliofanyika nchini Guinea. Young Africans (Yanga) ilipoteza kesho yake mbele ya wenyeji wao US Monastir ya Tunisia kwa mabao 2-0.

Matokeo hayo yamewanyong’onyeza wapenzi wa mpira miguu nchini kwa kufikiria kwamba, basi timu hizo zimefika mwisho wa safari yao.

Kwa bahati mbaya sana mashabiki wa klabu hizi kubwa hawakujaliwa uvumilivu na huku kila shabiki akiwa ni mtaalam na mwenye kuelewa zaidi ya benchi la ufundi pale timu inapopoteza.

Pamoja na timu hizi kupoteza vipo vitu vingi chanya vinavyoashiria kwamba ukiongezeka umakini basi klabu zetu zinaweza kufanya vizuri katika michezo iliyoko mbeleni na hata kufuzu katika hatua inayofuata.

Natiwa moyo na ukweli kwamba timu zetu zilikuwa ugenini pia na namna timu zetu zilivyomiliki michezo hiyo.

Natiwa moyo na maandalizi ya hizi timu. Natiwa moyo timu zinakwenda kucheza mbele ya mashabiki wao na zaidi natiwa moyo kuna utashi wa kisiasa kutoka upande wa serikali ili kuona kuwa timu hizi zinafanya vizuri.

Baada ya klabu za Azam na Geita Gold Mlandege na KMKM kutolewa katika hatua za chini, ni hamu ya serikali kuona timu mbili zilizobaki zinafanya vizuri.

Ukiangalia matokeo yote ya juma lililopita, utagundua kucheza nyumbani ilikuwa ni faida moja kubwa.

Karibu timu zote zilizokuwa nyumbani hazikupoteza mchezo isipokuwa Zamalek SC ya Misri iliyopoteza mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa kwa wageni wao, CR Belouizdad ya Algeria mjini Cairo. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa bado mpira wa Afrika unatawaliwa na faida ya nyumbani ambayo kama klabu za Simba na Yanga zitakuwa makini zinaweza kuitumia pia na kupambana kuambulia kitu ugenini.

Ukiangalia takwimu za Simba na Yanga katika michezo yao dhidi ya Horoya na US Monastri utaona timu hizi zilikuwa na umiliki wa zaidi ya asilimia 50 katika michezo yao jambo ambalo linaonyesha kuwa wapinzani wao waliingia na mbinu za kufunga lakini uwezo wa umiliki ulikuwa upande wa vilabu vya Simba na Yanga.

Japokuwa umiliki hautoi hakikisho la ushindi, lakini umiliki ni muhimu sana katika kutafuta ushindi. Iwapo umiliki waliokuwa nao ugenini ukihamishiwa hapa nyumbani na katika michezo inayofuata, basi Simba na Yanga bado zina nafasi ya kufanya vizuri.

Maandalizi ya klabu za Tanzania kwa mwaka huu yalikuwa ni ya kiwango cha kimataifa. Zimeondoka siku mbaya ambazo timu zilifikia siku ya mwisho wa safari za kwenda ugenini zikiwa hazina uhakika wa tiketi na hata safari za ndani ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini zilifanyika kwa mabasi. Simba iliweka kambi yake Dubai katika mwezi wa Januari huku Yanga ikiweka kambi Avic Town, kwenye Peninsula ya Kigamboni, Dar es Salaam. Pamoja na timu hizi kutofanya vema katika mchezo wa kwanza, bado yako mengi ya kuonyesha kutokana na maandalizi ya kiwango cha juu waliyoyafanya.

Katika michezo inayofuata mwishoni mwa juma hili, Jumamosi Simba itacheza na Raja Cassablanca ya ufalme wa Morocco huku Yanga ikicheza siku ya Jumapili dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Michezo yote itachezwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Kama ilivyo ada, mashabiki wa nyumbani ni moja ya faida za timu kuwa nyumbani. Iwapo Watanzania na mashabiki wa Simba na Yanga watafurika katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watu 60,000 basi milango ya ushindi inaweza kufunguka.

Wafuatiliaji wa mpira wanasema shabiki ni mchezaji wa 12 tunaamini mashabiki watajazana kuzishangilia timu hizo.

Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya shilingi tano milioni kwa kila bao litakalofungwa na timu za Simba na Yanga katika michezo yao ya wikendi hii.

Hii ni motisha kubwa sana na utashi wa ajabu kwa serikali kwani jukumu lake la kwanza ni kwenye timu za taifa lakini serikali hii iko nyuma ya klabu zinazoliwakilisha taifa na ambavyo kwa kweli zinawakilisha ‘dini’ kuu mbili za mpira katika Tanzania.

Uwanja wa nyumbani, hali ya hewa iliyozoeleka, mashabiki wa nyumbani na hamasa ya serikali zina uwezo wa kuziwezesha timu hizi kufanya vizuri kwenye michezo yao ijayo na hata kufika hatua ya juu zaidi. Dalili chanya zinaonekana. Kila la kheri Simba SC, Kila la Kheri Young Africans SC, Kila la kheri Tanzania

Columnist: Mwanaspoti