Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba, Yanga hii ndio njia ya kutoboa Nusu Fainali CAF

Simba Yanga Caf Rank Simba, Yanga hii ndio njia ya kutoboa Nusu Fainali CAF

Sat, 8 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imepewa Wydad Casablanca ya Morocco katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku watani wao, Yanga wenyewe wamepangwa kukipiga na Rivers United ya Nigeria kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya droo ilipangwa juzi usiku, jijini Cairo Misri.

Ni droo f’lani iliyowapokewa kwa hisia tofauti na wadau wa klabu hizo pamoja na makocha wa timu hizo, baada ya kuangalia rekodi za wapinzani wao hao na matokeo ya mechi zilizopita za michuano hiyo ya CAF, lakini mwishowe wakakubali kutulia na kusubiri kuona dakika 180 zitaamua nini?!

Simba itakayoanzia nyumbani kati ya Aprili 21 na 22, kabla ya kurudiana tena wiki moja baadaye jijini Casablanca, mara ya mwisho ilipokutana na Wydad ilikuwa Mei 28, 2011 katika mchezo maalumu wa play-off wa kusaka timu ya kwenda makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja huru, Simba ilichapwa mabao 3-0 na kuangukia kwenye play-off ya Kombe la Shirikisho kwa mabao ya jioni yaliyofungwa na Fabrice N’Guessi dakika ya 88, Ayoub El Khaliqi dakika ya 90+4’ na Mouhcine Iajour dakika 90+6’.

Upande wa Yanga, ilipokutana na Rivers miaka miwili iliyopita ilipasuka nje ndani, ikianza kunyukwa 1-0 nyumbani Septemba 12, 2021 kisha ikalala tena 1-0 wiki moja baadaye.

Hii ina maana Simba na Yanga zinaenda kusaka kisasi na pia kusaka tiketi za kwenda nusu fainali na kuandika rekodi mpya kwa klabu hizo kongwe nchini.

Mwanaspoti linakuletea tamu na chungu kwa mechi hizo na namna makocha wanavyozungumzia droo hiyo na walivyojipanga wakiwataka mashabiki wa timu hizo wakae kwa kutulia kwani kila kitu kinawezekana, muhimu wachezaji wajitume na kupewa sapoti ndani na nje ya uwanja wafanye kweli.

TUANZE NA SIMBA

Simba inayotinga robo fainali ya tatu katika misimu mitano iliyopita ya Ligi ya Mabingwa, itaanzia nyumbani kucheza na Wydad.

Hawa ndio watetezi wa michuano hiyo na inaonekana ni timu ngumu mbele ya Simba kwa rekodi ilizonazo, ingawa kwa msimu huu inaonyesha ndio kwanza imeanza kutulia tangu alipoondoka kocha Walid Regragui aliyewaachia taji la Ligi ya Mabingwa Afrika akienda kuifikisha timu ya taifa ya Morocco katika nusu fainali ya Kombe la Dunia kule Qatar 2022, halafu mabosi hao wakaajiri na kutimua makocha mawili tofauti.

Msimu huu ikiwa Kundi A, imeonekana kuwa hatari zaidi ikicheza nyumbani ambako imeshinda mechi zake zote tatu, huku ugenini ikipoteza moja kwa kufungwa bao la kichwa la beki wa kati ya JS Kabylie ya Algeria, huku ikitoka sare moja na kushinda mchezo mwingine mmoja.

Kwa michuano ya CAF imebeba mataji ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, 1992, 2017 na 2021-2022, pia imetwaa Kombe la Washindi mara moja 2002, ikabeba Super Cup 2018 na kwenye ligi ya kwao Batola ndio kinara ikibeba mataji 22 kama ilivyo kwa Simba katika Ligi Kuu Bara.

Kinara wa mabao wa timu hiyo ni mshambuliaji raia wa Senegal, Bouly Sambou mwenye mawili, huku beki wa kati Mkongomani Arsene Zola, Yahya Jabran na winga wao wa kushoto Zouhair El Moutaraji wote wakifunga moja-moja.

Simba kama inataka kupata matokeo kuanzia mchezo wa kwanza inapaswa kuilazimisha Wydad ifanye makosa kwani safu yao ya ulinzi licha ya kuruhusu bao moja tu, lakini mabeki wao wamekuwa wakifanya makosa na Wekundu wakitulia wanaweza kuwanyamazisha.

Ubora mkubwa wa Wydad upo eneo la kiungo na ile ya ushambuliaji ambako kiungo hatari ni Aymane El Hassaoun ambaye amekuwa ndio injini ya kutengeneza pasi za mabao akitokea katikati huku beki wao wa kulia Ayoub El Amloud akiwa ndio kinara anayejua kupandisha mashambulizi makali sambamba na kuzalisha krosi nyingi za mabao.

Mbali na hao pia wana winga wa kushoto Saif Bouhra ambaye ndio injini ya kutengeneza mashambulizi akitokea kulia lakini baadaye wanamuingiza winga mwingine wa kulia Abdellah Haimoud akitokea benchi.

Dakika zao za hatari za mabao inategemea na makosa ya wapinzani, ila inafunga sana kipindi cha pili, kwani katika mabao saba iliyovuna kwenye makundi imefunga mawili tu kipindi cha kwanza katika dakika za 34 na 38, huku mengine matano yakifungwa kipindi cha pili katika dakika za 51, 55, 59, 87, 90.

Thamani nzima ya kikosi cha Wydad ni Euro 19.2 milioni (sawa na Sh 49 bilioni) na mchezaji ghali zaidi ni kipa Ahmed Reda Tagnaouti ambaye ana thamani ya Euro 1.8 milioni (sawa na Sh5 bilioni), kulinganisha na Simba ambayo kwa mujibu wa mtandao wa www.trasfermarkt.com, thamani ya kikosi cha Simba ni Euro 2.23 milioni (sawa na Sh5.6 bilioni) na Saido Ntibazonkiza akiwa ndiye mwenye thamani zaidi akiwa ni Euro 550,000 (sasa Sh1.4 bilioni)

Kocha wa Simba, Robertinho aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya droo hiyo kuwakutanisha na Wydad lakini bado Simba ina nafasi ya kusimama kwenye malengo yake ya kucheza nusu fainali.

Robertinho alisema kwa sasa anaingia msituni kuanza kuwapigia hesabu Wamorocco kwa kuwatafutia mfumo sahihi wa kuwafunga nyumbani kisha watue kwa mkakati maalumu watakapocheza ugenini.

“Hii ni hatua ngumu, kila timu iliyofika hapa inastahili heshima, tunawaheshimu Wydad lakini narudia Simba haiwezi kuogopa mpinzani yeyote, tumeanza kutafuta mbinu na mfumo sahihi wa kutumia kwenye hizi mechi mbili, nafikiri kila kitu kinawezekana,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Tutacheza mechi ya kwanza nyumbani hapa tutakuwa na wachezaji kumi na mbili nikimaanisha wale kumi na moja kutoka kwangu na mashabiki wetu. Tunatakiwa kushinda kwa kutangulia kucheza kwa nidhamu wakati tukiwa na mpira na wakati hatuna mpira, kitu muhimu sana ni kutumia nafasi na baada ya hapo tutaangalia tukacheze nao vipi kule kwao.”

YANGA SASA

Yanga pia ina mechi ya kisasi na tayari klabu hiyo imekuja na kauli mbiu ya mchezo huo isemayo ‘Kisasi ni Haki’ kwani inakutana na Rivers United iliyowatibulia msimu uliopita kwa kung’oa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-0.

Katika msimu huu, Yanga itaanzia ugenini Aprili 23 kisha kumalizia nyumbani Aprili 30 ikiwa na akili moja tu ya kutaka kulipa kisasi na kuandika historia ya kutinga nusu fainali ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza tangu ianze kushiriki michuano ya Caf mwaka 1969.

Rivers iliyomaliza nafasi ya pili kwenye Kundi B, haina maajabu makubwa kulinganisha na Yanga ambayo ilikutana mara ya mwisho Septemba 19, 2021 kwenye Uwanja wa Yakubu Gowon, jijini Port Harcourt, Nigeria ila safari hii zitalazimika kuhama mji mwingine.

Hii ni kwa sababu Rivers imetakiwa kutumia Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio uliopo mji wa Uyo makao makuu ya Akwa Ibom ambao pia unatumiwa na timu ya taifa hilo Super Eagles.

Rivers iliyoanzishwa mwaka 2016 ikifahamika kama Sharks FC kisha kujiita Dolphins kabla ya kujipachika jina hilo jipya, imekuwa na kikosi chenye mabadiliko makubwa msimu huu kikionekana bora tofauti na Yanga inavyowachukulia.

Wanigeria hao changamoto kubwa kwao ni ukuta wao kwani wamekuwa wakifanya makosa na ndio maana katika mechi tatu za ugenini wamepoteza mbili (3-0 v Diadles Noirs na 1-0 v Asec), huku nyumbani wakishinda pia mbili na zilizosalia wakiambulia sare kotekote. Ilishinda ugenini 1-0 dhidi ya DC Motema Pembe.

Katika mechi mbili ilizoshinda nyumbani imewapiga wageni kwa mabao matatu matatu ikishinda 3-0 na 3-1, huku sare ikiwa ni ya mabao 2-2, kuonyesha namna gani timu hii inatafuta mabao na kuyatupia kambani, kitu ambacho Yanga ni lazima ianze kujiandaa mapema kwa sasa.

Ngome ya timu hiyo imeruhusu mabao sita na safu yao ya ushambuliaji ikifunga mabao tisa katika mechi zao sita za makundi hatua ambayo itawapa nguvu washambuliaji wa Yanga kutakiwa kutulia kutengeneza mabao yao wakitumia makosa ya wapinzani wao kwenye ulinzi.

Staa wao mkubwa ni kiungo mshambulaiji Paul Acquah, ambaye ana hat-trick moja aliyowapiga Motema Pembe kwenye makundi na kumfanya awe na mabao manne akiwa kinara wa michuano hiyo akilingana na Aubin Kramo Kouame wa Asec Mimosas na Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini.

Pia ndiye kinara wa kikosi hicho cha Rivers akifuatiwa na Nyima Nwagua aliyefunga mawili, hivyo mabeki wa Yanga wanapaswa kumchunga Acquah ambaye amekuwa na makali ya kufunga kwa miguu yote na hata kichwa licha ya kimo chake cha 1,84 mita huku Nwagua akiwa na mwili mkubwa, nguvu na kasi akiwa na mpira.

Timu hiyo imekuwa haitabiriki katika mabao yao wakifunga vipindi vyote, lakini ni hatari zaidi kipindi cha pili kwani kati ya mabao tisa iliyofunga makundi, sita imeyakwamisha wavuni kipindi cha pili katika dakika za 48, 53, 56, 73, 77 na 90+3, wakati matatu ni ya kipindi cha kwanza katika dakika za 1, 42 na 45+2.

Utamu zaidi ni kwamba kwenye mechi ya msimu huu, Rivers inakutana na nyota wanne wa Yanga waliokuwepo kwenye mechi ya mwisho ambao ni kipa Djigui Diarra, mabeki wakiwa ni nahodha, Bakar Mwamnyeto na Dickson Job sambamba na winga Jesus Moloko.

Yanga ikitoboa mbele ya Rivers na kwenda nusu fainali itavaana na mshindi kati ya Pyramids ya Misri au Marumo Gallants ya Afrika Kusini na Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi akizungumzia droo hiyo kwa njia ya simu kutoka Ubelgiji alisema, ingawa wanajipanga kulipa kisasi dhidi ya Rivers lakini wanatakiwa kuwa na tahadhari kubwa dhidi ya wapinzani wao hao kwa kuwa wamekuwa na timu yenye mabadiliko makubwa.

“Hakuna timu nyepesi hatua hii, nafikiri hatutakiwi kushangilia sana kukutana na Rivers kitu bora ambacho kinatakiwa kufanyika ni kuanza kupiga hesabu za mechi hizi haraka, tunaendelea kukusanya taarifa zao lakini pia nitakutana na viongozi wa klabu kuanza kupanga mikakati,” alisema Nabi ambaye alikuwa kocha wakati Rivers ikimng’oa.

“Tuna kikosi bora lakini kama tutaingia na akili ya kuona mechi ni rahisi tutakutana na mshtuko, hili nitazungumza na wachezaji wangu, kitu bora hapa ni kuhakikisha tunakuwa na utulivu katika kuzicheza mechi hizi mbili kwa ubora mkubwa.

Columnist: Mwanaspoti