Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba, Yanga balaa, nusura zicheze siku mbili mfululizo

Uwanjaaaaaaa.jpeg Simba na Yanga ni wapinzani wa Jadi katika Soka la Tanzania

Sun, 16 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ilikuwa Juni 4, 1972 katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijni Dar es Salaam. Ulichezwa mchezo wa kusaka bingwa wa Kombe la Karume, Bingwa wa Tanzania, kati ya Simba na Yanga. Zamani Ligi ilikuwa inachezwa kwa makundi na hatimaye kuwa na robo fainali na hatimaye fainali. Hii ilikuwa fainali.

HAKUNA MBABE

Juni Mosi, Simba ilikuwa ya kwanza kutinga katika hatua ya fainali baada ya kuifunga timu kutoka Iringa ya African Wonders mabao 5-0 katika nusu fainali ya kwanza. Juni 3, Yanga ilifuta baada ya kuitandika African Sports ya Tanga mabao 3-1 katika mchezo wa nusu fainali ya pili.

Wakati huu Simba ilikuwa ni bingwa wa Mkoa wa Pwani na Yanga walikuwa mabingwa watetezi wa Tanzania.

Mbungi ilipigwa katika uwanja huo, lakini hadi mwisho hakukuwa na mbabe. Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Willy Mwaijibe.

Ilikuwa kazi nzuri iliyofanywa na Emmanuel Arbert Mbele (hataki kuitwa Dubu) alikokota mpira na kupiga krosi iliyotua kichwani kwa mfungaji na kuandika bao la kuongoza.

Katika dakika ya 19, Maulid Dilunga aliambaa ambaa na mpira na kumhadaa beki wa Simba, Shaban Baraza. Dilunga alipiga hatua kadhaa na kuachia krosi iliyomkuta Kitwana Manara aliyeukwamisha wavuni kwa guu lake la kulia.

Hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

DAKIKA 30 ZA NYONGEZA

Katika dakika za nyongeza bado timu hizo hazikuweza kufungana pamoja na Adamu Sabu ‘Gerd Muller’ kuikosesha Simba bao la wazi.

Mashabiki wa Simba walishasimama kutaka kushangilia bao baada ya Sabu kuwapiga chenga mabeki wawili wa Yanga, Gobbos na Kapera lakini alishindwa kulenga lango la Yanga. Mwamuzi Manyota Ndimbo akapuliza filimbi ya kumaliza mchezo.

Katika dakika za mwisho kabisa mchezo ulitibuka na wachezaji wa pande zote mbili wakaanza kuonyeshana ubabe.

Ilikuwa ni mwendo wa kutembezeana buti na hata kutaka kuchapana makonde. Lakini kipyenga cha Manyota Ndimbo kilimaliza mchezo huo bila ya kupata mshindi.

Kutokana na mwanga hafifu uliokuwapo uwanjani, timu hizo hazikuweza kupigiana mikwaju ya penalti. Vikosi vya timu vilikuwa hivi. Yanga: Eliaas Michael, Athuman Kilambo, Ali Yusufu/Selemani Sanga, Hassan Gobbos, Adam Juma, Omari Kapera, Leonard Chitete, Sunday Manara, Abdulrahman Juma (nahodha), Maulid Dilunga na Kitwana Manara.

Simba: Lucas Semainda, Shaban Baraza, Mohammed Kajole, Khalid Abeid, Omari Chogo, Willy Mwaijibe, Haidar Abeid, Adam Sabu, Abdallah Kibadeni, Juma Mzee (nahodha) na Emmanuel Albert.

NGOMA YAHAIRISHWA

Juni 6, Chama cha Soka cha Tanzania (sasa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF) kilitoa taarifa ya kuahirishwa mchezo huo hadi Juni 18. Taarifa ilitolewa na Katibu Mtendaji wa chama hicho, Martin Mgude.

Katibu huyo alisema sababu za kuahirishwa kwa mchezo huo ni kuwapa nafasi wajumbe kuanza safari ya kwenda Mkoa wa Mara kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Tatu wa Halmashauri Kuu ya FAT uliokuwa unafanyika mjini Musoma Juni 10 hadi 11.

YANGA ILIOMBA POO

Lakini habari zilizopatikana baadaye zilisema hata kabla ya FAT kuahirisha mchezo huo, klabu ya Yanga ilishaandika barua FAT na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuomba mchezo huo usogezwe mbele kwa madai wachezaji wao wengi walikuwa majeruhi.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Yanga kuandika barua kwa FAT na BMT kuomba kusogezwa mbele kwa mchezo wa timu hizo zenye utani wa jadi. Awali Yanga iliomba kusogezwa mbele kwa mchezo uliopigwa Juni 4 na kutoka sare ya bao 1-1 kwa madai kama hayo.

Hata hivyo, FAT na BMT zilikataa ombi hilo la awali na kuitaka timu hiyo yenye masikani yake Jangwani kufika uwanjani bila ya kukosa.

MAJERUHI 10 WA YANGA

Katibu Mwenezi wa Yanga, Mshindo Mkeyenge alisema wachezaji 10 wa Yanga walikuwa wameumia na walitakiwa kupatiwa matibabu kwa takribani kwa muda wa wiki mbili.

Mkeyenge alifafanua kwamba, wachezaji hao walipata majeraha wakati Yanga ilipocheza dhidi ya Nyota Afrika (ya Mtwara) katika hatua ya robo fainali na African Sports (ya Tanga) kwenye hatua ya nusu fainali. Mkeyenge alisema sio kama walikuwa wakiogopa kucheza dhidi ya watani wao wa jadi, la hasha, bali walizingatia maumivu waliyokuwa wakiyasikia wachezaji wao.

SIMBA WAIKEBEHI YANGA

Meneja wa Simba, N. Marwa aliibuka na kuwaambia Yanga walikosea kuandika barua FAT na BMT kuomba kusogezwa mbele kwa mchezo huo.

Marwa alisema, viongozi wa Yanga walipaswa kuwatumia ujumbe wenzao wa Simba na kuzungumza nao kwa sababu ni rafiki zao na wangefikia mwafaka wa suala hilo.

“Iwapo viongozi wa Simba na Yanga wangejadiliana kwanza na kufikia mwafaka mchezo usifanyike, ingekuwa rahisi kwa wahusika kuuvunja hata kama maandalizi yalikuwa yameshafanyika,” alisema Marwa. Je, mshindi wa Kombe la Karume, Bingwa Tanzania mwaka 1972 alikuwa nani? Na nini kilitokea? Usikose kusoma makala zetu upate kujua kama mchezo ulichezwa ama la!

Columnist: Mwanaspoti