Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba, Yanga! Do or Die

Simba SC Squad List Kikosi cha Simba SC

Sat, 25 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba na Yanga zinakabiliwa na mechi muhimu ugenini mwishoni mwa wiki hii katika mashindano ya klabu Afrika dhidi ya timu za Vipers ya Uganda na Real Bamako ya Mali.

Katika Uwanja wa St. Mary’s Kitende, Simba ikiwa Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika itakabiliana na Vipers, Jumamosi kuanzia saa 1:00 usiku na Jumapili kwenye Uwanja wa Machi 26 (Stad du 26 Mars) mjini Bamako, Mali, Yanga itakabiliana na Real Bamako katika mechi ya Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia saa 1:00 usiku.

Simba inahitaji ushindi dhidi ya Vipers ili ifikishe pointi tatu ambazo zitaweka hai matumaini yake ya kuwa miongoni mwa timu mbili za kundi lake zitakazocheza hatua inayofuata.

Yanga inayoshika nafasi ya pili, inahitaji ushindi kujichimbia katika nafasi ya pili ama kwenda kileleni mwa kundi hilo kutegemeana na matokeo ya mechi ya Mazembe na Monastir. Haitakuwa michezo rahisi kwani ni kama vita ya kufa au kupona na kuna mambo zinapaswa kufanya ili kila moja ipate pointi tatu za kupaweka pazuri katika makundi.

SIMBA

Simba haitakuwa na kibarua chepesi dhidi ya Vipers kutokana na ubora ambao wapinzani wao hao wamekuwa nao lakini pia mwenendo usioridhisha walionao wawakilishi hao wa Tanzania katika mechi za hivi karibuni.

Uimara wa Vipers upo katika safu ya kiungo ambayo inaundwa na wachezaji wepesi wa kufanya uamuzi pindi wawapo na mpira lakini wana uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kupiga pasi ambazo zimekuwa zikifikia walengwa kwa usahihi.

Eneo la kiungo la Vipers ndio limekuwa likitegemewa na timu hiyo kuzalisha mabao na timu inayofanikiwa kuwadhibiti hasa Bright Anukani ina nafasi ya kupata matokeo mazuri.

Kuthibitisha hilo, katika mabao manane ya Vipers kwenye mechi 10 zilizopita, matano yamefungwa na viungo na matatu yamefungwa na washambuliaji.

Kuanza na washambuliaji wawili kunaweza kuwa na faida kubwa kwa Simba dhidi ya wapinzani wao hao kwani Vipers imekuwa na changamoto ya mawasiliano duni ya safu yake ya ulinzi hasa mabeki wa kati, hivyo hufanya makosa ambayo yamekuwa yakiwagharimu dhidi ya timu pinzani.

Kutumia washambuliaji wawili wa kati, kutaiweka Simba katika nafasi nzuri ya kuvuruga muundo wa kiulinzi wa Vipers na kuwanyima utulivu mabeki wake wa kati ambao wamekuwa wakifanya makosa pindi wanashambuliwa.

Simba pia inapaswa kujipanga kumdhibiti mshambuliaji na nahodha wa Vipers, Milton Kalisa ambaye ana kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki, kukokota mpira, kupiga chenga na kufunga mabao.

YANGA

Ina nafasi kubwa ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Real Bamako, Jumapili na hata katika mechi ya marudiano hapa Dar es Salaam, Machi 8 mwaka huu.

Hii ni kutokana na Real Bamako kutokuwa tishio sana kwa staili ya kiuchezaji wala kuwa na wachezaji wenye ubora wa hali ya juu ambao wanaweza kuipa ugumu Yanga kulinganisha na TP Mazembe au Monastir.

Kitu ambacho kinaweza kuisumbua Yanga ni soka la pasi za taratibu ambalo ndilo limekuwa uimara wa Real Bamako katika mechi zake nyingi msimu huu na hata mabao yake mengi imeyapika kwa kutumia staili hiyo.

Timu hiyo pia ina washambuliaji wenye uchu ambao huwa hawafanyi ajizi kufumania nyavu ikiwa safu ya ulinzi ya timu pinzani inafanya makosa na wamekuwa wazuri katika kutumia nafasi chache wamezozitengeneza.

Lakini kinyume chake, Real Bamako imekuwa na udhaifu ambao kama Yanga ikiutumia vyema inaweza kuwafanya ipate matokeo mazuri dhidi ya timu hiyo ya Mali.

Real Bamako sio wazuri kuzuia mipira ya krosi hasa zile za juu lakini pia viungo wake wamekuwa wakiachia mianya ambayo hutumiwa na wapinzani kuwamaliza.

Yanga inaweza kutumia vyema presha ambayo Real Bamako imekuwa nayo kwa sasa kutokana na mwendelezo wa kutopata matokeo yasiyoridhisha kuimaliza timu hiyo ya Mali, kwani wapinzani wao hao, wamecheza mechi tatu mfululizo bila kupata ushindi, wakipoteza mbili na kutoka sare moja.

ROBERTINHO, NABI FRESHI TU

Makocha wa Simba na Yanga, Nasreddine Nabi na Roberto Oliveira wametamba kupata ushindi katika mechi hizo.

“Ushindi dhidi ya TP Mazembe unaongeza hamasa na morali kwa wachezaji kwa mechi dhidi ya Real Bamako. Ni mechi ngumu lakini nina imani tukiwa na muendelezo wa kile tulihokifanya katika mechi iliyopita, tutapata ushindi,” alisema Nabi.

Robertinho kwa upande wake, alisema: “Ninaifahamu vizuri Vipers na nimefanya kazi pale. Nawaamini wachezaji wangu na najua watapambana kufanya vyema katika mechi hiyo muhimu.”

Columnist: Mwanaspoti