Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba, Namungo mtuwakilishe vizuri

Simba+namungo+pic Simba, Namungo mtuwakilishe vizuri

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa Simba na Namungo zitakuwa zina kibarua kizito wikiendi hii kuhakikisha zinapambana kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya nchi.

Namungo itaikaribisha Al Rabita ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi leo saa 1:00 usiku, huku Simba ikitarajiwa kucheza kesho ugenini nchini Nigeria dhidi ya Plateau FC.

Timu ya Namungo ilipata nafasi ya uwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushika nafasi ya pili Kombe la FA, huku Simba ikiwa bingwa msimu uliopita.

Kadhalika, Simba kwa sababu ilitwaa taji la Ligi Kuu ikabidi iwakilishe Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu hizi zote hakika zinatazamwa na mashabiki wa soka nchini ikitarajiwa zitafanya kazi nzuri siyo tu kuwakilisha bali kushindana na kupata kile inachostahili.

Ni wazi kwamba kila timu inajua namna mashindano hayo makubwa barani Afrika yalivyo, kwa maana siyo ya mchezo yanahitaji vikosi vipana, yanahitaji nguvu na maandalizi.

Katika suala la maandalizi timu zote mbili zilijiandaa kabla hata ya kuanza kwa ligi zikiwa zimesajili wachezaji wa kutosha wenye uwezo wa kuibeba timu.

Ukija upande wa Namungo inayowakilisha kwa mara ya kwanza michuano hiyo ikitokea kule mkoani Lindi, inatarajiwa kikosi walichosajili kitaleta ushindani kwa kupambana kupata matokeo ili watakapokwenda ugenini basi wamalize salama na kuvuka hatua moja kwenda nyingine.

Jambo zuri kwao ni kwamba wamesajili wachezaji wengi ambao wengine walishapata uzoefu kutoka baadhi ya timu za Ligi Kuu walikotoka na wengine ni wa kimataifa wana uzoefu kwenye timu zao za taifa.

Aidha, kocha wake Hemed Morocco sio mgeni na michuano ya kimataifa kwa sababu aliwahi kuwa Kocha wa timu ya taifa Zanzibar na Tanzania hivyo, ni wazi atajua namna gani ya kukiandaa kikosi chake.

Wanachotakiwa kufanya Namungo ni kujiandaa vizuri na kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia na kutambua kwamba kama ambavyo wamekuwa wakikutana na Simba na Yanga ndivyo ambavyo ushindani wao unatakiwa kuhamia huko kimataifa. Kikosi hicho kilionesha mchezo mzuri katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga ambapo walitoka sare ya bao 1-1.

Bila shaka kile walichokionesha watakifanya na leo. Kwa upande wa Simba wana uzoefu mkubwa na michuano ya kimataifa inategemea wamejiandaaje kimbinu dhidi ya wapinzani wao.

Katika misimu mitatu mfululizo waliyofanikiwa kucheza michezo ya ugenini ya kimataifa hawakuwa na matokeo mazuri sana na pengine watakuwa walijifunza kwa hiyo hakuna anayetarajia kuona wanarudia makosa. Simba ina wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu mkubwa na hilo halina shaka kwamba wanategemewa kuwakilisha vizuri.

Kocha wao Sven Vande- broeck anajua wachezaji wake tangu msimu uliopita amekuwa akifanya nao kazi. Watu wanataka kuiona Simba ile iliyoweka historia msimu wa mwaka juzi kwa kufika nane bora.

Basi ikiwezekana mwanzo mzuri kwao utawezesha kufika tena huko na pengine kuvunja rekodi. Timu zote mbili zinapaswa kutambua zinahitaji kuwa na nidhamu ugenini kwa kuheshimu wapinzani na kupambana kama siyo kupata sare, basi iwe ni ushindi ili zinapokuwa nyumbani watumie kuwa machinjioni.

Kwa Simba wanaelewa kwa sababu mwaka juzi licha ya kwamba walikuwa wanapata matokeo mabaya ugenini, nyumbani walijitahidi kushinda mechi zao zote.

Columnist: habarileo.co.tz