Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba Day ilikuwa zaidi ya tamasha

Simba Day Simba Day ilikuwa zaidi ya tamasha

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SAHAU matokeo yaliyotokea kwa Simba kufungwa bao 1-0 na TP Mazembe kwenye Simba Day juzi pale Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini yote kwa yote siku ile ilikuwa zaidi ya tamasha kutokana na burudani na uhondo walioupata mashabiki wa timu hiyo.

Picha lilianza mapema saa 1:00 asubuhi tayari mashabiki wa Simba walikuwa wamefika uwanjani kwa ajili ya tamasha lao na wengine walilala uwanjani hapo ili kuhakikisha hawapitwi na lolote.

Mwanaspoti kama kawaida halina shughuli ndogo, timu ilikuwa pale kukuletea kila kitu kinachojiri na lilishuhudia maeneo ya ndani na nje ya Uwanja wa Mkapa kukiwa kumejaa rangi nyekundu, nyeupe na bluu nyeusi ambazo ni jezi za Mnyama.

Nao wafanyabiashara walipiga mkwanja wa kutosha - sio wauza jezi, bodaboda, mamantilie, baa na hata wauza maji kila mtu aliondoka na kibunda cha maana.

Polisi na idara zote za usalama hazikuwa mbali. Zilihakikisha kila jambo linakwenda kama lilivyopangwa na kwa kiasi kikubwa walifanikiwa.

Kufikia saa 8:00 mchana tayari mashabiki wa Simba walikuwa wameujaza Uwanja wa Mkapa na tiketi zote zilikuwa zimekwisha, huku nje ya uwanja huo kukiwa na nyomi la mashabiki ambao walikuwa wanaendelea kuingia ndani na wengine wakiendelea na burudani kadha wa kadha kwenye baa za nje ya uwanja.

WASANII WALIKIWASHA

Sambamba na kuwepo kwa burudani kibao, wasanii wa muziki ni miongoni mwa watu walioingezea thamani na ubora Simba Day.

Meja Kunta alipiga singeli la kufa mtu. Joh Makini na Lord Eyes waliingia na bajaji kila mtu na yake na kukiwasha kinoma na ngoma zao kama Gere, Wapolo na Show time.

Marioo alifunika kinoma baada ya kuingia na bodaboda ya matairi manne huku akisindikizwa na ‘wahuni’ wanne waliokuwa na pikipiki za matairi mawili. Hao jamaa shoo yao usipime. Hizo pikipiki waliziendesha walivyotaka wao - mara wanyanyue tairi la mbele, mara la nyuma mara wakae, mara wasimame! Jamaa walitisha huku wakisindikiza ngoma kali za Marioo.

Profesa Jay kama kawaida hakuharibu na kingine mwamba huyu ndiye aliyetambulisha kikosi cha Simba sambamba na Mpoki wa Ze Comedy ambao walipiga kolabo la kibingwa.

MCHEZO WENYEWE

Mchezo ulianza kwa timu zote kucheza taratibu na kadri muda ulivyozidi kwenda kila timu ilikuwa ikitafuta bao, lakini hadi dakika 46 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakuna timu iliyokuwa imepata bao.

Katika kikosi cha Simba wachezaji wawili - Sadio Kanoute na Kibu Denis ndio wapya walioanza huku wengine wakiwa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein “Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Rally Bwalya Chris Mugalu na Benard Morrison ambao walikuwepo msimu uliopita.

Burudani kubwa ilikuwa kwenye eneo la kiungo ambapo Kanoute, Lwanga na Bwalya walikutana na changamoto kubwa ya viungo wa TP Mazembe wakiongozwa na fundi Kouame Koffi aliyekuwa bora zaidi.

Pia, TP Mazembe walionekana kuwa bora kuwatumia mawinga wa kushoto ambao walivuruga kabisa mfumo wa kocha wa Simba, Didier Gomes kwa kuwazuia Tshabalala na Kapombe kupanda mbele ili kuongeza nguvu kwenye mashambulizi kwani muda wote walijikuta wakikaba.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kwa Simba kuwaingiza Pape Sakho, Peter Banda, John Bocco, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Duncan Nyoni, Meddie Kagere na Henoc Baka wakitoka Kibu, Tshabalala, Kapombe, Mugalu, Bwalya, Kanoute na Lwanga .

Baada ya mabadiliko hayo Simba ilihama kutoka kwenye mfumo wa 4-4-2 na kucheza 3-5-2 lakini ilionekana kwamba ilichelewa kwani ilifanya hivyo baada ya kupigwa bao kali la kideoni na Jean Baleke aliyefunga dakika ya 84.

Hata hivyo, ubora wa Simba ulionekana kwani iliendelea kucheza kwa mfumo uleule uliozoeleka kwani katika mchezo huo ilikuwa ikicheza pasi fupifupi nyingi kama ilivyokuwa ikicheza msimu uliopita.

Huenda Simba ikaimarika zaidi mbele ya safri na kutisha katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara kwa kuwa wachezaji wote wapya na waliokuwepo msimu uliopita wanaonekana kuwa na vipaji vikubwa na kazi kubwa itakuwa kwa kocha Gomes kuamua amtumie nani na kwa mechi gani.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz