Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siku ya mazingira Duniani na vita kutokomeza COVID-19

MAZINGIRA NEW 770 770shar 50brig 20 C1 C T.png Siku ya mazingira Duniani na vita kutokomeza COVID-19

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KILA tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Sikuya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaliamuliwa mwaka 1972 katika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu masuala ya Mazingira, uliofanyika katika Mji wa Stockholm nchini Sweden.

Mkutano huo uliazimia kwamba tarehe 5 Juni, kila mwaka iwe ni siku ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali na umuhimu wa hifadhi ya mazingira katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,

kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za hifadhi ya mazingira na mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Upotevu wa bioanuai, uharibifu wa tabaka la ozone, na shughuli nyingine mbalimbali zinazochangia uharibifu wa mazingira

Akiongea katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu alisema kuwa Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za kimazingira.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na uharibifu wa ardhi, ufyekaji na uharibifu wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini na upotevu wa bioanuai. Changamoto hizi kwa ujumla zinasababisha athari kubwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii.

Katika kukabiliana na changamoto hizi serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kupambana na hali hii.

Mojawapo ya njia za kupambana na changamoto hii ni kutumia Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ili pamoja na mambo mengine kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.

Kaulimbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Kaulimbiu hii inaakisi hali halisi ya nchi yetu kuathirika na

mabadiliko ya tabianchi. Katika miaka ya hivi karibuni nchi imeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ukame mkali na wa mara kwa mara pamoja na mafuriko ambayo yamekuwa yakiikumba nchi yetu na kusababisha hasara kubwa ya miundombinu, makazi ya watu na hata vifo katika baadhi ya sehemu.

ATHARI ZAKE

Hivi karibuni mafuriko yaliyoukumba mkoa wa Lindi na kusababisha hasara kubwa, takriban vijiji 16 viliathiriwa na mafuriko hayo pamoja na watu 19 kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo.

Aidha, takriban watu 15,000 wamekosa makazi pamoja na uhaba wa chakula na kuathiriwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kutumia mbinu mbalimbali za asili na za teknolojia rafiki za kuhifadhi mazingira ikiwemo kilimo cha matone, nishati mbadala, ufugaji wa mifugo chotara na upandaji wa miti ya asili kwenye vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Katika Taarifa hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu, aliongeza kuwa Tanzania na dunia kwa ujumla, zinakabiliwa na janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watu. Uwepo wa janga hilo, umesababisha kusitishwa kwa shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu.

Aidha, kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kwamba mwaka huu hapatakuwapo na mikusanyiko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa, yaliyopangwa kufanyika mkoani Lindi.

Kwa muktadha huo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, wamekubaliana kuwa maadhimisho ya wiki ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizo ya ugonjwa wa corona.

Aidha, kila mkoa utafanya shughuli za maadhimisho hayo kwa kutumia vyombo vya habari vilivyopo kwenye maeneo yao pamoja na mitandao ya kijamii kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na:

mashindano ya kuandika insha zinazohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hotuba za viongozi, ujumbe mbalimbali utakaotumwa kwenye mitandao ya simu pamoja na mikutano ya kitaalamu kuhusu mabadiliko ya tabianchi itakayofanywa kwa njia ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizo ya ugonjwa wa corona.

MKUU WA NEMC

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dk. Samuel Gwamwaka, katika kuadhimisha Siku ya Mazingira ya Duniani aliwasisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti,kutunza vyanzo vya maji na kuzingatia kwa umakini sheria na taratibu za kuhifadhi mazingira ili kuepuka athari ziletwazo na mabadiliko ya tabianchi.

“Tuendelee kuyatunza mazingira yetu kwa kutunza vyanzo vya maji maana vingi vimeharibiwa, tuache kukata miti, ili kuepuka madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dk. Gwamwaka.

Inafahamika, hifadhi ya mazingira si kazi ya serikali pekee yake bali ni jukumu la kila mmoja katika jamii. Kila mmoja katika kaya ana wajibu na fursa muhimu ya kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira kitaifa.

Kushirikiana , inahusu masuala kama kupambana na kukabilianadhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, kila mwananchi ana wajibu katika nafasi yake, kulinda mazingira kwa ujumla.

Mkuu wa NEMC anakumbusha shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira nchini mwaka huu, zitalenga kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuelimishana jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Columnist: www.tanzaniaweb.live