Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siku ya Wanawake na dhana ya UN katika uongozi

E8f4e017c95fb33e33c311a074036981 Siku ya Wanawake na dhana ya UN katika uongozi

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KILA tarehe 8 Machi, yaani siku kama ya juzi Jumatatu dunia huadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Siku hii huadhimishwa kukumbuka tukio la tarehe 28 Februari, 1909 kule New York nchini Marekani ambapo wanawake waliandamana kutaka malipo ya mshahara sawa na wanaume kutokana na wao kufanya kazi sawa na walizokuwa wakifanya wanaume.

Baadae, Chama cha Kijamaa nchini Marekan kikaamua kuiadhimisha siku hii tarehe 8 mwezi Machi, 1909 na ndipo tarehe hii ikachukuliwa kama tarehe ya kimataifa ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Tanzania nayo ikiwa sehemu ya jamii nayo imekuwa ikadhimisha siku hii kwa matukio mbalimbali yakiongozwa na wanawake.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni, "Wanawake katika Uongozi chachu ya kufikia Dunia yenye Usawa."

Kaulimbiu hii inaleta maswali kadhaa kwa kuzingatia mikataba inayoongoza na kuelekeza hatua mbalimbali za kufuatwa ili kupinga na kuondoa ukandamizaji dhidi ya wanawake na hatimaye kuleta usawa katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa nini nasema inazua maswali kadhaa? Tukumbuke mwezi Desemba, 1979 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio namba 34/180 lililozalisha Mkataba wa Kimataifa unaopinga aina zozote za Ukandamizaji dhidi ya wanawake kwa kifupi CEDAW. CEDAWA ilianza kufanya kazi rasmi tarehe 3 Septemba mwaka 1981.

Mkataba huu ulizitaka nchi wanachama kufanya yafyatayo: Mosi, kuweka kanuni ya usawa baina ya wanawake na wanaume katika Katiba za nchi zote wanachama, sambamba na kuweka mazingira mazuri kuhakikisha kanuni hiyo inatekelezwa.

Pili, kupitisha, kuweka na kuchukua hatua mahususi za kikatiba ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo dhidi ya wanaokandamiza wanakwake, lengo likiwa ni katika kuzuia aina yoyote ya ukandamizaji dhidi ya wanawake.

Tatu, kuweka ulinzi wa haki za wanawake katika misingi ya usawa na wanaume kupitia mamlaka/mahakama zenye uwezo wa kisheria na taasisi nyingine za serikali ili kuwalinda wanawake dhidi ya aina yoyote ya ukandamizaji.

Nne, kujizuia kutokana na kujihusisha na kitendo chochote au tamaduni zinazokandamiza wanawake na kuhakikisha mamlaka zinazoshughulika na umma na taasisi zote zinaendana na wajibu huu.

Tano, kuchukua hatua stahiki kuondoa aina yoyote ya ukandamizaji dhidi ya wanawake kwa mtu mmoja mmoja, shirika au kampuni.

Sita, kuchukua hatua zote stahiki ikiwa ni pamoja na kutunga sheria, kurekebisha na kuondoa sheria zilizopo sambamba na kanuni zinazochangia ukandamizaji dhidi ya wanawake.

Saba, kuondoa vifungu vya sheria ambavyo vinachagia ukandamizaji dhidi ya wanawake.

Haya yameelezwa katika ibara ya 2 ya Mkataba wa Kupinga Aina Zozote za Ukandamizaji dhidi ya Wanawake, yaani CEDAW.

Ili kuleta yaliyomo katika CEDAW katika muktadha wa Afrika, tarehe 11 Julai, 2003 Umoja wa Afrika ulipitisha Azimio lililozaa Nyongeza ya Mkataba unaohusu haki za Wanawake katika Mkataba wa Afrika Unaohusu Haki za Binadamu na Watu yaani Protocol on the African Charter on Human and People's Rights on the Rights of Women in Africa.

Mkataba huu unajulikana zaidi kama Mkataba wa Maputo kuhusu Haki za Wanawake Afrika.

Mkataba wa Maputo ulirejea Azimio namba AHG/Res. 240 (XXX1) lililotokana na kikao cha kawaida cha wakuu wa nchi na serikali barani Afrika kilichokutana mwezi Juni, 1995 Addis Ababa kufuatia kuandaliwa kwa makubaliano ya awali jijini Lome, nchini Togo mwezi Machi, 1995.

Kipekee kabisa ibara ya 9 ya Mkataba wa Maputo inazungumzia Haki ya Wanawake Kushiriki katika Siasa na Mchakato wa Ufanyaji Maamuzi katika nchi za Afrika.

Ibara hii ya 9 ya Mkataba wa Maputo inaakisi ibara ya 4, ibara ndogo ya kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kupinga Aina Zozote za Ukandamizaji dhidi ya Wanawake (CEDAW) ambayo inasomeka kama ifuatavyo:

Article 4 (1) Adoption by States Parties of temporary special measures aimed at accelerating de facto equality between men and women shall not be considered discrimination as defined in the present Convention, but shall in no way entail as a consequence the maintenance of unequal or separate standards; these measures shall be discontinued when the objectives of equality of opportunity and treatment have been achieved.

Kwa tafsiri yangu mkataba wa CEDAW unazitaka nchi wanachama kuchukua hatua maalumu zisizo za kudumu (ama za muda mfupi) zinazolenga katika kuleta usawa wa kiuhalisia baina ya wanawake na wanaume, na hatua hizi hazipaswi kuchukuliwa kama unyanyasaji/ukandamizaji... Ibara inamalizia kwa kusema, hatua hizi zitakoma pindi malengo ya usawa wa fursa na namna wanawake wanavyohudumiwa yatakapofikiwa.

Kwa mtazamo wangu nadhani kuna changamoto kwenye tafsiri halisi ya hatua maalumu zisizo za kudumu (temporary special measures) na ukomo wake.

Hatua hizi maalum zisizo za kudumu ukomo wake ni miaka mingapi? Mitano? 10? 15? Au 20?

Kwa nini? Kwa sababu mara kadhaa tumeshuhudia kwa mfano katika nafasi za Ubunge wa Viti Maalum katika vyama vya siasa, wanaopata nafasi mara nyingi hujirudia na kwa bahati mbaya wengine hufikia hatua ya kustaafu siasa pasina kuvuka hatua hii ya viti maalumu baada ya miaka 10 au 15. Nadhani hapa kuna changamoto kwenye tafsiri pana ya hii ibara ya CEDAW.

Binafsi ninadhani kwamba labda kwa mujibu wa ibara hii ya CEDAW huenda ukomo ungekuwepo labda baada ya muhusika kuwa amehudumu vipindi walau viwili kwani katika vipindi hivi viwili anaweza kuwa amewezeshwa kifursa, kiuchumi, kiutendaji na kimaamuzi bila ya kuathiri uwezo wake kiweledi.

Lakini hili pia halimaanishi ama halizuii hatua zisizo za kudumu kwa zaidi ya vipindi viwili, hasa kutegemea uwiano baina ya wanawake na wanaume katika vyama vya siasa, mgawanyiko wa kikanda na kuaminika kwa wahusika katika kusimamia matakwa ya chama na serikali katika chombo cha kutunga sheria au vyombo vingine vya maamuzi.

Nina imani kubwa wanawake wanaweza sana kuleta mabadiliko chanya katika vyombo vya maamuzi wakiwezeshwa na wakijiwezesha.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ni mfano tosha wa namna wanawake na kina mama wanavyoweza kuleta matokeo chanya na makubwa katika nchi.

Ninadhani kikubwa kinachotakiwa ni kujenga mifumo imara ya kuweza kuwapata wale watakaoweza kuvaa viatu vya wale watakaomaliza muda wao kisheria na kwa mujibu wa Katiba.

Lakini pia kuna haja ya kurejea tafsiri hii ya 'hatua maalumu zisizo za kudumu' ili kuwepo na mipango itakayofuataia (succession plan) iliyo bora hasa ikihusisha wanawake vijana katika Uongozi.

Nadhani hapa ile tafsiri waliyolenga Umoja wa Mataifa kupitia CEDAW inaweza kuleta tafsiri pana ya usawa na hatimaye kufikia malengo ya milenia sambamba na malengo endelevu (SDGs).

+255 719 258 484

Columnist: www.habarileo.co.tz