Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siku ya Mtoto wa Afrika:  Hakuna maendeleo kwa taifa bila kutilia maanani mahitaji ya watoto

048edcf84bec65f5322ee1adc676cb10 Siku ya Mtoto wa Afrika:  Hakuna maendeleo kwa taifa bila kutilia maanani mahitaji ya watoto

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JUNI 16 ya kila mwaka, Tanzania inaungana na nchi zingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Chimbuko la maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa Kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi.

Kwa sababu hiyo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana, mosi kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliyopewa na serikali ya kibeberu, pili waliitaka serikali ya mzungu iwape ruksa kufundishwa kwa lugha zao wenyewe.

Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia Juni 16 kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.

Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo.

Kwa hivyo, siku hii inaadhimishwa kwa maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inapaswa, sisi watu wazima, kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zetu ili kushughulikia changamoto nyingi zinazowakabili watoto katika bara zima la Afrika na hasa hapa nyumbani.

Kupitia maadhimisho haya, serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “2021 Tutekeleze Ajenda 2040: Kwa Afrika inayolinda haki za Mtoto”.

Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Mwaka huu tunakumbushana kuwa ili kuifikia Afrika inayolinda haki za mtoto, ipo haja ya kuhakikisha kwamba ‘hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kupata stahiki zake’ kwa kuongeza nguvu ili kuwafikia watoto hasa wale wasiofaidika na kukua na maendeleo ya Tanzania.

Hivyo, kanuni kuu ni kuzingatia wajibu wetu kuhakikisha maendeleo ya pamoja kwa watoto, yaani, wakati wowote wa kuandaa mipango na sera za kutekeleza Agenda 2040, watoto wanapaswa kuwa ndani ya mipango ili ‘kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora’.

Hii ni muhimu hasa katika mazingira ya Tanzania ambapo watoto huunda idadi kubwa ya wakazi wake.

Wazazi watambue kuwa familia ndio taasisi ya kwanza kuweka msingi wa maendeleo ya watoto kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na mataifa yaliyo mengi duniani, ikiwemo Tanzania.

Mataifa yanapokaa na kukubaliana malengo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto humaanishi kuwa serikali na wadau wa maendeleo wanao wajibu kuyatekeleza, lakini zaidi sisi wazazi na jamii kuanzia katika ngazi ya familia nasi tunayo sehemu ya kutekeleza. Vinginevyo familia zetu zitaachwa nyuma.

Takwimu za Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto, zinaonesha watoto wamekuwa wakipitia magumu ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, utelekezwaji, vipigo, utumikishwaji wa kazi ngumu, mimba na ndoa za utotoni ambapo yote haya yanakatiza ndoto zao za kimakuzi na mendeleo.

Vitendo hivi hufanywa na ndugu zetu, jamaa zetu na sisi wenyewe wazazi. Namna hii mchango wetu katika maendeleo ya watoto wetu ni hasi. Hawawezi kushindana na watoto wanaolelewa katika mataifa yaliyoamka, mathalani China, Japani na kwingineko. Tunaweza kubadili hili kwa kuongeza umakini katika malezi ya watoto wetu.

Ulinzi na usalama wa mtoto si jukumu la maofisa wa ustawi wa jamii peke yao bali ni jukumu la taifa kwa ujumla. Hakuna anayeruhusiwa kumdhuru, kumuumiza au kumnyonya mtoto.

Yeyote anayejua kwamba kuna mtoto anayeonewa au kutendewa vibaya hana budi kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo kwa Ustawi wa jamii; Polisi; Dawati la Jinsia na Watoto; Ofisi za serikali za mtaa na kadhalika.

Hivyo, tunatumia maadhimisho haya ya Siku ya Mtoto wa Afrika kuwakumbusha viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa letu hayawezi kupiga hatua bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto masikini na walio katika mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za halmashauri.

Tukumbushane kwamba gharama ya kutokufanya chochote ili kubadili hali ya watoto wetu ni kubwa mno.

Kushindwa kuwekeza katika huduma muhimu na ulinzi wa watoto wote si tu kunawanyima watoto haki zao lakini kutaingiza gharama kubwa zaidi baadaye kwa ajili ya maisha tegemezi watakayoishi, kunapoteza na kupunguza uzalishaji.

Hii si kwa Tanzania tu bali ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu.

Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho, kimwili, kisaikolojia na kiakili. Matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yanafumbatwa kwa namna ya pekee, katika huduma kwa watoto.

Leo hii jamii inawahitaji wajenzi wa ukarimu, watu wanaoweza kujitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani katika familia ya binadamu kwa kuzama zaidi katika misingi ya haki, mshikamano, udugu wa kibinadamu na utulivu. Kila mmoja anapaswa kuchangia katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili na unyama wanaoweza kutendewa ndani na nje ya familia zao. Watoto wanapaswa kuepushwa ndoa na mimba za utotoni kwa kupewa na kurithishwa maadili mema.

Kipindi cha janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto waliopata mimba kwa sababu ya kukaa muda mrefu majumbani mwao.

Wazazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu juu ya ulinzi na matunzo ya watoto wao. Watoto wanapaswa kuepushwa na vishawishi kwa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi kwa wakati.

Wafundwe pia kuwa na kiasi kwani katika maisha hawataweza kupata kila kitu wanachohitaji. Watoto wafundishwe umuhimu wa kuwa na nidhamu katika maisha! Waswahili wanasema, watoto wakilindwa vyema, watawaheshimu na kuwakumbuka wazazi wao!

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yawakumbushe viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa lolote lile hayawezi kupiga hatua mbele bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto masikini, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

0685 666964 au [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz