Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siku ya Kiswahili na nia ya kusambaza Kiswahili duniani

5f266c144c3fcc12f3168e56bfea5638 Siku ya Kiswahili na nia ya kusambaza Kiswahili duniani

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TUNAENDELEA na makala inayohusiana na maadhimisho ya Siku ya Kiswahili (Masiki), yalifanyika Januari 19 -20 Januari, 2021 Jijini Dodoma.

Maadhimisho haya yaliandaliwa kwa ushirikiano wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza), chini ya usimamizi wa Wizara zenye dhamana ya utamaduni: Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ya Zanzibar.

Aidha, maadhimisho haya yaliandaliwa kwa kushirikiana na taasisi na idara zinazojihusisha na Lugha ya Kiswahili na wadau wa Lugha ya Kiswahili kwa ujumla. Vilevile, Maadhimisho haya yamefanikiwa kutokana na michango ya washirika mbalimbali wanaounga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili.

Maadhimisho haya yalifunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Januari 19 na yalifungwa Januari 20 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah. Maadhimisho haya yalikuwa na kaulimbiu isemayo, “Bidhaisha Kiswahili kwa Maendeleo Endelevu ya Tanzania.”

Katika Maadhimisho haya jumla ya makala nne ziliwasilishwa: Uchunguzi wa Fursa na Changamoto za Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni (Dk M. S. Khatibu), Kiswahili na Fursa za Ajira; Uandishi na Uchapishaji wa Vitabu (Profesa M. M. Mulokozi), Kiswahili katika Uchumi wa Bluu (Dk Zainab Idd) na Ubidhaishaji wa Kiswahili (Profesa F. E. M. K. Senkoro).

Vilevile, katika maadhimsho hayo kulikuwa na kumbukizi mbili: Kumbukizi ya Mzee Suleiman Maulid Hegga (Mohamed Mwinyi) na kumbukizi ya Mohamed Said Abullah (Dk Masoud Mohamed).

Maadhimisho haya ya Siku ya Kiswahili yana historia ndefu. Yalianzishwa kwa wazo lililotolewa Julai 31, mwaka 1992 katika Kijiji cha Kwembe, mkoani Dar es Salaam nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hayati Horace Kolimba. Siku hiyo ilifanyika hafla fupi ya kumpongeza Mzee Saadan Abdul Kandoro ambaye sasa ni marehemu kwa mchango wake alioutoa kwa lugha ya Kiswahili.

Vilevile, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Mwaka 2020 ambayo Rais John Magufuli aliinadi kwa wananchi kuwa ataitekeleza katika kipindi chake cha miaka mitano; 2020 - 2025, ina mikakati ya kukiendeleza zaidi Kiswahili. Baadhi ya mikakati hiyo ni kama ifuatayo:

Mosi, kuendeleza diplomasia ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ikiwa ni pamoja na Lugha ya Kiswahili kutumika kikamilifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

Pili, kuimarisha mafunzo ya lugha kwa kutoa programu maalumu ya Lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za kigeni kwa ajili ya kuzalisha wataalamu na wakalimani wa Kiswahili kwenye viwango vya kimataifa.

Tatu, kutangaza lugha ya Kiswahili katika AU kama urithi wa Mtanzania na Mwafrika.

Nne, kuhamasisha matumizi ya Kiswahili katika kutoa matokeo ya utafiti wa kisayansi na machapisho ya kitaaluma.

Pamoja na Nishani ya Juu ya Shaaban Robert iliyotolewa kwa Rais John Magufuli katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili, kulitolewa pia tuzo kwa, Mwandishi nguli wa vitabu vya taaluma ya Kiswahili, Redio, televisheni na magazeti yenye matumizi fasaha na sanifu na yanayofanya jitihada za kukikuza Kiswahili, chuo kikuu kilichotahini na kuendesha tafiti nyingi za Kiswahili na wanafunzi waliofanya vizuri katika somo la Kiswahili nchini.

Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyopata tuzo hizi ni gazeti letu pendwa la HabariLEO. Sisi, wadau wa Kiswahili tunaoandika makala katika gazeti hili na kusoma habari zake, tunalipongeza kwa kupata tuzo hii. Ni imani yetu kwamba tuzo hii itakuwa chachu kwa gazeti hili kukiendeleza zaidi Kiswahili.

Aidha, Maadhimisho hayo ya siku ya Kiswahili yalitokana na maazimio mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapiga hatua zaidi. Miongoni mwa maazimio haya ni:

Mosi, nchi inapaswa kuwa na Sera Maalumu ya Matumizi ya Lugha ya Kiswahili.

Pili, ifanyike mikakati ya kukiwezesha Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.

Tatu, mabaraza na taasisi za Kiswahili ziwafundishe watumiaji wa Kiswahili kuhusu msamiati wa kisasa ikiwa ni pamoja na maelekezo ya Kiswahili katika simu za mkononi na kompyuta.

Nne, taasisi zinazofundisha Kiswahili kwa wageni ziboreshe mazingira ya ufundishaji: Vyumba vya madarasa, maeneo ya kupumzikia, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ujenzi wa hosteli, utoaji wa vyeti vya uthibitisho, kujitangaza zaidi pamoja na kuwa na utaratibu bora wa malipo ya viza kwa wanafunzi wa Kiswahili kwa wageni.

Tano, kuanzishwe madawati ya Kiswahili na utamaduni wake katika balozi za Tanzania nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na tuzo za kidunia za kiswahili pamoja na ubalozi wa heshima kwa wanaokisambaza kiswahili duniani.

Sita , mabaraza ya Kiswahili yaandae mikakati mahususi ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili na Serikali iyawezeshe kwa kuyapatia wataalamu na itenge fedha katika bajeti kwa ajili ya miradi ya Kiswahili ya mabaraza haya.

Saba, ili kukabiliana na ushindani, waandishi na wachapishaji wa vitabu watumie soko la kidijiti, ikiwa ni pamoja na kuzingatia hakishiriki na hakiambatani.

Nane, kozi za ukalimani, tafsiri na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni ziwe za lazima katika vyuo vikuu nchini.

Tisa, kuwe na kanuni zinazowataka wawekezaji kujifunza Kiswahili kwa kipindi maalumu kutegemeana na mahitaji yao.

Kumi, kuwe na muda maalumu wa vitabu vya fasihi kutumika katika mitaala ya Lugha ya Kiswahili shuleni ili kuwezesha wanafunzi kupata maudhui mapya kupitia kazi za waandishi wengine.

Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza) wameahidi kuyafanyia kazi maazimio haya na kupeleka taarifa kwa maandishi kwa asasi, taasisi, idara na wadau wote wa Kiswahili. Aidha, mabaraza haya mawili yatatoa taarifa zaidi ya ushughulikiaji wa maazimio haya katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yatakayofanyika Zanzibar, mwaka 2022.

Ni matarajio ya wadau wote wa Kiswahili kwamba maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yataendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wapenzi wa Lugha ya Kiswahili ili kujadili maendeleo ya lugha yao na kuweka mikakati ya kuzikabili changamoto zinazojitokeza ili Kiswahili kipige hatua zaidi na kuwawezesha kimapato watumiaji wake na nchi kwa ujumla.

Tujivunie Kiswahili.

Mwandishi wa makala haya ni Mhariri Mkuu Bakita, anapatikana kwa namba 0765 - 616 421

Columnist: habarileo.co.tz