Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shubiri ya ufundi duni, umaskini unavyotumbukiza shimoni mradi

Gagaga.webp Shubiri ya ufundi duni, umaskini unavyotumbukiza shimoni mradi

Fri, 19 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

DC Muro awafuatilia wafadhili warudi

IJUMAA iliyopita ilikuwa sehemu ya kwanza ya makala hii kuhusu mradi wa nishati ya gesi wilayani Arumeru na namna inavyoleta ahueni ya kiuchumi dhidi ya dhiki ya kuni. Endelea na safu ya pili.

“HUU mtambo wa baiogesi uliharibika wenyewe, gesi ilikuwa haitoki. Nilimjulisha fundi, alivyokuja akanimbia nikitoe kinyesi hapa. Najiuliza hiki kinyesi nakitoa vipi katika huu mtambo?” Ni maneno ya Unice Palangyo, aliyekuwa akihaha kupata suluhu ya kutengenezewa mtambo wake.

Anasimulia kuwa nishati hiyo kabla ya kuharibika, ilikuwa ikimsaidia kupunguza matumizi ya kutafuta kuni, hivyo kwa sasa imegeuka shubiri baada ya kukosekana ufundi.

Palangyo, mkazi wa kijiji cha Oldonyowas wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, anaeleza kukosa matumaini ya kuendelea na nishati hiyo mbadala itokanayo na kinyesi cha ng’ombe.

Arusha inaongoza kuwa na wafugaji 111,183 sawa na asilimia 45 nchini kwa mujibu wa takwimu za Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2016, huku ikiatajwa kuwa kinara wa kutumia kuni, kwa wastani wa kaya sita kati ya 10 zinatumia kuni kupikia.

Hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Upatikanaji Nishati Tanzania Bara, kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), mwaka 2016 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Wananchi wa kijiji hicho walihamasishwa kutumia nishati mbadala ya kinyesi cha ng’ombe kupika chakula, lengo ni kupunguza matumizi ya kuni na kutunza mazingira.

Ilipoanzishwa, wananchi hao walichangamkia fursa hiyo na kupatiwa mtambo wa baiogesi waliofungiwa kwa gharama ya Sh. 215,000 pamoja na jiko la kupikia.

CHANGAMOTO

Ingawa kuna wengi walioshangilia kuibuliwa kwake wapo waliobaki katika machungu, sababu ni kushindwa kuitumia, hususan wanapokumbwa na gharama za kukarabati miundombinu.

Ni hali inayoendana na shaka ya watumiaji hao, baadhi wakihoji ukweli wa tetesi zinazodai wenye mradi wamerudi kwao nchini.

Palanjo anataka adha ya fundi, pale anapomuita afike mtengenezaji huyo, anaanza kwa kutoa kinyesi chote katika mtambo, jambo analodai ni mtihani kwao wamiliki.

Anaendelea kwa kuhoji: “Hivi unawezaje kuzoa hiki kinyesi? Hapo ndipo paliponishinda na ndio maana nimeshindwa kuendelea na mtambo huo, maana huu ni mtihani juu ya mtihani, mafundi wenyewe hawawezi wanakuja kutuambia sisi tutoe kinyesi chote.”

Pia, kuna wanaolalamikia gharama za ufundi wa mitambo hiyo ya baiogesi, pindi inapopata tatizo kubwa na mwenyeji, Neema Lucas akiwa na ufafanuzi wa kiufundi kwamba, kuna wakati mipira iliyowekwa inasababisha gesi kupotea njiani, hata kumlazimu kumuita fundi.

Kwa mujibu wa Neema, hapo ni gharama inayoanzia Sh. 20,000 kutegemea na tatizo na ana ufafanuzi: “Sisi anatujua hivyo wakati mwingine tunamuomba tunamlipa Sh. 10,000 ingawa hii hela ni kubwa kulingana na maisha yetu hapa kijijini.”

Obed Mollel, mkazi wa kitongoji cha Zahanati, anarejea kilichopo kwa wanufaika wa awamu ya kwanza ya mtambo, kwamba iliharibika na hawajarekebishiwa.

Anasema ni hali inayowapa hofu pale mtambo utakapoharibika, kwani hawajui watakapopata msaada, kwa sababu kuna changamoto zilizojitokeza awali bado hazijashughulikiwa.

Mollel anasema alipojiunga na mradi wa baiogesi, aliahidiwa nishati hiyo ingekuwa na uwezo wa kuwasha taa, jambo ambalo halijatekelezwa, ikiishia kuwasha kupikia pekee na hadi sasa hawana mawasiliano na mwekezaji, aliyeondoka kurudi kwao, Italia.

URIO ASEMA

Wakati wananchi wakilalamika suala la kuharibika kwa miundombinu ya Biogas bila kupata msaada na mitambo hiyo kuiacha, Ombeni Urio, mwenye kampuni iliypjenga mitambo ya Oikos na kuna wakati ardhi inachangia kupotea kwa gesi.

“Ukiona mpaka unaambiwa uzoe kinyesi katika mtambo, ina maana tumefanya jitihada zote za kutafuta ‘likeji’ ikashindikana ndio maana tunamuambia akitoe kinyesi ili tujue tatizo lipo wapi,” anasema.

Urio anafafanua urefu wa kuchimba mtambo ni mita 1.85 sawa na mita sita za ujazo, zinajazwa lita 6,350 za kinyesi mmiminiko.

Anasema mteja anaposhindwa kutoa kinyesi katika mtambo huo, mbadala wake anatakiwa kugharamia Sh.180, 000 iwapo wameufunga wao na kama ni kutoka kampuni nyingine Sh 400,000.

Urio anasema, jiografia ya udongo wanayojenga mitambo ya nishati mbadala, kuna wakati ardhi ya eneo inadidimia bila wao kujua na anaongeza: “Kuna maeneo ardhi hudidimia na wahusika wa eneo hawana uelewa na ardhi yao.

“Sasa tunapoweka mtambo ardhi ikididimia na ule uzito wa kinyesi ambao unawekwa mtambo unaweza kugeuka na kusababisha gesi kutawanyika na kuanza kutokea pembeni kwa mtu kama huyu ni lazima atoe kinyesi chote ili asaidiwe tatizo lake.”

SHIDA KUJITAKIA

Kasoro zingine Urio anazieleza: “Wakati mwingine ni uzembe wao kutokulisha kwa wakati yaani anapunguza ng’ombe au kutokulisha kwa wakati. Hii nayo ni changamoto itakayomfanya asipate gesi wakati anapotaka kupika.

“Kuna wengine imetokea ‘leakage’ (uvujaji) kwenye pampu tunaenda kumrekebishia, watu wanalima bila kuangalia kama paipu imepita na kutoboa bila kujua. Inabidi tumbadilishie, kwani hujikuta gesi inashuka kila wakati,” anafafanua Urio.

Kuhusu dai la gharama kubwa wanazotozwa watumiaji umeme wa gesi, Urio anasema inaendana na ukubwa wa tatizo ulivyo, akidai ni kati ya Sh. 10,000 hadi Sh. 50,000.

Anasema, kuna wanaojaza maji mengi katima gesi ambayo kiufundi ni kosa, kwa sababu wadudu anaowataja kwa jina la anarobian’ hutengeneza gesi wanaposhambulia mlo na wanapokosa chakula ambacho ni kinyesi cha ng’ombe, gesi haiwezi kutengenezwa.

DC MURO

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, anasema walikuwa katika subira ya nyendo za ugonjwa wa virusi vya corona umalizike, ili wafadhili hao wafanye mapito ya mradi wao.

“Zipo baadhi ya familia zimeshindwa kutumia mradi huo. Sisi tulichofanya ni kuwaomba wenzetu wa Oikos kutengeneza mradi wa pili ya mapito ya mradi, ili tuone tunaweza kufanya nini ya kuhakikisha tunawasaidia hawa wananchi ambao wamekumbwa na changamoto,” anasema Muro.

Anaendele:“Mimi nikiwa kama kiongozi Mkuu wa Wilaya, siwezi kulalamika kwamba wananchi wangu hawakuwa na uelewa na jukumu letu ni kutatua changamoto.”

Muro anasema, namna ya kutatua changamoto hiyo ni kuomba marejeo ya mradi, waweze kufanikiwa na muhimu wenzao wa kampuni ya Oilcos iwatafutie fedha zitakazosaidia kuwaleta wataalamu.

Anasema mradi huo makao makuu yake yako nchini Italia, ambako kuliathirika sana na ugonjwa huo hata kuukwamisha mradi.

“Wengi wapo Italia baada ya shughuli hizi kukamilika. Walifunga ofisi na kurudi kwao, hawakujua kama janga lingekuwa kubwa kiasi hiki,” anaeleza

Anasema katika namna ya kupata suluhishi ya dharura hiyo, alizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Arumeru, awatumie wataalamu waliokuwepo kuwasaidia.

Katika hilo, Muro anatoa rai kwa wananchi wenye changamoto yoyote ya nishati uhakikisha wanatoa taarifa kwa viongozi wao, akieleza: “Ombi langu wapitie ngazi husika kwa maofisa watendaji wetu wa kata ili taarifa zao ziweze kuja kwetu ili tuweze kuwasaidia.”

Muro anakiri kuwa bado hana takwimu halisi ya wanaokabiliwa na changamoto katika mradi huo wa baiogesi, kwa sababu wanajitokeza mmoja mmoja mmoja.

Columnist: www.tanzaniaweb.live