Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shida ya Stars Kombe la Dunia ni kwa Mkapa

Kwa Mkapa Shida ya Stars Kombe la Dunia ni kwa Mkapa

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NDOTO ya Watanzania kuiona timu yao ya Taifa, Taifa Stars ikicheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar, iliyeyuka Alhamisi iliyopita, baada ya kuchabangwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakati Wabongo wakitafakari kipigo hicho kilichotokea jioni, Benin ni kama ilimwagia pilipili kwenye kidonda kibichi cha Stars kwa kuicharaza Madagascar mabao 2-0 majira ya usiku, ikiwa nyumbani na kuifanya safari ya Stars kuishia njiani.

Ni matokeo ambayo ndiyo yaliwatoa moja kwa moja Stars, huku Benin ikifikisha pointi 10 baada ushindi huo na kuicha Stars na pointi zake saba.

DR Congo, ambayo ilikuwa imeshinda mabao 3-0, yenyewe ilifikisha pointi nane, kwani mwanzo ilikuwa na pointi tano. Kwa maana hiyo nafasi moja inayohitajika kwenye Kundi J, itakwenda kwa Benin au DR Congo na kuwaacha Watanzania wakiwa hawaamini kilichotokea baada ya kuongoza kundi kwa muda mrefu.

Kimahesabu ni kwamba, Benin mchezo wa jana ilikuwa ikihitaji sare tu ili kufikisha pointi 11 na kutinga raundi ya mtoano huku DR Congo yenyewe ikihitaji kushinda kufikisha alama hizo na kuwaacha Wabenin hao na alama zake 10.

Hayo ndiyo mahesabu yaliyoiondoa Stars bila kuangalia matokeo yoyote ya mechi za jana kwani sare ama ushindi kwa timu yoyote kati ya DR Congo ama Benin ni wazi Tanzania ilishaikosa nafasi hiyo moja.

Hata hivyo, kilichoisukuma nje Stars na kushindwa 'kutoboa' kwenye Kundi J na kwenda kwenye mechi za mtoano ni kutotumia vema uwanja wake wa nyumbani. Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa sumu kwa Stars, kwani imezoa pointi nyingi ikicheza ugenini kuliko nyumbani.

Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Madagascar, tayari Stars ilikuwa imevuna pointi nne ikicheza ugenini na tatu tu ikicheza nyumbani, huku ikiwa imemaliza mechi zake.

Iwapo ingeshinda mechi zake mbili ilizopoteza nyumbani ingekuwa na pointi 13. Ni pointi ambazo zingeiweka pazuri na hata si ajabu ingemaliza kinara wa kundi na kwenda kucheza mtoano.

Stars ilivyowapa matumaini Watanzania

Ilianza michuano hii kwa kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Septemba 2, mwaka huu, ikiwa ugenini.

Baada ya Dieumerci Mbokani kufunga bao, Simon Msuva alisawazisha na mechi ikaisha hivyo. Ndiyo mechi iliyoanza kuwapa matumaini kuwa inaweza kufanya maajabu kwenye michuano hii.

Oktoba 10, mwaka huu, Stars ilikwenda nchini Benin na kufanya maajabu ya kuitungua kwao timu hiyo bao 1-0, tena ikitoka kufungwa nyumbani.

Ushindi huu, ulizidi kuwapa moyo Watanzania kuwa inaweza kwenda Qatar, lakini hali haikuwa hivyo. Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Madagascar, Stars ikiwa haijapoteza mechi yoyote ile ugenini.

Ilifia Benjamin Mkapa

Stars imefungwa mechi mbili kati ya tatu ilizocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani. Ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Madagascar Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 7 na ndiyo mechi pekee kushinda nyumbani kwenye michuano hiyo ngazi ya makundi.

Oktoba 7, Stars ilipoteza tena nyumbani kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Benin, na kuweka rekodi ya kupoteza mechi mbili. Ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa ziliifelisha Stars.

Columnist: www.tanzaniaweb.live