Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shekhan, Fei Toto mwingine au Mwashiuya mwingine?

Shekhan Shekhan Ibrahim Khamis

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakubwa zetu walikuwa Zanzibar wiki iliyopita wakikimbizana kuinasa saini ya kiungo kinda wa JKU anayeitwa Shekhan Ibrahim Khamis. Ana miaka 18 tu na ukiona wakubwa wanakimbizana ujue ana kitu. Haijatokea muda mrefu kwa wakubwa kukimbizana kwa mchezaji mwenye miaka 18.

Naambiwa kwamba Simba walikuwa wanamsubiri feri baada ya kumtumia tiketi ya boti, lakini Yanga wakawa wajanja kwa kwa kutumia ‘Uzanzibar’ wa Makamu wao wa Rais, Arafat Haji kumchukua kwa ndege na kuja naye Dar es Salaam. Baadaye ametangazwa kuwa mchezaji wa timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mbwembwe hizi za kukimbizana kwa wachezaji wa ndani au wale wa kigeni kamwe usitazamie ziishe. Ni sehemu fulani hivi ya burudani ambayo Simba na Yanga wanaweza kukupa nje ya uwanja. Wana mbwembwe fulani hivi ambazo unaweza kuandika kitabu chenye kurasa 1,000 kuelezea walivyokimbizana kunasa mastaa kwa miaka mingi sasa.

Niliamua kwenda kasi kujua kipi ambacho kiliwakimbiza Simba na Yanga hadi Zanzibar kwenda kuinasa saini ya kinda huyo. Nimetazama video zake. Kwa haraka haraka anaonekana ana kitu. Umbo kubwa, kasi, umiliki wa mpira na ana matumizi mazuri ya miguu yote miwili.

Hapa karibuni Zanzibar imepotea katika ramani ya soka. Haitoi wachezaji wengi mahiri kama ilivyokuwa zamani. Zamani Zanzibar ingeweza kutoa hadi wachezaji wanne wanaoanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania. Mastaa hawa walikuwa wanatokea Malindi, KMKM, Small Simba, Jamhuri na Mlandege.

Msimu uliopita nilikuwa naifuatilia Ligi ya Zanzibar sikuona vipaji vya ajabu. Baadaye akatokea Ibrahim Bacca ambaye sijui Yanga walimuona wapi. Na wiki iliyopita wakubwa wamekimbizana kwa Shekhan. Inatokea nadra kwa wakubwa kuvuta mchezaji moja kwa moja kutoka ligi ya Zanzibar ya leo. Vipaji ni bidhaa adimu Zanzibar ya siku hizi.

Na sasa najiuliza kama Shekhan atakuwa Fei Toto mwingine katika soka letu au Geofrey Mwashiuya mwingine katika soka letu. Fei alitokea katika klabu ya JKU na nusura atue katika mikono ya Simba. Ghafla Mwigulu Nchemba na Singida yake wakafanikiwa kuinasa saini yake. Siku chache baadaye wakawaachia ndugu zao Yanga. Mwigulu ana Uyanga mwingi.

Kuanzia hapo hadi sasa Fei amekidhi matarajio ya wengi. Alikuwa hazina ya Yanga halafu akawa hazina ya timu ya taifa. Majuzi amewaudhi Yanga kwa kutimkia Azam, lakini Fei ameendelea kuwa yule yule tu. Ameendelea kuwa mahiri na kipaji chake maridhawa. Hajarudi nyuma.

Lakini stori hizi za usajili zina pande nyingi. Kuna mchezaji anaitwa Geofrey Mwashiuya naye akiwa kinda kama hivi aliwahi kuwakimbiza Yanga hadi Mbeya. Wakavuka Mbeya mjini wakavuka Songwe wakaenda hadi Mbozi kuinasa saini yake wakati anachezea timu ya Kimondo. Mwashiuya alijaribu kuruka kuruka lakini hakuweza kufikia matarajio.

Shekhan atachagua njia gani? Kuwa Fei au Mwashiuya? Niliposikia ni kiungo nilimpa tiki ya kwanza ya kiasili tu. Kwamba Zanzibar imekuwa ikitoa wachezaji wengi wa nafasi ya kiungo katika miaka ya karibuni. Nawajua viungo zaidi ya saba waliocheza ligi yetu miaka ya karibuni wakitokea Zanzibar.

Wakati mwingine ni rahisi kwa mchezaji kutimiza matarajio ya wengi kama akiwa na ‘kiburi chanya’ na nidhamu ya hali ya juu. Kwanini kiburi chanya? Kuna wachezaji makinda wanafeli katika hizi timu kwa sababu ya hofu. Hawajiamini na wanashindwa kukabiliana na ukubwa wa timu.

Haishangazi kuona kwamba wakati mwingine wanafeli halafu wanakwenda kwingine wanang’ara na baadaye kurudi katika timu kubwa. Mfano mzuri ni Yanga walipomsajili kinda Hassan Dilunga kutoka JKT Tanzania. Hakuweza kuhimili vishindo. Akaenda zake Mtibwa kukomaa akarudi zake Simba na kuwa staa mkubwa.

Kitu kingine kinachoharibu hawa vijana ni pale anaposifiwa mechi mbili tatu atakazocheza vizuri. Anajiona staa. Anavimba kichwa. Anajikuta ana naisha mengi nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Mpira unamshinda kwa kuendekeza pombe na wanawake. Imewahi kutokea hata kwa wachezaji wakubwa waliohamia hizi timu zetu mbili wakitokea timu za kawaida au nje ya nchi.

Halafu kuna makinda wengine wana roho ngumu na wanahimili vishindo moja kwa moja. Hawa ndio kama kina Simon Msuva. Alipitia mengi alipotua Yanga ikiwemo kuzomewa na mashabiki wake. Baadaye akaibuka kuwa staa wa timu. Ni kama kinachoonekana kutokea kwa Clement Mzize kwa sasa. Licha ya umri wake na ugeni katika soka la juu lakini hatimaye amehimili vishindo.

Kinachonisisimua unaposoma habari za Shekhan ni pale unapotamani awe mchezaji wa maana aweze kulisaidia taifa. Kila siku zinaposonga mbele ndivyo vipaji vinapotea nchini. Wakubwa wanagombana zaidi kwa wachezaji wa kigeni ambao wamekuwa na msaada mkubwa katika timu zao kuliko wachezaji wazawa. Unaposikia habari kama hii ya Shekhan unatabasamu kwa sababu ya Taifa Stars.

Inanikumbusha namna ambavyo tunanufaika na ujio na Mzize katika soka letu. Inanikumbusha pia namna ambavyo tumeshika roho zetu kwa Mohammed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe. Kweli wakiisha ni wazawa gani wanaweza kuzicheza nafasi zao kwa ufasaha kama wao wanavyofanya? Utasikia Simba wamekwenda Ivory Coast kuleta mabeki wa pembeni.

Si unaona katika lango la Simba? Kama Aishi Manula ungekuwa mwisho wake basi tayari nafasi yake inakwenda kwa mgeni kutoka Morocco. Wale wasaidizi wa Tanzania hawafikii kiwango cha Mmorocco. Huu ndio ukweli ambao tunalazimika kuumeza.

Mwisho wa John Bocco umewadia. Unadhani kuna mshambuliaji gani mwingine wa Kitanzania anayeweza kuziba lengo lake ndani ya Simba? Hauwezi kuona kwa urahisi sana. Kila siku taifa linapungukiwa vipaji na timu kubwa zinaangalia zaidi nje ya nchi. Haiwi faida kubwa kwa nchi lakini hauwezi kuwazuia kwa sababu wanafanya hivyo kwa malengo yao binafsi.

Tusubiri kumuona Shekhan. Kama akiwa kama inavyofikiriwa basi itakuwa jambo zuri kwa Yanga na taifa. Hawa wachezaji wakicheza timu kubwa wanapata faida kubwa ya mechi nyingi za kimataifa tofauti na wanapoibukia katika klabu za kawaida ambazo hazishiriki michuano ya kimataifa. Tusubiri tu kuona kama atakuwa Fei Toto mwingine au Mwashiuya mwingine. Mpira upo katika mahakama yake.

Columnist: Mwanaspoti