Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shamba la mifugo Sao Hill kuongeza uzalishaji mitamba bora ya ng’ombe

NG'OMBE Shamba la mifugo Sao Hill kuongeza uzalishaji mitamba bora ya ng’ombe

Sat, 20 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SEKTA ya mifugo ni miongoni mwa chache ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza pato la Taifa. Mpaka kufikia mwaka 2019, sekta hiyo imechangia kwa asilimia 7.4, baada ya ukuaji wake kuongezeka kwa kasi ya asilimia tano.

Kwa kutambua mchango huo serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuwekeza katika mashamba makubwa ya mifugo ili kuyapa uwezo wa kuzalisha mifugo bora itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Moja ya shamba ambalo serikali imewekeza ni la Sao Hill, lilipo kijiji cha Itulavanu, Kata ya Ikongorisi mkoani Iringa.

ILIPOTOKA SHAMBA LA SAO HILL

Akielezea safari ndefu ya shamba hilo, Kaimu Meneja, Mtama Gerald Galusi, anasema kuwa lilianzishwa mwaka 1967 baada ya serikali kulitaifisha kutoka kwa wakulima wa kizungu.

Meneja huyo ansema kuwa mwaka 1968, shamba hilo lilianza kufanya kazi rasmi na kutumika kama sehemu ya kuzalisha mitamba bora ‘breeding unit’ na kuwauzia wafugaji wadogo wadogo wa Nyanda za Juu Kusini.

Galusi anaeleza kwamba Sao Hill imekuwa na uzalishaji mzuri kwa sababu shamba hilo linafaidika na hali ya hewa nzuri ya baridi, ambayo inawafanya mifugo kustawi vyema na kutoa uzalishaji mzuri tofauti na mashamba mengine ambayo yapo katika ukanda wa joto.

Anasema shamba hilo pia linafaidika na Mto Ruaha, ambao maji yake yanatiririka vipindi vyote vya majira kuelekea kwenye bwawa la Mtera.

Mafanikio ya shamba tangu kuanzishwa kwake

Akizungumzia mafanikio ya shamba hilo ambalo hadi sasa lina ng’ombe 1,600, meneja huyo anasema wamefanikiwa kuzalisha mitamba mingi na kuisambaza kwa wafugaji wadogo kwa bei nafuu.

Mitamba hiyo imewanufaisha wafugaji wa wilaya zote za mikoa ya Iringa na Mbeya.

Akazitaja baadhi ya wilaya hizo ni Rungwe na Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Busokelo, zimefaidika na utaratibu wa ‘kopa ng’ombe lipa ng’ombe,’ uliosababisha wananchi wengi kuwa na ng’ombe wa maziwa.

Anaendelea kusema kuwa shamba hilo limezalisha eneo la malisho pamoja na mbegu za majani kwa ajili ya kuwauzia wafugaji wadogo wa kimkoa kwa gharama nafuu.

Galusi anasema ng’ombe kutoka Sao Hill wanapatikana kwa bei nafuu ambayo mfugaji mdogo anaweza kumudu, akitolea mfano Mtamba mwenye mimba anauzwa kwa shilingi 1,600,000, tofauti na mashamba ya watu binafsi ambayo inafikia kati ya 3,000,000 na 4,500,000.

Aidha, meneja huyo ameipongeza serikali kwa kuwajali na kuwapa wafugaji mitamba bora kwa bei ambayo kila mtu anaweza kununua.

Changamoto zinazokabili shamba hilo

Galusi anasema katika kila mafanikio hapakosi changamoto, hivyo matatizo yanayolikabili shamba hilo ni uchache wa vitendea kazi, hususan usafiri wa kutembelea maeneo ambayo ina mifugo.

Changamoto nyingine ni kuwa eneo hilo lina mvua nyingi ambazo husababisha kupungua kwa madini joto ambayo ni muhimu kwa mifugo, jambo ambalo linawalazimu kununua madini hayo kwa bei kubwa.

Matarajio katika uzalishaji

Kwa upande wa matarajio, Galusi anasema hadi kufikia mwezi Juni, 2020 wamepanga kusambaza mitamba aina ya Borani kati ya 120 hadi 130, kutokana na uhitaji wa ng’ombe hao kuwa mkubwa.

Anasema mitamba hiyo dume aina ya Borani inasaidia kuboresha uzalishaji kwa ng’ombe wa asili kwa wafugaji wadogo wadogo. Wito kwa Wadau wa Mifugo.

Meneja huyo anatoa wito kwa wadau wa Mifugo wazalishe kwa tija ili wawe na maziwa na nyama za kutosha ili kujenga uwezo wa kusambaza kwenye viwanda ambavyo vinachakata mazao ya mifugo.

Pia, aliwashauri wafugaji kutumia mashamba ya serikali kupata madume bora ili waboreshe mifugo yao pia kuitumia kama mashamba darasa ya kujifunzia.

Anaendelea kuwashauri wadau kutumia njia ya uhimilishaji kwani inasaidia kuboresha kosaafu za ng’ombe, ambao wanakuwa haraka tofauti na ukuaji wa ng’ombe wa asili.

Robert Semaganga, Ofisa Mifugo ambaye ni mratibu wa sekta ya ng’ombe wa maziwa, ameishukuru serikali kwa kuanzisha na kuwekeza katika shamba la Sao Hill, kwani limekuwa msaada mkubwa kwa wafugaji.

Akitolea mfano, Semaganga, anasema “Kuna shamba la Justine Bimbiga ambaye ana ng’ombe 54, ambao wengi ni zao la shamba hili, hii inafurahisha kuona mfugaji kuonyesha matokeo bora ya Sao Hill. Pia wanafunzi wa vyuo mbalimbali hufika hapo kujifunza kwa vitendo,” anasema Semaganga.

Jobisho Mkonyi, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Mufindi, anasema kuwa uwepo wa shamba la Sao Hill, kumewasaidia kupata mitamba kwa bei nafuu, ambapo mtamba aliyekuwa anauzwa 1,600,000, sasa anapatikana kwa 1,200,000. Kiasi kilichobaki wamepunguziwa kama ofa kwa wafugaji.

Anaongeza kwa kusema uwepo wa shamba hilo kunawafanya wapate huduma za wataalamu wa mifugo kirahisi na karibu.

Aidha, aliiomba serikali kuendelea kuwasaidia ili waendelee kupata ng’ombe walio bora zaidi ambao wanatoa maziwa mengi.

Ushauri wa Serikali kuhusu Malisho

Mkurugenzi wa Idara ya Malisho, Dk. Asimwe Rwiguza, anasema wafugaji wengi bado wanategemea malisho ya asili ambayo kimsingi hayatoshelezi na hayana viini lishe vya kutosha.

Amewahimiza wafugaji kuandaa mashamba ya malisho na kutumia mbegu bora zinazopatikana kwenye mashamba ya serikali ili kuboresha lishe za mifugo yao.

Aanasema wizara kupitia Idara ya Malisho na Uendelezaji wa Rasilimali za Mifugo, imeendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu uzalishaji na utunzaji wa malisho.

Faida zinazopatikana kupitia mifugo

Kulingana na Wizara ya Mifugo, ufugaji wa ng’ombe bora una faida nyingi kiuchumi, kwani licha ya nyama na mbolea, humpatia mfugaji nishati ya kupikia ya gesi inayojulikana kitaalam kama ‘Biogas’.

Nishati hii ya gesi inapatikana kutokana na kinyesi cha ng’ombe ambacho wengi wanaita samadi.

Wafugaji wakielimishwa na kuhamasishwa vizuri kutumia njia hii mbadala ya matumizi ya nishati ya gesi inayotokana na samadi, inapunguza matumizi ya kuni ambayo kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa ikiyapiga vita kwa kuharibu mazingira.

Mfugaji na mkulima kutoka kijiji cha Igowole, Michael Mhosole, aliwaambia maofisa habari wa wizara hiyo, waliomtembelea kuwa ng’ombe aliowapata kutoka Sao Hill, wamemuinua kiuchumi kwa kuuza maziwa ya kutosha na kutumia gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Anasema anapata nishati hiyo ya gesi baada ya kujenga mtambo unaotumika kuchakata samadi ya ng’ombe na kuibadilisha kuwa nishati ya gesi tayari kwa matumizi ya kupikia.

Mhosole anasema kuwa nishati ya gesi inayotokana na ng’ombe ikitumika vizuri inasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Pamoja na samadi kunizalishia gesi, pia naitumia kwa ajili ya kurutubisha udongo katika mashamba yangu,” anasema Mhosole.

Aidha, anatoa wito kwa wafugaji wenzake kuweka juhudi katika kutunza mifugo yao vizuri kwa kuwapatia huduma zinazohitajika, ikiwamo kuandaa mashamba ya malisho na chakula cha kutosha katika kipindi cha kiangazi ambacho kunakuwa na uhaba.

Columnist: www.tanzaniaweb.live