Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shaffih tumaini jipya Tuzlaspor

Shaffih Pic Shaffih tumaini jipya Tuzlaspor

Wed, 7 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Tuzlaspor ya Uturuki imemtambulisha kinda wa Kitanzania, Shaffih Omary kama miongoni mwa wachezaji inaoamini watakuwa mashujaa wao kwa miaka michache ijayo kutokana na ukubwa wa kipaji chake.

Wiki iliyopita, Tuzlaspor inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Uturuki maarufu kama TFF First League ilitumia mitandao yake ya kijamii kumtambulisha kinda huyo ambaye ni zao la taasisi ya kuvumbua na kuendeleza vipaji ya African Youth Empowerment (AYE).

Utambulisho huo, uliambatana na ujumbe usemao, “Tuzlaspor inaendelea kutafuta, kuandaa wachezaji nyota wa siku zijazo duniani. Wachezaji wetu wapya tunaamini majina yao yatatajwa siku zijazo.... Tunakuletea nyota hawa kwa furaha.”

Awali, Nje ya Bongo iliripoti juu ya mchakato uliofanywa na AYE huku mawakala mbalimbali wa soka wakipishana Tanzania kutafuta vipaji na haya ni moja ya matunda yake, huku ikiaminika yapo mengine makubwa zaidi yanakuja.

Akiwa Tuzla huko Istanbul, Shaffih mara baada ya utambulisho huo kwenye mazunguzo na gazeti hili, kinda huyo aliyetokea mtaani kabisa, ametoa shukrani zake za dhati kwa AYE ambayo imemfanya kupiga hatua kwenye kile alichokuwa akikiota kwa kipindi kirefu maana hapo kabla hakuwa akiona njia za kufikia malengo yake.

“Nashukuru Mungu kwa hatua niliyopiga, sio kwa akili au uwezo wangu hapana, nisiwe muongo, naamini ilipangwa hii ndio itakuwa njia yangu ya kutokea, siwezi kuacha siku zote kuitaja familia yangu ya AYE, wamenisaidia sana.”

“Nilikuwa mmoja kati ya vijana waliojitokeza kwenye usajili wao na nikajiandaa kwa ajili ya kuonyesha kipaji changu, vijana walikuwa wengi lakini wakala aliyekuwa pale alivutiwa na mimi na akataka kuniona zaidi. Niliendelea kuonyesha kipaji changu na hatimaye wakaona ninafaa kuja huku kuendele-zwa.”

“Najua haikuwa rahisi kufanikisha hili maana kuna mambo mengi, walitumia muda wao na gharama kubwa lakini ahadi yangu kwao ni sitawaangusha, nitapambana kuonyesha kipaji changu ili nipige hatua zaidi, haya ndio maisha yangu.”

“Naamini kupitia soka nitasaidia familia yangu ambayo ilitoa baraka zote kwa kijana wao niende kujaribu bahati yangu Uturuki ambako nafasi ilionekana kupatikana,” anasema.

Akiwa Uturuki, Shaffih atakuwa akisimamiwa na Firat Totik anayeamini kijana huyo anaweza kuwa Mbwana Samatta ajaye kwa Tanzania.

“Nimeona wachezaji wengi wa Kitanzania wenye uwezo mkubwa lakini kwa uzoefu nilionao wa kutambua vipaji, nadhani Shaffih anaweza mchezaji mkubwa, kikubwa ni watu kuendelea kuweka wazi macho na masikio yao kwake, ana kila kitu, anaweza kukua zaidi.

“Alipofika tu Tuzlaspor makocha walivutiwa naye, waliuliza anatokea wapi, tukasema ni Tanzania walishangaa kuona nchi kama Tanzania inaweza kuwa kijana mwenye kipaji kama chake, ni mwepesi akiwa na mpira, ni mbunifu sana,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Muyimba Gerald amemtakia kila la kheri Shaffih huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi zao za kutaka Tanzania iwe na wachezaji wengi wa kulipwa nje ya nchi.

Mtendaji huyo anaamini kama Tanzania itakuwa kama mataifa ya Afrika Magharibi kwa kuwa na wachezaji wengi wa kulipwa barani Ulaya itasaidia kufanya vizuri kwa timu ya taifa.

“Itapendeza siku moja kuona Tanzania ikishiriki Kombe la Dunia, sisi kama AYE lengo letu ni kufungulia dunia wachezaji wa Kitanzania wale ambao tutaona wana vipaji, mchakato wetu wa kusaka vipaji upo wazi, wale ambao walishiriki mwanzo wanaweza kuwa mashuhuda.

“Najua ni kiu ya wapenda michezo na Watanzania kijumla kuona timu zetu za taifa zikifanya vizuri hata upande wa vijana, taasisi yetu imejitoa kwa namna ambavyo tunaweza ili kufanikisha hilo kwa taifa, yeyote ambaye atataka kuungana nasi milango ipo wazi,” anasema kiongozi huyo wa AYE akisisitiza mchakato mwingine wa kusaka vipaji wataufanya mwakani.

Columnist: Mwanaspoti