Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali yetu inapotubu dhambi bila kuungama

Bajeti Mwigulu Serikali yetu inapotubu dhambi bila kuungama

Thu, 22 Jun 2023 Chanzo: mwanachidigital

Juni 15, 2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba alisoma bungeni Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023-2024 na kuliomba Bunge liidhinishe mapato na matumizi ya Sh44.4 trilioni.

Ukurasa wa 113 hadi 115 ni mabadiliko ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290. Serikali inapendekeza punguzo la tozo za mabango ya biashara kutoka Sh10,000 hadi Sh7,000 (kwa yasiyowaka taa) na Sh10,000 kutoka Sh13,000 (yenye kuwaka taa).

Hoja ipo ukurasa wa 113 wa hotuba ya bajeti. Serikali inaomba kuhamisha majukumu ya kukusanya ushuru wa mabango, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na sasa makusanyo yafanywe na Tamisemi. Ombi hilo limeelekezwa pia kwenye kodi za majengo, kwamba sasa Tamisemi ikusanye badala ya TRA. Also Read

Sh40 bilioni kutolewa na Serikali kuongeza ununuaji wa mbolea Kitaifa 10 min ago Lema afichua sababu vijana kushindwa kuoa, kuwapeleka watoto kwa bibi zao SIASA 10 min ago

Serikali, kupitia Bajeti ya 2016-2017, ilibadili sheria. Kodi za majengo na mabango zikahamishwa kutoka Tamisemi na jukumu la makusanyo likakasimishwa kwa TRA. Uamuzi huo, kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na siasa.

Uchaguzi Mkuu 2015, uliiwezesha Chadema kushinda halmashauri za majiji yote makubwa, kasoro Tanga. Dodoma haikuwa jiji wakati huo. Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza, majiji yenye kuongoza kwa mapato makubwa nchini, yalitwaliwa na Chadema.

Kipindi ambacho Tamisemi wananyang'anywa mamlaka ya kukusanya kodi za majengo na mabango, tayari walikuwa wameshathibitisha ufanisi mkubwa. Ilala na Kinondoni, peke yake, halmashauri hizo zilikuwa zinakusanya Sh25 bilioni, kodi za mabango kwa mwaka. Hapo Temeke haijatajwa.

Ufanisi wa Tamisemi ni kwa sababu mamlaka yake yapo mitaani. Wenyeviti wa mitaa na wajumbe, walikuwa wakifanya kazi moja kuhakikisha ujumbe unafika kwa wakati na kodi stahiki zinakusanywa. Asilimia 20 ya makusanyo, yalibaki mtaani kuhudumia mitaa yao, hivyo kuhamasisha wenyeviti na wajumbe kufanya kazi kwa bidii.

Majukumu yalipohamishiwa TRA, hali ikawa tofauti. Mamlaka hiyo haina nyenzo za kufikia wananchi nyumba kwa nyumba, zaidi ya kutumia fedha nyingi kulipa magari, kuweka mafuta na posho za watangazaji, wapite mitaani kuhamasisha ulipaji wa kodi za majengo na mabango. Pamoja na hivyo, mwitikio ulikuwa hafifu.

Baada ya miaka saba, Serikali imeona irejeshe majukumu kwa Tamisemi ili kupata ufanishi wa awali. Hivyo, uamuzi wa sasa ni toba ya dhambi iliyofanyika kwa sababu za kisiasa. Tatizo, Mwigulu hajaitamka dhambi, ila kwa anayeijua, inaonekana dhahiri.

Uamuzi wa kuinyang'anya Tamisemi mamlaka ya kukusanya kodi za majengo na mabango, ulitafsiriwa kuwa ulilenga kuwakomoa wapinzani. Walishinda halmashauri nyingi, tena zenye mapato makubwa. Kitendo cha kuipa TRA majukumu ya Tamisemi, kilionekana ni kuwafanya wapinzani wasiwe na mapato makubwa, hivyo wafeli katika uongozi wao.

Je, Tamisemi wanarudishiwa majukumu ya kukusanya kodi za majengo na mabango kwa sababu Rais ni Samia Suluhu Hassan au kwa kuwa halmashauri zote kwa sasa zinaongozwa na CCM? Uchaguzi Mkuu 2025, wapinzani wakinyakua halmashauri nyingi na CCM kuendelea kuongoza serikali kuu, hayataletwa mabadiliko mengine?

Vipi chama kingine kikichukua dola, halafu halmashauri nyeti zikiwa chini ya vyama vingine, je, hayatajirudia yaliyotendeka miaka saba iliyopita? Kwa nini Serikali inarejesha mamlaka ya kodi za mabango na majengo Tamisemi, pasipo kukiri (kuungama), dhambi ya kisiasa iliyoitenda?

Kuna wakati Serikali iliamua kodi za majengo zitozwe kwenye manunuzi ya umeme kwa njia ya Luku. Likasababisha manung'uniko mengi. Mwanaharakati Rosemary Mwakitwange, aliweka hadi kusudio kwa kwenda mahakamani kupinga hili.

Kuanzia Januari 2024, mzigo wa kodi za majengo utaondolewa kwenye Luku. Hili liwe fundisho kwa Serikali, inapotenga bajeti zake, ihakikishe inaunda vyanzo vinavyotekelezeka. Kujifungia na kuamua, ndiyo kuibuka na tozo za kwenye Luku ambalo zinaumiza watu na kusababisha zogo la kitaifa.

Taifa la wacheza kamari

Katika hotuba hiyo, jedwali namba tano, linaonyesha mgawanyo wa bajeti kisekta. Sehemu inayoonyesha "Maendeleo ya Uchumi", utaona kuwa Vijana, Kazi na Maendeleo ya Kukuza Ujuzi, fedha ambazo zimetengwa ni Sh20.3 bilioni. Zikiwa zimepungua kutoka Sh31.2 bilioni, mwaka wa fedha unaoishia, yaani 2022-2023.

Taarifa hiyo itakushitua mno ukisoma ripoti ya uchumi wa michezo ya kubahatisha Tanzania. Mwaka wa fedha 2018-2019, mapato ya michezo ya kubahatisha yalikuwa Sh96 bilioni. Yakiwa yamepanda kutoka Sh78 bilioni, mwaka uliotangulia. Hiyo ni ripoti ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Mtandao wa utafiti na takwimu za kibiashara kwenye tasnia mbalimbali duniani, Statista Market Forecast, inaeleza kuwa mapato ya michezo ya kubahatisha Tanzania mwaka 2023, yanatarajiwa kufikia dola 75.09 milioni (Sh180 bilioni).

Kwa mujibu wa Statista, thamani ya soko la michezo ya kubahatisha Tanzania itakuwa dola 110.1 milioni (Sh260.4 bilioni), ifikapo mwaka 2027. Hali ikiwa hivyo, Serikali inapunguza fedha kwenye eneo la upishi wa vijana kuwa wataalamu.

Sehemu VI ya bajeti, inayoainisha "Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada, Tozo na Hatua Nyingine za Mapato", kipengele (n), Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41. Utaona kuwa mkazo mkubwa kwa sasa ni serikali kukusanya mapato kwenye michezo ya kubahatisha.

Serikali pia inakwenda kupunguza maumivu kwa wachezesha kamari, kwa kuwapa punguzo la kodi kwenye mapato ghafi, kutoka asilimia 25, hadi asilimia 18. Hapa maana yake waendeshaji wa kamari, wataona ahueni zaidi. Wakati huohuo, Serikali inapandisha bei ya leseni na tozo za michezo.

Ukiachana na bajeti kuu ya Serikali, Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha 2023-2024, inaonesha kuwa hadi Aprili 2023, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, ilishatoa leseni 8,778 za michezo ya kamari. Hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 114 ya malengo. Mwaka ujao wa fedha, leseni mpya 11,880, zitatolewa.

Ufafanuzi huo, unamaanisha kuwa mkazo wa kukuza sekta ya kamari ni mkubwa, wakati huohuo uwekezaji kwa vijana ni mdogo. Maneno ni mengi kuanzia nyumba za ibada hadi kwa wanasiasa, kwamba vijana wasiwe waraibu wa kamari, badala yake wafanye kazi za vipato.

Kamari au michezo ya kubahatisha, kama ilivyo jina lake, inapaswa kuchukuliwa kama michezo ya kujaribu bahati na kujifurahisha. Hivi sasa, vijana wengi, tena siku hizi hadi wazee, wamegeuza kuwa michezo ya kubahatisha ni vyanzo vya mapato.

Serikali, kwa kutambua hilo, inapaswa kuwekeza vizuri kwenye eneo la vijana. Kuwajengea ujuzi na uwezo. Waweze kujiajiri au kuajiriwa. Wimbi la vijana kuona michezo ya kubahatisha ni fursa za kimaisha, hadi kuwa mateja wa kamari, ni matokeo ya kukosa machaguo (options) ya kimaisha.

Siri ni moja tu, eneo lenye uchumi mkubwa hukimbiliwa na wengi. Watanzania wamejazana Dar es Salaam kwa sababu ndio mkoa wenye mzunguko wa kifedha uliotanuka kuliko mikoa mingine yote. Biashara ya dawa za kulevya inapigwa vita duniani kote, ila inazidi kushamiri.

Sababu ni hii; Taasisi ya Global Financial Intergrity ya Marekani, ilitoa ripoti ya makadirio ya mzunguko wa kifedha kwenye biashara ya dawa ya kulevya. Iliandika kuwa mwaka 2014 peke yake, dawa za kulevya zilitengeneza mapato ya dola 652 bilioni (Sh1,562 trilioni).

Kiwango hicho kikubwa cha fedha, ndicho kinashawishi watu kukimbilia utajiri wa haraka. Kuna wanaokufa na wengine wanafungwa maisha. Bado kasi ya wahalifu inachipua kwa kasi. Fedha ndio kivutio. Mzunguko wa kifedha kwenye michezo ya kubahatisha, unashawishi vijana kuuona utajiri wa ghafla bin vuu kwa kucheza kamari.

Bajeti inayoombwa kwa ajili ya Wizara ya Madini kwa mwaka ujao wa fedha ni Sh89 bilioni. Maana yake inazidiwa mbali na mapato ya michezo ya kubahatisha. Habari, Michezo na Utamaduni, bajeti ni Sh35.4 kama ilivyokuwa mwaka jana. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Sh173.3 bilioni.

Rejea matarajio ya mapato ya michezo ya kamari kuwa Sh260 bilioni ifikapo mwaka 2027, halafu pitia fungu la Biashara na Viwanda kuwa Sh324.2 bilioni. Je, huoni dalili za michezo ya kubahatisha kuelekea kushindana na sekta nyeti; Viwanda na Biashara?

Miaka nane iliyopita, Tanzania ikiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, aliyekuwa Mgombea Urais wa CCM, John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan, waliinadi Tanzania ya viwanda. Miaka miwili baadaye, ikawa Tanzania ya Standard Gauge (SGR) na Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP).

Uchaguzi Mkuu 2020, Magufuli hakuhubiri viwanda, bali SGR na JNHPP. Magufuli alipofariki dunia na hatamu kushikwa na Samia, mkazo umeendelea kwenye SGR na JNHPP. Sasa, matokeo ndio haya, kwamba mapato ya kamari, yanakwenda kukimbizana na bajeti ya Biashara na Viwanda.

Uchambuzi anuwai

Uwekezaji kwenye Elimu ni mkubwa na huu umekuwa mwendo mzuri wa Rais Samia. Sh5.685 trilioni mwaka unaoisha, mwaka ujao ni Sh5.952 trilioni. Katika mgawanyo wa mafungu ya bajeti, Elimu inashika nafasi ya pili, nyuma ya fungu la Huduma za Utawala ambalo ni pana, linalojumuisha hadi Deni la Taifa. Lenyewe limetengewa Sh18.2 trilioni.

Punguzo la ushuru wa bidhaa kwa asilimia 56, ni ahueni mno kwa wenye viwanda. Kumekuwa na kilio cha muda mrefu, wawekezaji wakilia na mazingira magumu ya kuendesha biashara Tanzania. Zaidi, Serikali imekuwa ikipata fedha nyingi kuliko wanaowekeza mitaji yao.

Sauti za wafanyabishara wa Kariakoo zimesikika. Moja ya malakamiko yao kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kima cha chini cha mtaji kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwa Sh100 milioni. Bajeti mpya inataka mabadiliko ya kima cha chini kuwa Sh200 milioni na uelekeo ni kufikia Sh500 milioni.

Kilimo, fedha zilizotengwa ni Sh1.465 trilioni. Kwa miaka miaka miwili mfululizo, Serikali imeonesha nia ya dhati ya kumkomboa Mtanzania, maana asilimia 80, wanategemea kilimo. Mwaka unaoisha sekta hiyo ilitengewa Sh1.216 trilioni. Pamoja na hivyo, changamoto ipo kwenye usimamizi.

Miezi miwili iliyopita, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, alionesha jinsi fedha za Serikali zisivyosimamiwa vizuri. Vilevile, wakulima wamekuwa wakilia pembejeo wakati Serikali imetenga fedha nyingi za ruzuku. Hivyo, tatizo kubwa la Serikali wakati mwingine sio vipaumbele, bali nidhamu na uadilifu wa fedha.

Columnist: mwanachidigital