Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali ya Rais Magufuli imewekeza katika maendeleo makubwa ya watu

56b83f133d106d214892c5235663b3dd Serikali ya Rais Magufuli imewekeza katika maendeleo makubwa ya watu

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Ni habari njema katika utekelezaji wa sera za maendeleo ya taifa, pale nchi yetu ya Tanzania inapoingia katika uchumi wa kati.

Lakini habari ya kutia moyo zaidi ni kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli, kuzidi matarajio ya malengo ya utekelezaji wa sera za maendeleo ya nchi, kwa kuifanya nchi ifikie katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda wa malengo kufikia.

Kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’ imeonesha matunda, na ama kwa hakika kazi inaleta hamasa zaidi kwa watekelezaji, pale wanaposhuhudia matunda yake. Lakini, kwa Rais Magufuli na serikali yake kazi hii haikuwa nyepesi.

Siku za hivi karibuni tulisikia malalamiko yaliyochochewa na baadhi ya wanasiasa, wakiutuhumu uongozi wa Rais Magufuli, kuendesha siasa za kujinyima na kujibana sana kiuchumi huku fedha zikielekezwa kwenye miradi wanayoiita white elephant projects yaani miradi isiyotekelezeka.

Waswahili wana methali isemayo ‘Akutukanaye hakuchagulii tusi’. Methali hii inarandana na msemo wa mtu anayekuchukia hakuchagulii jina, maana atakuita jina lolote alimradi amekuudhi.

Kwa maneno mengine watu hao walishawishi tuikatae kaulimbiu ya ‘HAPA KAZI TU’ na wakaanzisha ya kwao ya ‘KAZI NA BATA’.

Lakini ukifanya tathmini ya kina, utagundua kuwa kauli mbiu yao ya ‘KAZI NA BATA’ ilikuwa propaganda za kisiasa tu. Makala haya yatadadavua kwa kina mapungufu ya propaganda hiyo na kuonesha kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati, uongozi wa Rais Magufuli umewekeza katika maendeleo ya watu.

Kwanza nianze kwa ufafanuzi juu ya miradi mikubwa na ya kimkakati. Watanzania wanapaswa kujivunia uthubutu na uthabiti wa Rais Magufuli katika kuianzisha na kuitekeleza miradi hiyo.

Kwa mfano, ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge (SGR) ni mradi wa kimkakati ambao utachangamsha sana uchumi wetu. Tanzania imekuwa na utegemezi mkubwa wa barabara, kusafirisha abiria na mizigo na ndio maana ajali zinaongezeka, barabara zinaharibika kila siku na kuathiri uchumi wetu.

Wakulima vijijini wamekosa faida katika mazao yao, kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji wa mazao na pembejeo ni finyu. Reli ni suluhisho la kudumu kwa kero hizo.

Lakini, pia reli hii itasafirisha mizigo nchi jirani za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda na kuleta hamasa kubwa ya matumizi ya bandari zetu.

Watanzania wazalendo hawana budi kumuunga mkono Rais Magufuli katika ujenzi wa Reli ya Standard Gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga sambamba na uboreshwaji wa bandari ya Mtwara ili kuwafanya watu wa Malawi, wapatao takribani milioni 19 watumie bandari yetu.

Miradi hii ya reli ya kisasa ni uwekezaji utakaoleta faida kubwa kwa nchi yetu. Pili, uboreshaji wa Kampuni ya Ndege nchini (ATCL) kulikotokana na manunuzi ya ndege mpya na kuanzishwa kwa vituo vya ndege nje na ndani ya nchi, ni jambo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na katika kuchagiza ukuaji wa sekta ya utalii nchini.

Sote tunatambua kuwa Tanzania inaongoza barani Afrika kwa vivutio vya utalii. Hivyo, kufufua kampuni ya ndege kumeifanya nchi kulikamata soko letu la ndani, baada ya kuanzisha vituo vya ndege vya ndani 8 zaidi kufikia jumla ya vituo 13.

Uwekezaji huu wa kimkakati unarahishisha huduma ya kusafirisha watalii nchini, lakini pia kuwezesha usafirishaji wa haraka wa rasilimali muhimu na watu katika sekta zingine.

Pamoja na uwekezaji mkubwa ambao serikali inafanya katika ujenzi wa barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa hapa nchini, pia kumekuwepo na ukarabati wa reli za zamani na ujenzi wa meli na vivuko vyote.

Hatua zote hizo zimelenga kufungua na kurahisisha usafirishaji nchini. Lakini pia mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere ni wa kimkakati mno kwa masilahi mapana ya nchi yetu.

Bwawa hilo lina uwezo wa kufua umeme wa Megawati 2,115, ambao utaiwezesha nchi kupata umeme wa uhakika na pia utawasaidia wananchi kunufaika na huduma ya nishati hiyo muhimu kwa gharama nafuu.

Mwisho wa siku kama kauli mbiu yetu ya Tanzania ya Viwanda inavyohamasisha, upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha, utasaidia kukuza uchumi wa viwanda vikubwa na vidogo.

Pamoja na uwekezaji huo mkubwa wa kimkakati na wenye tija kwa ukuaji wa uchumi, bado Serikali ya Rais Magufuli imefanya uwekezaji katika huduma na maendeleo ya watu kwa mafanikio makubwa.

Watu wanaodai serikali hiyo haijawekeza katika huduma za jamii, wanapiga porojo tu. Kwa mfano, ripoti ya Mkutano wa Umoja wa Kimataifa Juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD, 2018) ya tathmini ya maendeleo ya nchi maskini zaidi duniani, iliielezea Tanzania kuwa ilikuwa imeshavuka katika kigezo cha uhimilivu wa kiuchumi, lakini bado ilikuwa imekwama katika vigezo viwili ambavyo ni pato la wastani la kila Mtanzania, lililosimama kwenye Dola za Marekani 902 na kigezo cha ustawi wa rasilimali watu, yaani Human Assests Index, ambacho ilikuwa chini ya kizingiti cha kufikia lengo la kuingia katika uchumi wa kati.

Kazi ngumu na yenye kuhitaji fikra na upeo mkubwa, iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano imefanikisha kuleta mabadiliko makubwa katika vigezo hivyo viwili vilivyobaki.

Watanzania wanatakiwa kukumbuka kuwa kwa mujibu wa UNCTAD, kigezo cha ustawi wa rasilimali watu kinagusa maeneo matano ambayo ni: Vifo kwa watoto chini ya miaka mitano, uandikishwaji wa wanafunzi shuleni, kujua kusoma na kuandika kwa watu wazima, vifo vinavyotakana na uzazi na utapiamlo.

Serikali imefanya uwekezaji wa kuridhisha katika huduma ya mama na mtoto, ambapo vituo 487 vya afya vimejengwa nchi nzima. Uwekezaji huo umeongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia hospitali kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi 83 mwaka 2020, na muhimu zaidi idadi ya vifo vya wachanga, vimepungua kutoka 25 hadi 7 tu kwa jumla ya watoto 1,000.

Katika kigezo cha utapiamlo, serikali imetekeleza miradi ya lishe nchini kwa matokeo makubwa mno. Kwa mfano, hali ya udumavu kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano, imepungua kutoka asilimia 34.7 hadi 31.8 wakati huo huo ukondefu umeshuka kutoka asilimia 3.8 hadi 3.5.

Ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi shuleni ni moja ya mafanikio makubwa ya sera ya elimu bure inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Ongezeko hilo linaanza na idadi za shule za msingi na sekondari na pia idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni.

Kwa mfano, kwa shule za msingi uandikishwaji umeongezeka kutoka 8,298,282 mwaka 2015 hadi 10,938,156 mwaka 2020. Kwa shule za sekondari uandikishwaji umeongezeka kutoka 1,648,359 mwaka 2015 hadi 2,185,037 mwaka 2020. Mbali na vigezo vya UNCTAD, serikali pia imesambaza umeme vijijini kupitia mradi wa REA kwa mafanikio makubwa kutoka vijiji 2,081 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwaka 2020.

Lakini, pia imesambaza huduma ya majisafi na salama mijini na vijijini kwa mafanikio makubwa hivyo kuweza kupunguza magonjwa ya milipuko yatokanayo na ukosefu wa maji.

Matunda ya wazi na yanayoonekana kutokana na jitihada za serikali kuwekeza katika maendeleo ya watu, ni kupungua kwa umaskini wa mahitaji ya msingi.

Takwimu zinaonesha kuwa kwa mijini umaskini ulipungua kutoa asilimia 21.7 hadi 15.8 na vijijini umaskini ulipungua kutoka asilimia 33.3 hadi 31.2 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Takwimu hizo za kuvutia, zinakuja kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.

Kama Rais Magufuli angekuwa ni kiongozi wa kubana matumizi kama inavyodhaniwa, angeelekeza nguvu zaidi kwenye miradi ya kimkakati tu na siyo kuwekeza katika huduma za jamii na maendeleo ya watu.

Labda sifa inayomfaa Rais Magufuli si ya kubana matumizi, ila ya kuhimiza matumizi sahihi ya fedha za kodi za wananchi. Tukumbuke kuwa huko nyuma fedha nyingi za serikali zilikuwa zinatumika vibaya, ikiwemo kuendesha semina zisizo na tija kwa taifa.

Kwa mfano, serikali iliacha kutumia fedha za Sherehe za Uhuru mwaka 2015, badala yake zilitumika kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia, hatua kama hiyo ilisaidia kupatikana kwa barabara pana na bora ya Morocco-Mwenge jijini Dar es Salaam hivyo kupunguza msongamano wa magari, uliokuwa unaleta hasara kubwa ya matumizi ya mafuta na muda.

Sasa katika muktadha wa uwekezaji huo wa miradi ya kimkakati na uwekezaji katika huduma za jamii na maendeleo ya watu, unajiuliza huyu anayetaka ‘KAZI NA BATA’ angepewa uhalali wa kisiasa wa kuongoza nchi na kutekeleza sera zake, angefanya nini zaidi ya alichokifanya Amiri Jeshi wetu Rais Magufuli? Kwa hakika Watanzania wanapaswa kuyaelewa maono ya mbali ya Rais Magufuli ;na hawapaswi kuyumbishwa na propaganda zisizo na uelekeo kwa maisha yao na maendeleo ya Tanzania.

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili.

Columnist: habarileo.co.tz