Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali imekuwa ikichukua hatua muda wote kukabiliana na corona

Cb33520a475f09ae238367c63b80d406 Serikali imekuwa ikichukua hatua muda wote kukabiliana na corona

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MACHI 16, mwaka 2020, Tanzania ilitangaza rasmi kupata mgonjwa mmoja wa virusi vya corona (COVID-19) na idadi iliendelea kuongezeka hadi kufikia waathirika 509 na vifo 21 kwa mujibu wa taarifa rasmi za serikali hadi sasa.

Janga la COVID-19, limeyakumba mataifa mengi duniani na chanzo la tatizo hilo lilianzia nchini China kwenye Jimbo la Wuhan ambapo mwishoni mwa mwaka 2019 taarifa za uwepo wa ugonjwa huo zilianza kuripotiwa na hatimaye kadri siku zilivyosonga, ndivyo kasi ya maambukizi yalivyoongezeka.

China ilianza kuchukua hatua mbalimbali za kuudhibiti, ikiwa ni pamoja na kuzuia watu kutoka nje, kusafiri nje ya jimbo hilo huku wakielekeza jinsi ya kujikinga kwa kufuata kanuni zote za afya zilizotolewa kudhibiti maradhi hayo.

Hata hivyo, baada ya muda kidogo, ugonjwa huo uliendelea kusambaa katika nchi mbalimbali hatimaye kufika bara la Afrika na Tanzania ikiwemo na serikali ikachukua hatua ili kuwakinga wananchi wake dhidi ya janga hilo.

Moja ya jitihada zilizochukuliwa ni serikali chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli ni utoaji wa elimu kwa umma juu ya ugonjwa huo mpya wa COVID-19 sambamba na wataalamu wa afya na kamati husika zikielezea na kutoa vipeperushi vya dalili za ugonjwa na nini kifanyike.

Mambo muhimu yaliyotolewa ya kuzingatia kwa wananchi yalikuwa ni umuhimu wa usafi hadi kunawa mikono kwa kutumia sabani na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuepuka msongamango na kukaa umbali wa mita mbili kati ya mtu na mtu na uvaaji wa barakoa.

Katika kusisitiza hilo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto wakati huo, Ummy Mwalimu alitoa maelekezo na taarifa kwa umma juu yah atua zinazochukuliwa na serikali katika mapambano ya COVID-19.

Moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali ni kufunga shule na vyuo nchini kwa muda ili kuzuia kuenea au kusambaa kwa virusi hivyo, sambamba na kutaka maeneo ya kazi watumishi kuchukua hatua zilizoainishwa na ikiwezekana kutimiza wajibu wao kwa njia ya mtandao pale inapibidi.

Aidha, serikali kupitia maagizo ya wizara ya afya na waraka wa wasafiri wanaoenda au kuingia nchini iliweka vituo vya karantini kwa wale wote wanaotoka nje ya nchi hususani kwenye nchi zilizokuwa na maambukizi ya kiwango cha juu lakini pia serikali lilianzisha kambi za kuhudumia waathirika wa COVID-19.

Kambi hizo zilikuwa kwenye hospitali zote za mkoa nchini, hospitali maalumu na vituo maalumu vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia waathirika baada ya kupimwa na kubainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Katika kambi hizo kwa jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo lenye idadi kubwa ya watu na mwingiliano mkubwa wa watu lilikuwa na kambi maeneo tofauti, ikiwemo kambi la Mloganzila, Amana, Hospitali ya Mwananyamala, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Temeke na hospitali nyingine binafsi.

Vituo hivyo vilipokea waathirika na kuwapa huduma za tiba huku vikiangalia afya zao kuimarika.

Mbali na hatua hizo, serikali ilichukua hatua nyingine zaidi ikiwemo kufunga shughuli zote za michezo na kuzuia mikusanyiko sherehe za harusi na nyingine kama hizo na pia kutoa muongozo kwenye shughuli za maziko kwa kuruhusu idadi ndogo ya waombolezaji.

Hizo zote ni hatua zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya corona na hadi kufikia Disemba mwaka 2020, Rais Magufuli alisema nchi ilifanikiwa kukabiliana na janga hilo ukilinganisha na mataifa jirani na nchi nyingine.

Moja ya mafanikio hayo kwa mujibu wa Rais Magufuli ni kuondoa hofu ya ugonjwa huo na kuhimiza wananchi kufanya kazi kwa bidi lakini kwa kuchukua tahadhari, jambo ambalo lilipata mwitikio mkubwa na kusaidia kukabili janga hilo.

Katika hatua hizo, nyumba za ibada nazo zilifuata utaratibu uliotolewa na serikali wa kuepuka misongamano na waumini kuketi umbali wa mita mbili baina ya muumini mmoja na mwingine lakini pia uvaaji wa barakoa na kuzuia watu kusalimiana kwa kushikana mikono.

Katika hilo, miongozo ya serikali ilifika pia kwenye vyombo vya usafiri, ambavyo kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), na vyombo vingine vya serikali wakiwemo polisi wa usalama barabarani walihakikisha kila gari la abiria linabeba idadi ya abiria hao kulingana na idadi ya vitu na hakuna ruhusa ya kupakia zaidi ya hapo.

Hatua hiyo, ilisaidia kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona na pia maeneo karibu yote yanayotoa huduma yaliweka masharti kwamba ili kuhudumiwa ni lazima mtu awe amevaa barakoa.

Awali Shirika la Afya Duniani (WHO), liliyataka mataifa duniani kuchukua hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo huku taarifa mbalimbali zilizotolewa kama tathmini kwa nchi ziliopata athari kubwa zikionesha kuwa Bara la Afrika litaathirika zaidi, lakini haikuwa hivyo.

Wakati Tanznaia ikipambana na janga hilo, nchi mbalimbali duniani zilipitisha amri ya zuio la watu wake kutotoka nje au kusafiri ili kujikinga na kuenea kwa COVID-19 ambapo nchi jirani ya Kenya, Rwanda, Zambia na Uganda zilifunga mipaka.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitoa agizo hilo Mei mwaka 2020 na kusisitiza kwamba amefunga mikapa yake na nchi ya Tanznaia na nchi nyingine jirani kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Wakati juhudi za kuzuia maambukizi zikiendelea, Rais Magufuli alitoa mwito kwa wataalamu wa tiba asili na mbadala kufanya utafiti na kutumia miti ya asili iliyokuwa ikitumika kutibu maradhi mbalimbali ili itumike kusaidia kupambana na corona.

Katika hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Dawa Asili wa Chuo Kikuu cha Tiba Shirikishi cha Muhimbili( MUHAS), Dk Joseph Otieno, anasema kujifukiza ni tiba ya muda mrefu iliyokuwa ikitumika katika jamii mbalimbali nchini na ilionesha matokeo chanya.

Dk Otieno anaamini kwamba tiba hiyo ikitumika vizuri, husaidia kuboresha mfumo wa upumuaji na kuusaidia mwili kupata nguvu ya kupambana na maradhi.

Hata hivyo, anashauri miti inayofaa ni ile tu iliyofanyiwa utafiti wa kisayansi na kudhibitishwa na kuwa na machapisho ndiyo inaruhusiwa kutumika kama tiba asili na sio vinginevyo.

Baadhi ya miti hiyo ni pamoja na mkaratusi, mipera, mchaichai na kivumbasi ambavyo anasema ina mafuta tete muhimu kwa ajili ya kusaidia mfumo wa upumuaji wa mwanadamu.

Hata hivyo, juhudi za kupambana na COVID-19 nchini zimeendelea kuchukuliwa kwani itakumbukwa Januari mwaka huu, Rais Magufuli alisema nchi inachukua tahadhari zote za kupambana na corona na kusema suala la chanjo ni lazima nchi ifanye uchunguzi wake kwa sababu chanjo inahusu afya ya watu.

Katika hilo, Rais Magufuli alishauri wataalamu wajiridhishe kabla ya kukimbilia kupokea chanjo hiyo kwa sababu baadhi ya mataifa yaliyopokea na kuanza kuwachanja watu wake, baadhi zimeonesha madhara na kuzuiwa kutumika.

Katika juhudi za kusaidia nchi kupambana na janga hilo, wadau wa maendeleo zikiwemo nchi za China na nyingine, zilitoa msaada wa vifaa tiba na barakoa kama msaada wao wa kuisaidia Tanzania kupambana na corona.

Hayo yote yamefanywa ndani ya serikali ya Tanzania kama hatua za kupambana na corona, na hivyo kupingana na dhana ya baadhi ya mataifa na taasisi zilizoripoti kuwa nchi haichukui hatua zozote kukabiliana na COVID-19.

Columnist: www.habarileo.co.tz