Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serengeti muwakilishe vyema Cecafa

Youths 15 Serengeti muwakilishe vyema Cecafa

Sat, 12 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya Taifa ya Soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti boys inatarajiwa kushuka dimbani leo dhidi ya wenyeji Rwanda katika mchezo wa kwanza wa makundi wa michuano ya Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Tanzania iko katika kundi B lenye timu tatu, baada ya kucheza na Rwanda itachuana na Djibout.

Baadhi ya timu zilizopita za umri huo zilifanya vizuri katika michuano ya aina hiyo mwaka jana na mwaka juzi.

Serengeti kabla ya kutua Rwanda ilikwenda kuweka kambi Morocco kwa maandalizi hivyo inatarajiwa kuwa maandalizi mazuri waliyofanya watapeperusha vyema bendera ya taifa.

Inachopaswa kujua timu hiyo ni kutowadharau wapinzani bali kuwaheshimu na kufanya vizuri kwa maelekezo ya makocha wao.

Ni imani ya watanzania wengi kuwa kama ambavyo ndugu zao walikuwa wakiwakilisha vyema huko nyuma na wao sio tu wamekwenda kushiriki bali kushindana.

Wakifanya vizuri mashindano hayo wanapata nafasi zaidi ya kujihakikishia ushiriki wa michuano mikubwa ijayo baadaye ya Afrika.

Kushiriki mashindano kama hayo kuna faida nyingi kwa vijana kwanza kuna nafasi ya kupandishwa hadi katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20.

Na unapopandishwa maana yake umeaminiwa na kupewa heshima na ndio unakuwa mwanzo wa safari ya maisha ya kisoka kwa wale wenye ndoto kubwa.

Kujituma kwao kunaweza pia kuwapa ulaji kama ilivyo kwa baadhi ya waliopita walichukuliwa na klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa wanaokula matunda ni Nikson Kibabage anayecheza soka la kulipwa Morocco, Ally Ng’azi anayecheza soka la kulipwa Marekani, Kelvin Nashon yupo JKT, Kibwana Shomari anayecheza Yanga na wengine kadhaa wapo klabu mbalimbali za Azam FC, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na kwingine.

Macho ya watanzania siku zote hupenda na kuunga mkono timu inayofanya vizuri. Na huku kwenye soka la vijana ndiko kwenye matumaini zaidi.

Kaka zao chini ya umri wa miaka 20 Ngorongoro heroes wamefanya vizuri katika michuano ya Cecafa kwa umri huo ilifanyika Arusha hivi karibuni.

Walimaliza nafasi ya pili baada ya kufungwa na Uganda mabao 4-1 katika mchezo wa fainali. Licha ya kushindwa kuchukua ubingwa imefuzu kucheza fainali za Afrika za vijana zitakazofanyika baadaye Mauritania.

Kile walichokionesha kaka zao, basi wao wafanye mara mbili kuonesha ubora kwasababu kama ni maandalizi walifanya kwa muda mrefu hawana pa kuficha nyuso zao.

Kutokana na kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo ya kuwakilisha taifa kwa hakika watafanya vizuri.

Yote yanawezekana kwa juhudi na moyo wa upambanaji wa kupigania matokeo, jambo la muhimu ni kuzingatia kile walichoelekezwa katika maandalizi yao.

Wapinzani wao Rwanda ni wazuri na wamekuwa wakiwekeza katika soka la vijana kwa hiyo zitakutana timu mbili zitakazokuwa na ushindani wa hali ya juu.

Kwa upande wa Djibout hawapaswi kubezwa kwani miaka ya karibuni wamekuwa wakibadilika huenda wakaleta upinzani kama Serengeti itawadharau.

Lakini yote kwa yote, Serengeti bado ni bora wana wanaweza kufanya kile ambacho wameagizwa na kuleta ushindi kwa watanzania.

Kila la heri kwao!

Columnist: habarileo.co.tz