Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sebo aliacha lindo kisa soka

Sebo Pic Sebo aliacha lindo kisa soka

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kukosekana kwa misingi imara ya kuendeleza vipaji kunachangia kuwanyima vijana fursa ya kutajirika kupitia fani mbalimbali ikiwamo soka huku wachache wanaopata nafasi ya kutumia vipaji vyao wakibadili maisha yao na ya wanaowazunguka.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na beki wa Azam FC, Abdallah Kheri ‘Sebo’ ambaye amefunguka mambo mbalimbali huku akikiri kuwa soka limemfanya aweze kubadilisha maisha ya familia yake kwa kuwajengea nyumba ya kuishi.

Anasema pesa yake ya kwanza mara baada ya kupata nafasi ya kucheza soka Bara akisajiliwa na Azam FC aliitumia kuwajengea wazazi wake nyumba ya kuishi ili waweze kukubaliana na kipaji chake ambacho aliamua kukiendeleza na kuachana na ajira ya jeshi.

“Nakumbuka wazazi wangu waliamini sana katika kazi ya jeshi lakini mimi nilithamini zaidi kipaji changu ambacho niliamini ipo siku kitaweza kunitoa sehemu moja hadi nyingine,” anasema na kuongeza;

“Baada ya kupata nafasi ya kusajiliwa Azam FC namshukuru Mungu nilipata fedha nyingi nilifanya uamuzi wa kuwajengeza wazazi wangu nyumba ambayo wanaishi hadi sasa japo siwezi kuweka wazi kiasi nilichokipata lakini kiliniwezesha kujenga nyumba,” anasema na kuongeza kuwa mara baada ya kufanya hivyo wazazi wake wameanza kuunga mkono juhudi zake.

AKACHA LINDO KISA SOKA

“Nilianza kucheza timu ya mtaani ilikuwa inaitwa River Side chini ya Abdulhafidh Abasi maarufu kama ‘Kaka Chichi’ ambaye ndiye aliyekuwa kocha wangu na msimamizi kwenye misha yangu ya soka,” anasema na kuongeza;

“Nilipotoka River nilipata nafasi ya kucheza timu ya Fire ambayo ilinipa nafasi ya kusomea kozi ya uaskari wa zimamoto lakini ndoto ilikuwa ni kucheza mpira na niliendelea kucheza na nikapata bahati ya kuitwa timu ya vijana ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 20 chini ya kocha Stewart Hall,” anasema.

Anasema akiwa chini ya Hall, Stars ya vijana ndio alipata nafasi ya kuonekana na bahati yake ikaanzia hapo kwani wakiwa kwenye mechi ya mashindano kati ya timu ya taifa ya vijana (Under 20) na Nigeria ambayo walifungwa mabao 2-0, alionyesha ubora uliowashawishi matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC kumsajili.

WAZANZIBAR WANAFELI HAPA

“Kwa wafuatiliaji wa soka hawawezi kupingana na hiki ninachokisema Zanzibar imebarikiwa kuibua vipaji vingi sana na ina wachezaji wakubwa na wazuri ambao wakija Tanzania Bara wanaonyesha ubora lakini ligi yao haifanyi vizuri,” anasema na kuongeza;

“Sababu kubwa inayo iangusha ligi ya huko ni kukosa wadhamini, inasababisha ligi kukosa ubora na ushindani tofauti na Bara ambako uwekezaji mkubwa uliowekwa ndio unawafanya wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali kutamani kuta kucheza.”

Anasema endapo uwekezaji mkubwa ukifanyika kwenye ligi ya Zanzibar basi itakuwa na ligi yenye ushindani na kuendelea kukuza na kuendeleza vipaji vingi ambavyo vinapotea kutokana na nguvu ndogo ya fedha iliyopo kwenye ligi yao.

WAWA, AGGREY USIPIME

“Ni kweli nimecheza na mabeki wengi ndani ya misimu minne niliyocheza Azam FC nimepata bahati ya kucheza na wazawa pamoja na wageni, naweza kusema ubora wangu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na wao.” anasema na kuongeza;

“Pamoja na kucheza na wengi lakini nimevutiwa na ubora wa Aggrey Morris ambaye kwa namna moja ama nyingine amekuwa akinipa mbinu nyingi kwa kumfuatilia na kunipa maelekezo pale ninapocheza pamoja na yeye uwanjani.”

Sebo anasema kwa upande wa wageni aliopata nafasi ya kucheza nao hawezi kumsahau Pascal Wawa kutokana na namna alivyokuwa kiongozi kiwanjani na mwalimu nje ya uwanja wakikutana alikuwa ni mtu wa kumuelekeza mambo mengi.

“Wawa ni tofauti na wachezaji wengine wengi wa kigeni waliopita Azam FC hakuwa mchoyo wa ujuzi, alitamani kila mchezaji anayecheza nafasi ya beki awe na ubora kwani muda mwingi alikuwa akifundisha kwa vitendo na kuzungumza na mtu ili aweze kuimarika.” anasema beki huyo ambaye ameweka wazi kuwa mbali na kutumika zaidi nafasi ya beki wa kati pia ana ujuzi mzuri wa kucheza nafasi ya beki namba mbili.

KINACHOWATESA WACHEZAJI

“Kila kocha anapoingia kwenye timu anakuja na mfumo wake hivyo kama mchezaji unatakiwa kujitambua kuongeza nidhamu ili kumshawishi kocha aweze kukuelewa,” anasema na kuongeza;

“Sio rahisi kwa mchezaji kuendelea kuwa na ubora ule ule kutokana na mabadiliko ya mfumo na mazoezi ya mwalimu mwingine mbayo ili mchezaji aweze kuendna nayo anatakiwa kupewa muda lakini kabla hata haujaingia kwenye mfumo anaondolewa na kuletwa mwingine unatakiwa kuanza tena upya sio rahisi.”

Sebo anasema ili mchezaji aweze kuwa bora na kuendeleza kipaji chake anatakiwa kukaa chini ya kocha mmoja kwa muda ili kuweza kuisaidia timu pia kupata mafanikio lakini kama wachezaji watabadilishiwa makocha mara kwa mara ni ngumu kufikia malengo kutokana na wao pia kukosa mwendelezo wa ubora.

USIMUONE HIVYO SURE BOY

“Nakumbuka mambo mengi kutoka kwa Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni mtu ambaye alikuwa mcheshi sana na mtu ambaye muda mwingi alikuwa anapenda kuona kila mmoja anakuwa na furaha,” anasema na kuongeza;

“Mudathir Yahaya ndiye alikuwa mchezaji ambaye tulikuwa tunakaa pamoja tukiwa kambini mbali na hayo yote nimekua naye na nimesoma naye shule moja hivyo nikisema nimuelezee hapa sitamaliza leo, nawamiss sana, kuondoka kwao kuna kitu kimepungua kwenye maisha yangu ya kawaida.”

Anasema baada ya kuondokewa na wote ameanza kupya kutengeneza marafiki wapya kwasababu hao ni wachezaji ambao alikuwa anaishi nao na amewakuta ndani ya timu hiyo na walimpokea vizuri na kumfundisha namna ya kuishi vizuri ndani ya timu hiyo.

Columnist: Mwanaspoti