Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sasa tufute sherehe nyingine zinazotafuna mabilioni ya fedha

Sherehe Pic Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amefuta sherehe za Mapinduzi

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeamua mwaka huu kutokuwa na sherehe za kitaifa kuadhimisha miaka 59 tangu yafanyike Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.

Kutokana na uamuzi huo, Rais Hussein Mwinyi ameelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizi zipelekwe kusaidia kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu.

Hapo awali sherehe hizi zilikisiwa kugharimu Sh700 milioni na kupunguzwa hadi kufikia Sh450 milioni.

Fedha hizo sasa zitatumika kujenga madarasa, vyoo, kukarabati nyumba za walimu na kununua madawati.

Huu ni uamuzi unaofaa kupongezwa na umekuja baada ya kutolewa mara nyingi ushauri wa kupunguza matumizi ya fedha nyingi kwa sherehe za kila mwaka.

Baadhi ya watu wamekuwa wakipendekeza kuwa sherehe hizi zifanyike kitaifa baada ya kila miaka mitano badala ya kila mwaka.

Katika sherehe hizi huwepo matayarisho ya mwezi mmoja ya vikosi mbalimbali kwa ajili ya gwaride la siku ya kilele cha sherehe hizi, Januari 12.

Hii bila shaka hugharimu fedha nyingi, hasa matumizi ya mafuta ya kuwekwa kwenye magari yanayowapeleka askari uwanjani na kuwarudisha walikotokea.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba sherehe hizo hutumia kati ya saa nne hadi sita ambapo vikundi vya ngoma na sanaa vinasafirishwa kati ya Unguja na Pemba kwa kutegemea sherehe hizo zinafanyka wapi.

Vikundi hivi hununuliwa sare na kupatiwa huduma muhimu za malazi na chakula kwa siku chache wanapokuwa katika shamrashamra za sherehe.

Karibu kila mwaka wageni wengi hualikwa kutoka Tanzania Bara na pia huja viongozi wakuu au wawakilishi wa nchi mbalimbali.

Gharama za kuwahudumia na kuwapatia ulinzi hawa viongozi ni kubwa na huzidi wanapokuwa ni wengi.

Hatua ya kufanya sherehe za wastani na fedha zilizopangiwa kutumika kwenda katika sekta ya elimu ni ya busara, ukizingatia hali ya kiuchumi iliyotokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, ukame na vita vya Ukraine na Russia vilivyosababisha mfumuko mkubwa wa bei za vyakula na mafuta.

Sherehe za kitaifa zilikuwa zitumie Sh450 milioni, lakini ukichunguza unaweza kukuta ni zaidi ya hapo. Hii ni kwa sababu maandalizi rasmi ya sekta mbalimbali za Serikali na binafsi nayo yanayo gharama zake.

Matumizi huwa makubwa kwa sababu ya ukweli kila sekta hutaka ionekane imeshiriki vizuri katika hizo sherehe.

Kwenye wengi pana mengi na yenye mitazamo tofauti ya utashi wa kisiasa, kupenda mambo ya fahari au kuweka mbele masilahi binafsi badala ya yale yaliyokusudiwa na kufanyika hayo mapinduzi.

Ni ukweli usio na shaka kwamba wapo walionuna na kutofurahishwa na uamuzi huo wa Rais Mwinyi kwa sababu tayari walishatayarisha mipango ya kunufaika na fedha za sherehe za mapinduzi kwa njia moja au nyingine.

Si ajabu wapo waliokwisha amua wafanye nini ili wanufaike na fedha hizi, lakini wamejikuta wanaambiwa wameotea kama inavyofanyika kwa wachezaji mpira anapokuwa yeye na goli na kujitayarisha kutingisha wavu.

Wakati kama huu wa kuelekea kilele cha sherehe za mapinduzi panakuwepo patashika nguo kuchanika ya kugombea zabuni za kushona sare, kuhudumia chakula na usafiri na kutengeneza mapambo.

Hivyo vikao vya kupanga nini kifanyike havihesabiki, navyo vinachota fungu kubwa la fedha, lakini hili halipo mwaka huu na waliojipanga kufaidika wameula na chuya.

Uamuzi huu wa Serikali hautofautiani na hatua ambazo nchi mbalimbali zimechukua kupunguza matumizi ya lazima na kupanga upya mipango yake ili kukabili hali ngumu ya uchumi inayotikisa nchi tajiri na masikini hivi sasa.

Ni vizuri kwa mwenendo huu pia kutumika kwa sherehe nyingine kama hizi zinazofanyika Zanzibar kila mwaka, kama za kutangazwa kwa elimu bila malipo mwaka 1964.

Siku hizi hata ndani ya jamii tunaona mbadiliko ya kuacha kufanya sherehe kubwa na za kifahari. Zama zimebadilika na jamii na Serikali nazo zinapaswa kubadilika na kwenda na wakati.

Tunaambiwa kupanga ni kuchagua, basi tupange kwa kuchagua yepi ni muhimu zaidi kutekelezwa na yepi yasubiri hali itapokuwa nzuri.

Tuweke mbele masilahi ya taifa letu, kama kuimarisha huduma za elimu, afya na miundombinu badala ya kutumia fedha nyingi kufurahia magwaride, ngoma na karamu za vyakula.

Columnist: Mwananchi