Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sasa ndo mtaielewa Simba

MASTAA WAGENI SIMBA Sasa ndo mtaielewa Simba

Thu, 20 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nimetazama usajili wa Simba umejaa wanaume haswa. Umejaa watu wa kazi kwelikweli. Essomba Onana ni mtu na nusu. Hakuwa MVP wa Ligi Kuu Rwanda kwa bahati mbaya. Aubin Kramo ni fundi kwelikweli. Hakuwa MVP wa Ligi Kuu Ivory Coast kwa bahati mbaya. Hawa ni aina ya wachezaji tunaowahitaji kwenye ligi yetu.

Simba imemshusha pia Fabrice Ngoma. Huyu ni kiungo wa boli. Anajua muda gani mpira utembee. Anajua muda gani mpira ukimbie. Uzoefu wa kutosha. Ufundi wa kutosha mguuni.

Hivi ni kweli Simba wako serious wa mbio za ubingwa msimu ujao? Naanza kupata shaka taratibu. Kuna taarifa kuwa timu ipo kwenye maandalizi ya msimu ujao nchini Uturuki, lakini kocha mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho' yupo kwao nchini Brazil.

Naanza kupata shaka kidogo. Inawezekana vipi muda wa maandalizi kocha akaondoka kambini? Kocha akaiacha timu? Itakuwa na faida gani kama kocha hayupo na timu Uturuki? Hivi Simba mko serious kweli? Naanza kupata shaka.

Mara Clatous Chama kagomea kusafiri na timu hadi walipomalizana. Mara mwekezaji amekata tamaa ya kuwekeza tena. Mara jezi za msimu mpya kuzinduliwa Mlima Kilimanjaro. Hakuna kinachoeleweka. Maandalizi ya msimu bila kuwa na wachezaji wote. Bila kuwa na benchi la ufundi lililokamilika. Bila kuwa na eneo moja, wakati mwingine ni kama kujipotezea muda tu.

Simba wanaonekana kufanya usajili mzuri sana, lakini usajili pekee yake haukupi ubingwa. Unahitaji mambo mengine yote yawe sawa. Kitendo cha kuanza kwenda kambini nusunusu ni dalili nyingine mbaya.

Kuanza mvutano na mchezaji muhimu na tegemezi kama Chama ni dalili mojawapo ya kutojipanga. Kama kuna jambo la kuboresheana maslahi kwa mchezaji kama Chama lilipaswa kufanywa mapema sana wakati tu msimu uliopita umemalizika. Kuna mahala Simba wanataka wenyewe kuanza kujichanganya. Kumbuka wana deni kubwa sana kwa mashabiki wa Simba.

Kukosa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo sio jambo mashabiki wa Simba wanalolifurahia. Kila msimu kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sio jambo ambalo mashabiki wa Mnyama wanalolifurahia tena.

Simba wanahitaji kwenda mbele. Simba wanahitaji kujipanga sawasawa. Kusikia timu ipo Uturuki, kocha yupo Brazil, Chama kachelewa sana kujiunga na timu, mwekezaji anaanza kususa sio habari njema sana kwa wana Simba. Sio aina ya stori ambazo wanataka kuzisikia kwa sasa.

Nadhani huu ni msimu ambao Simba wanapaswa kuwa na umoja kuliko wakati mwingine wowote. Ni muda wa kwenda kurejesha heshima iliyoanza kupotea ndani ya misimu miwili ya hivi karibuni.

Simba msimu uliopita ilikuwa na makipa watatu Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim. Aishi anaumwa, Beno ameondoka. Nilidhani Simba walitakiwa kusajili makipa wengine wawili haraka sana.

Kitendo cha timu kusafiri kwenda Uturuki bila makipa wa kutosha ni wasiwasi mwingine. Hakuna eneo ambalo halitakiwi kuchezewa kama idara ya kipa. Kwenye mpira hatima ya mechi iko hapa. Simba wamesajili vizuri, lakini kuna maeneo yananipa wasiwasi.

Hivi Simba wako serious kweli na ubingwa wa msimu ujao? Naomba maoni yako kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ni kweli wamesajili vizuri, lakini kuna kitu naona hakijakaa sawa. Timu inatajwa kuwa Uturuki kambini, Kocha anatajwa kuwa kwao Brazil kuhudhuria kozi. Serious? Yaani timu inakwenda kwenye maandalizi bila kocha? Aisee! Wachezaji wamekwenda Uturuki kwa mafungu, wengine tunaonana nao tu kwenye klabu za usiku hapa Dar. Kuna kitu kinanipa wasiwasi pale Msimbazi.

Kutakuwa na ushindani mkubwa sana kuelekea msimu ujao. Singida Fountain Gate, Azam FC na Yanga wamefanya usajili pia wa uhakika. Kama Mnyama anataka ubingwa ni lazima ajiweke pia kibingwa. Kama Simba anataka kweli ubingwa ni lazima kila kitu kiwekwe sawa.

Kocha mkuu ni lazima awe na timu kwenye maandalizi. Wachezaji wote ni lazima wawepo kambini kwenye maandalizi. Viongozi ni lazima watimize majukumu yao kwenye uongozi. Simba wanajua namna ya kushinda ubingwa. Huwezi kushinda kombe mkiwa nusu nusu. Makipa wawili ni lazima wasajiliwe mapema ili waungane na wenzao.

Kama Robertinho ataleta mzaha, mechi za Ngao ya Jamii zitaanza kumtoa Jasho. Hiki kikosi cha Simba kuelekea msimu ujao ni lawama tupu. Mara nyingi huwa kinaondoka na kocha kama kukiwa na dalili za kushindwa kutimiza malengo.

Kwa namna yoyote ile, Simba wanataka ubingwa msimu huu. Kwa namna yotote ile, Yanga wanataka kuvuka hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haya mambo mawili hayatimii kirahisi rahisi. Hatua hizi kubwa haziji kwa bahati mbaya. Kila kitu ni lazima kiwe sawa ndani ya klabu. Ni kweli Simba wamesajili vizuri? Jibu langu ni ndiyo. Ni kweli Simba wako serious na ubingwa? Jibu langu ni Hapana.

Columnist: Mwanaspoti