Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Samatta na Trossard walivyolazimika kwenda njia tofauti

Samatta Pic Mbwana Samatta

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nilienda Ubelgiji miaka michache iliyopita kushuhudia ufalme wa Mbwana Samatta wakati huo akicheza Genk. Kabla ya kuondoka kwenda Birmingham kucheza Aston Villa halafu akaenda zake Uturuki kucheza Fenerbahce, halafu sasa amerudi tena Genk.

Samatta Genk ni nyumbani lakini nilipotembelea Genk miaka michache iliyopita mchezaji anayeitwa Leandro Traossard ndiye ambaye alikuwa nyumbani zaidi kuliko Samatta. Wakati Samatta alikuwa staa zaidi kuliko Trossard lakini Trossard alikuwa nyumbani zaidi kwa sababu amezaliwa eneo linaloitwa Maasmechelen dakika 16 kutoka Genk.

Wimbo wa Samagoal ulikuwa unaimbwa zaidi na mashabiki kukiri ukubwa wa Samatta na tabia yake ya kucheka na nyavu lakini kipaji cha Trossard kilikuwa wazi. Ilikuwa inaonekana atafika mbali. Miaka michache baadaye mastaa hawa wamechukua njia tofauti.

Kuna uzungu na uswahili wetu umesababisha njia ziwe tofauti. Leo Trossard amekuwa staa mkubwa katika Ligi Kuu ya England. Anatamba na Brighton and Hove na haina muda mrefu anaweza kwenda Liverpool, Manchester City, Chelsea, Arsenal au Manchester United.

Alipiga hat trick katika pambano dhidi ya Chelsea lakini imekuwa tabia yake kuzifunga timu kubwa. Wakati huu anakaribia kwenda timu kubwa inafikirisha kidogo. Kwanini Samatta amerudi Genk na yeye anasonga mbele?

Wamepita katika njia tofauti kukutana Genk. Samatta alipoteza miaka takribani sita ya kucheza Afrika katika michuano ya Ligi ya Mabingwa. Alicheza Simba vema mwaka mmoja halafu akawa na miaka mitano ya kucheza TP Mazembe.

Wakati haya yakitokea huku akipoteza muda Afrika, Trossard alikuwa akiingia katika mifumo ya kwao akiwa kinda mbichi. Wakati Samatta akiwa ameiva na kujiunga Genk, Trossard alikuwa bado hajakomaa vema. Kumbe Samatta alikuwa akicheza katika kiwango bora cha maisha yake. hatujui umri halisi wa Samatta lakini tunafahamu umri halisi wa Trossard.

Napata hisia kwamba kama Samatta angetoka Simba na moja kwa moja kwenda Ulaya si ajabu angefika mbali kama huku ambako Trossard anaelekea kwa sasa. Si ajabu alikwenda Aston Villa katika wakati ambao nguvu zilikuwa zinaanza kupungua.

Lakini si ajabu hakujengwa katika mifumo ya soka la Ulaya tangu akiwa mtoto mdogo. Ni tofauti na Trossard ambaye alikuwa anaingia katika mifumo wakati Samatta akisumbuka na mpira wa Afrika. Ni lazima itokee tofauti ya umri au matumizi ya nguvu wakati fulani wa maisha yenu ya soka.

Mchezaji mwingine ambaye anaonekana kunufaika na hili ni Leon Bailley. Yupo Aston Villa na juzi alifunga bao la kwanza dhidi ya Manchester United pale Villa Park. Huyu naye alikuwa rafiki mkubwa wa Samatta pale Genk.

Nilipofika Genk kwa mara ya kwanza alikuwa na umri wa miaka 18 tu. Baada ya hapo alikwenda zake Bayer Leverkusen na sasa yupo Aston Villa akiwa na umri wa miaka 25 tu. Akiizoea Ligi Kuu ya England unaweza kusikia anakwenda Chelsea au juu zaidi.

Nadhani baada ya kucheza Aston Villa, Samatta alitakiwa kwenda juu hatua moja kucheza katika klabu kubwa zaidi lakini hilo halikuwezekana. Achilia mbali sababu za hapa na pale lakini labda hatua hii aliipoteza alipokaa zaidi katika mpira wa Afrika huku akitamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Inawezekana alifika Aston Villa wakati nguvu zikianza kumalizika. Mchezaji ambaye kama atakaza anaweza kwenda mbali zaidi ni Kelvin John kwa sababu ameingia katika mfumo wa mpira wa Ulaya akiwa na umri mdogo zaidi. Amekwenda akiwa na umri wa miaka 18 tu. Tazama ambavyo kabla ya kwenda katika timu za wakubwa ameshacheza mechi kibao za kimataifa za michuano ya vijana hasa ile ya Uefa. Kutoka hapo yeye na kundi la wenzake ni rahisi kupandishwa katika kikosi cha wakubwa cha Genk au klabu nyingine za Ligi Kuu Ubelgiji na kwingineko.

Mwisho wa siku Samatta ataendelea kuwa shujaa wetu hata kama ameshindwa kufanya hivi vitu ambavyo kina Trossard wanavifanya katika Ligi Kuu ya England. Wao waliandaliwa mapema zaidi kuliko yeye ambaye alisota Mbagala kisha akaenda kusota Lubumbashi.

Samatta aliingia Ulaya wakati huo akiwa na miaka 23. Kuanza kutamba Ulaya wakati umefika ukiwa na umri wa miaka 23 sio jambo rahisi sana. Kuna wachezaji wanaotoka katika nchi tajiri wanaweza kuingia katika mifumo kirahisi zaidi kwa sababu maandalizi yao na Ulaya huwa hayatofautiani sana.

Kwa mfano ni rahisi tu kwa mchezaji kutoka Japan, Korea Kusini au Brazil akaenda Ulaya akiwa na umri wa miaka 23 halafu akatamba. Ni rahisi kwa mchezaji kutoka Morocco, Misri, Tunisia akatamba. Lakini kutoka katika nchi zetu hizi za chini ukiwa na miaka hiyo ni ngumu kidogo.

Miaka 23 ya Pasipoti inakupeleka Ulaya ukiwa hoi. Wakati huo unamkuta Trossard akiwa na miaka 20 ambayo ameshapikwa na kucheza mechi nyingi za vijana za michuano kama ya Uefa. Ni rahisi kwake kwenda mbali zaidi kuliko wewe.

Ujumbe wangu ni kuangalia namna ya kuwapeleka vijana wetu nje wakiwa wadogo zaidi. unaposikiliza simulizi la watu kumtaka Fei Toto aende Ulaya muda huu unagundua kwamba ni kichekesho kama vichekesho vingine.

Huyu Samatta katika umri wa miaka 23 hakuingia kikosi cha kwanza cha Genk. Alicheza katika timu ya akiba na vijana kwa ajili ya kumkaribisha azoee soka la Ulaya. Hili ni jambo la kawaida.

Tushukuru alijitunza na kujituma kiasi cha kutuachia kumbukumbu nzuri ambazo zinatufanya tutembee vifua mbele mpaka leo. Amefunga mabao mengi Ligi Kuu ya Ubelgiji lakini pia mabao yake dhidi ya Liverpool katika Ligi ya Mabingwa na bao lake dhidi ya Man City katika pambano la fainali Kombe la Ligi vinatufanya tuwe na vitu vya kuzungumza mbele ya mashabiki wa nchi nyingine.

Columnist: Mwanaspoti