Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Safari njema Christian Atsu, malaika wa wengi nyumbani

Christian Atsu 1140x640 Safari njema Christian Atsu, malaika wa wengi nyumbani

Sun, 26 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati nilipoliona jeneza la Christian Atsu likishushwa kutoka katika ndege ya Turkish Airlines Jumapili usiku kutokea Uturuki nilikumbuka mambo mengi. Nilisikia uchungu. Nikamkumbuka rafiki yangu, John Terry, mlinzi wa zamani wa Chelsea.

Wakati fulani niliwahi kusoma mahala Terry alikuwa akiwauliza rafiki zake Waafrika aliokuwa anacheza nao Stamford Bridge, Jon Obi Mikel, Solomon Kalou na Michael Essien kwanini walikuwa wanatuma pesa nyumbani Afrika mara kwa mara?

Kwa Wazungu huwa hawana utaratibu huu. John Terry mwenyewe alikuwa anapokea kiasi cha Pauni 200,000 kwa wiki pale Darajani lakini baba yake aliwahi kukutwa akiuza kete za cocaine katika choo cha baa pale London. Baba yake wala hakuonekana kujali kipato cha John Terry.

Huu ni utamaduni wa Wazungu. Wale wachezaji waswahili walimwambia wazi Terry kwamba nyuma ya mafanikio na vipato vyao huwa wanahudumia familia zao Afrika. Familia ambazo zinabeba mamia ya watu.

Kuna watoto wa wajomba, watoto wa shangazi, wadogo zao, babu zao wote wanaishi katika mshahara wako unaolipwa Chelsea. Ndivyo zinavyoishi familia zetu. Mtu mmoja anachomoka na kufanikiwa kimaisha na baada ya hapo nyuma yake anabeba watu 120 wanaomtegemea.

Nilipoliona jeneza la Atsu niliamini amekufa. Wakati akiwa chini ya kifusi pale Uturuki huku akijaribu kutafuta upenyo wa kuchomoka na kuendelea kujiweka hai, ilikuwa inamaanisha pia kwamba Atsu alikuwa anapigania uhai wa watu wengine.

Kupigania uhai wa wengine kwa vijana kama Atsu kunaanzia nyumbani kwao Afrika Magharibi. Vijana wengi wenye vipaji kama Atsu huwa wanatoka katika familia ambazo zimetokea katika umaskini uliotopea. Vipaji vyao ndio njia pekee ya kuwafikisha mbali.

Kwa mfano huyu Atsu, alizaliwa katika kitongoji cha Ada Foah kilichopo Accra, Ghana. Alikulia katika umaskini uliotopea huku yeye akiwa mmoja kati ya watoto 10 katika familia. Baba yake alikuwa mvuvi tu kando ya Ziwa Volta.

Mpira ndio ambao ulimtoa katika umaskini huo na kwenda Ureno kuanza maisha ya soka. Kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa Kiafrika, huko Ulaya ndipo wanapotimiza ndoto nyingi. Kitu cha kwanza ni kupata pesa, lakini kingine kinaweza kuwa kuoa mwanamke wa kizungum E za. Ureno ndiko alikompatia mkewe, Marie-Claire Rupio.

Anapofariki dunia mchezaji kama Atsu katika maisha yetu ya Kiafrika ni zaidi ya msiba. Kuna wanasoka wa Kiafrika ambao hawatuachii misiba miwili kwa sababu maisha yao yanakuwa ya kuponda starehe Ulaya. Likizo zao wanakwenda Miami au Ibiza.

Lakini kuna wanasoka ambao sehemu ya pesa zao wanatoa misaada kwa familia, lakini pia kwa familia nyingine ambazo haziwahusu. Mfano kni huyu Atsu. Msiba wake umekuwa mzito zaidi kwa sababu ukisoma sehemu fulani unagundua kwamba alikuwa na msaada mkubwa kwa jamii yake.

Msiba wake umeacha msiba mwingine mzito kwa kituo cha watoto yatima pale Ghana kinaitwa AATC. Yeye ndiye alikuwa mfadhili wao mkubwa. Kwa sasa hawajui hatima yao. Atsu alikuwa anawatunza lakini pia amewahi kuwanunulia basi la shule.

Mchezaji kama Sadio Mane amekwenda mbali zaidi. Sio tu kwamba yeye ni msaada mkubwa kwa familia yake, lakini pia ni msaada mkubwa katika mji wake wa Sedhiou pale Senegal. Yeye ndiye ambaye anajenga shule, hospitali pamoja na misaada mingine mikubwa katika jamii.

Didier Drogba kupitia mfuko wake wa jamii wa Didier Droba Foundation amejenga hospitali kubwa nchini Ivory Coast. Mifano kama hii ipo mingi kwa wanasoka au hata wanamichezo mbalimbali kutoka katika Bara la Afrika. Watu hawa ni baraka kwetu.

Anapopotea mchezaji kama Atsu ambaye amechuma mishahara katika nchi mbalimbali za Ulaya na sasa hivi alikuwa anachuma nchini Uturuki, mioyo ya watu wake wa nyumbani huwa inaumia mara mbili ya msiba wa kawaida. Tayari kipato cha jamii kinakuwa kimepotea na kuna malaika wanaanza kuhangaika.

Kina John Terry huwa hawaelewi hivi. Kwanza wamekulia katika nchi tajiri ambazo raia wake wanajitegemea na kujisaidia kwa kila jambo. Zaidi ya yote ni kwamba kuna tamaduni za kila mtu kujitegemea katika kipato. Sisi hatuna tamaduni hizo. Tuna tamaduni za kutegemeana katika sera za ujamaa.

Sio kwamba hawa kina Atsu hawafaidi maisha yao binafasi. Hapana, Wanafaidi sana. Wanaendesha magari mazuri. Wananunua nyumba nzuri za kifahari barani Ulaya na kwingineko, lakini bado wana akiba kubwa ya kusaidia jamii nyingine.

Usiutazame msiba wa Atsu kama msiba wa kawaida wa kifo cha kijana aliyekuwa na uwezo mkubwa uwanjani. Hapana. Kuna kitu zaidi ya hiki ambacho kinaumiza zaidi. Kuna watu wengi ambao pia wanaweza kupoteza ajira nchini kwake.

Hawa wachezaji wa Kiafrika pia huwa wanarudi nyumbani na kuanzisha miradi mingi huku wakiajiri watu mbalimbali. Staa wa Nigeria, Ahmed Mussa ni miongoni mwa matajiri waliowekeza katika vituo vya mafuta nchini Nigeria. Anapotoweka mchezaji kama yeye katika uso wa dunia basi huku nyuma mambo yanayumba na si ajabu kufutika.

Kuna wanasoka wengi wa Kiafrika waliofariki dunia wakiwa Ulaya. Wengine kama kina Marc-Vivien Foe na Cheickh Tiote walifia viwanjani kabisa. Binafsi kifo cha Atsu nimekiangalia kwa sura tofauti baada ya kugundua kwamba mastaa hawa kama ilivyo kwa mastaa wa Amerika Kusini huwa wanabeba maisha ya wengi nyumbani.

Katika ubinadamu wa kawaida kifo cha Atsu kinaumiza, lakini ukikiangalia katika sura hii kinaumiza zaidi. Nenda katika mitandao kisha angalia sura za watoto wadogo yatima ambao Atsu alikuwa anawatunza ndipo utakapogundua kwamba kifo chake kimeacha simanzi kubwa zaidi kwa wengi.

Columnist: Mwanaspoti