Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sabilo namba zake zinaongea mguuni

Sixtus Sabilo.jpeg Sixtus Sabilo

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatajwi sana midomoni mwa mashabiki wa soka nchini, lakini kazi yake inambeba uwanjani na kumpa heshima kubwa kwa wanaomfuatilia.

Achana mabao yake aliyofunga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021-2022 yaliyoipeleka Namungo katika makundi, chungulia orodha ya wafungaji mabao na asisti wa msimu huu utaujua ukali wa Sixtus Robert Sabilo.

Yupo nyuma ya kinara wa mabao Reliants Lusajo aliyewahi kucheza naye Namungo, akizidiwa bao moja tu. Lusajo ana sita, wakati Sabilo ana matano huku akiwa kinara wa asisti kwa kutoa pasi nne zilizozaa mabao akiwafunika hadi kina Clatous Chama, Feisal Salum na Stephane Aziz Ki.

Mwanaspoti linakuletea ubora wa mshambuliaji huyo ambaye anakipiga katika kikosi cha Mbeya City kwa sasa na kufunguka malengo yake msimu huu.

MISIMU WA SABA

Ni misimu wake wa kucheza mashindano ya ushindani akianza na Stand United ambayo ameitumikia kwa miaka miwili na nusu na baadaye KMC ambayo aliitumikia kwa mwaka mmoja na kuitumikia nusu msimu na kutimkia Polisi Tanzania akiitumikia msimu mmoja.

Baada ya hapo alitua Namungo FC na kuitumikia kwa miaka miwili akahamia Mbeya City timu ambayo amekuwa tegemeo kutokana na mchango wake akihusika katika mabao tisa.

MABAO 25

Mkali huyo wa kutupia na pasi za mwisho kwenye timu tano alizocheza amefunga mabao 25 hadi sasa huku akihusika kuzifunga timu 18 alizokutana nazo akizitumikia timu tano ambazo ni Stand United, KMC, Polisi Tanzania, Namungo na sasa Mbeya City

TIMU ALIZOZIFUNGA

Sabilo amezifunga timu 18 hadi sasa hukuvikiwemo vigogo vya Simba, Yanga na Azam FC. Timu zote hizo zimeonja machungu kutoka kwake na nyingine ni Ruvu Shooting, Mwadui FC, Singida Big Stars, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania, Namungo, Ihefu FC na Lipuli zote hizo amezifunga bao moja moja.

Wakati Singida United, Ndanda FC, Njombe Mji ambazo zimeshuka daraja, Dodona Jiji amezifunga mabao mawili mawili na Kagera Sugar ameifunga mabao manne.

MKALI WA ASISTI

Mbali na kutupia, nyavuni ambapo hadi sasa anashika nafasi ya pili, Sabilo pia ndiye anayeongoza kwa kutoa pasi za mwisho ‘asisti’.

Msimu huu akiwa anaitumikia Mbeya City, Sabilo amefunga mabao matatu kwenye uwanja wa nyumbani kwa kuzifunga Ihefu FC, Polisi Tanzania na Namungo huku ugenini akifunga mabao mawili amezifunga Dodoma Jiji na Singida Big Stars.

KMC HAKUWA NA MAAJABU

Sabilo anasema alitua KMC akitokea Stand United hakuwa na mwanzo mzuri kutokana na kupata majeraha na kujikuta akikaa nje kwa muda mrefu tofauti na matarajio yake.

“Nilisajiliwa mwaka mmoja lakini nimeitumikia timu hiyo miezi sita nikicheza mechi saba moja tu ndio nilianza kikosi cha kwanza sita nilikuwa naanzia benchi kutokana na kutokuwa fiti, kwenye michezo niliyocheza sikupata nafasi ya kufunga bao hata moja zaidi ya kutoa pasi mbili tu za mabao na kutolewa kwa mkopo kwenda Polisi Tanzani,” anasema.

MBABE KAGERA SUGAR

Mshambuliaji huyo ambaye amecheza timu tano zilizokuwa zinashiriki Ligi Kuu Bara amefanikiwa kuzifunga timu 18 lakini ameonekana kuwa mwiba mkali zaidi akikutana na Kagera Sugar kutokana na kuifunga mabao mengi zaidi tofauti na nyingine. Ameifunga mabao manne.

DAKIKA 770 BILA KADI

Hadi sasa, Sabilo amecheza mechi tisa za Ligi Kuu akitumikia dakika 770 na kuifungia timu yake mabao matano na asisti nne.

Mara nyingi imekuwa vigumu wachezaji kucheza bila ya kupata onyo la kadi ya njano au nyekundu katika Ligi Kuu lakini Sabilo ameonyesha ni mchezaji mwenye nidhamu na ukomavu baada ya kucheza dakika hizo bila ya kuonyeshwa kadi ya njano wala nyekundu.

MSIKIE MWENYEWE

Mchezaji huyo anasema muunganiko wa haraka walioupata kikosini umempa nafasi ya kufanya vizuri huku akimtaja Tariq Seif kuwa na nyota wengine wamekuwa wakimrahisishia kazi huku akibainisha ishu ya mfungaji bora ni mapema kuiweka akilini.

Anasema kwa sasa mkakati wake ni kuona anaipambania timu kutokana na kumwamini na kumpa namba kwenye kikosi cha kwanza na kwa mwenendo walioanza nao anaiona Mbeya City ikizitesa timu nyingi.

“Kazi yangu ni kufunga na kutengeneza nafasi kwa wenzangu wakiwa kwenye maeneo mazuri. “Kikubwa ni kuhakikisha tunasonga mbele na kufikia malengo yetu, ishu ya kufunga mabao mangapi sio muhimu sana nitafunga na kutoa pasi kila nitakapopata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema.

Columnist: Mwanaspoti