Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sababu tano muhimu kusajili nembo biashara

BRELA TZ Sababu tano muhimu kusajili nembo biashara

Sun, 21 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ALAMA ya biashara au huduma ambayo kwa wengi hujulikana kama nembo au ‘logo’ ni alama ya kipekee ambayo inatambulisha aina fulani ya bidhaa au huduma inayotolewa au kuzalishwa na mtu, kikundi au kampuni fulani.

Katika historia, usajili wa alama hizi ulianza kufanyika chini ya sheria katika karne ya 19 ingawa ni bayana kwamba hata kabla ya hapo alama hizi zilikua zikitumika.

Moja ya sababu kubwa iliyosababisha kuanza kusajili alama za biashara au huduma ni ukuaji wa teknolojia hasa kuongezeka kwa masafa ya vyombo vya habari na kuwafikia watu wengi zaidi.

Katika historia alama za mwanzo kabisa kusajiliwa ni pamoja na ‘Deviled Entremets’ ambayo ilisajiliwa Mwaka 1870 na Kampuni ya William Underwood huko Boston, Marekani.

Mwaka 1875, Mfanyabiashara William Bass aliingia katika historia ya kusajili Alama ya Biashara ya kwanza nchini Uingereza iliyojulikana kama ‘Red Bass triangle’.

Alama hii ilikua na mwonekano wa pembe tatu nyekundu (kitako kikiwa chini na ncha kali ikiangalia juu) na maneno yaliyosomeka Bass.

Nchini China alama ya kwanza kusajiliwa ilijulikana kama ‘Nestle Eagle Brand’ ambayo ilisajiliwa mwaka 1874. Hizo ni baadhi ya alama za kwanza kusajiliwa katika nchi mbalimbali.

Kwa Tanzania alama ya biashara ya kwanza kusajili ilijulikana kama ‘His maters Voice’ iliyosajiliwa Septemba 11, 1922.

Kila jambo linalofanyika kuna sababu kadhaa nyuma yake, vivyo hivyo kwa usajili wa alama hizi. Makala hii itaangazia sababu tano kuu za kwanini ni muhimu kusajili alama za biashara au huduma “nembo”.

UTAMBUZI WA BIDHAA/HUDUMA

Sifa kuu ya alama ya biashara au huduma ni kutofautisha bidhaa moja kati ya nyingine zinazofanania, mfano bidhaa ya maji ya chupa ya kunywa zote ni bidhaa ila zinatofautishwa na alama ya bidhaa nembo.

Kwa bidhaa za aina moja ziingiapo sokoni ni vigumu sana kutambua utofauti wake, hivyo kumfanya mnunuzi kushindwa kuwa na uhakika na bidhaa atakayonunua.

Hii inaweza kumfanya mteja kushindwa kuitambua pia bidhaa aliyotumia awali atakapohitaji kutumia tena, hivyo kuanza kubahatisha.

Kwa kutumia alama ya biashara mteja anaweza kuitambua bidhaa aliyotumia mara ya kwanza kwa kuangalia alama ya bidhaa iliyopo na kuinunua tena kwa mara nyingine tena.

KUTANGAZA BIDHAA/HUDUMA

Alama za biashara au huduma zina mchango mkubwa katika kuitangaza biashara au huduma fulani, hasa katika matangazo ya michoro na maandishi, lakini kwa matangazo mengine ambayo huwa sio ya moja kwa moja.

Matangazo haya mara nyingi hujitokeza katika filamu, mabango, vipeperushi, au nyimbo, mara kadhaa unaweza kuwa umeshuhudia nembo fulani inajitokeza katika nyimbo au filamu mathalani katika kinywaji au duka, hii ni aina fulani ya kutangaza biashara.

Hivyo kuwa na nembo ambayo imesajiliwa inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa sana katika kuifanya bidhaa au huduma iweze kufahamika kwa umma.

KUFIKA SEHEMU YA BIASHARA/HUDUMA

Siku zote katika maeneo ya biashara, msongamano wa biashara za aina moja, kwa hali hii wakati mwingine inakua vigumu kwa wateja kutambua sehemu ya biashara ambayo wanakwenda.

Katika mazingira haya pale nembo inapotumika humsaidia mteja kuweza kutambua sehemu ya biashara anayokwenda na kufika kwa urahisi. Hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kuongeza idadi ya wateja wanaofika katika eneo lako.

KUIPA HADHI BIASHARA/HUDUMA

Katika kutoa huduma au kuuza bidhaa, wateja hugawanywa katika makundi mbalimbali kulingana na mpango wa mauzo wa mtu au kampuni husika.

Mara nyingi kuna baadhi ya wateja kabla ya kununua bidhaa au kupata huduma wanaangalia hadhi ya bidhaa au huduma na mara nyingi kuna baadhi ya watu hawawezi kabisa kununua au kutumia bidhaa za aina fulani kwa sababu ya hadhi yake.

Katika hali hii nembo ina mchango mkubwa sana katika kuipa hadhi na mwonekano wa kipekee bidhaa au huduma inayotolewa, na pia kumwezesha mteja kufanya maamuzi sahihi kulingana na ubora wa bidhaa au huduma fulani inayotambulishwa na nembo.

KINGA YA KISHERIA DHIDI YA BIASHARA YAKO

Ni muhimu kuilinda kisheria biashara yako dhidi ya washindani au waharibifu wa biashara za wengine. Mara kadhaa imejitokeza kwamba mtu au kikundi cha watu wanazalisha bidhaa zenye ubora wa chini kwa kutumia nembo ya bidhaa nyingine au kutoa huduma hafifu kwa nembo ya sifa na hadhi sehemu fulani.

Pindi bidhaa hizi ziingiapo sokoni, huharibu sifa nzuri ya bidhaa iliyokuwapo awali. Lakini kama nembo yako ya bidhaa au huduma imelindwa basi inakua ni vigumu kwa wao kutumia nembo hiyo.

Kwa upande mwingine, kuendesha biashara kwa kutumia nembo ambayo haijasajiliwa, mshindani anaweza kuisajili nembo hiyo na kuwa yake bila pingamizi kwa sababu nembo hiyo kisheria haina mmiliki.

Endapo mtu atatumia nembo iliyosajiliwa kisheria basi mmiliki anaweza kumchukulia hatua za kisheria kwa kwenda mahakamani kudai fidia ya matumizi yasiyo halali ya nembo yake na hasara aliyopata kwa udanganyifu huo.

JE, UNAWEZAJE KUSAJILI ALAMA YAKO YA BIASHARA AU HUDUMA?

Kwa Tanzania alama ya biashara au huduma (nembo) zinasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Huduma (BRELA) chini ya Sheria ya Alama za Biashara na Huduma Sura ya 326. Taratibu zote za Usajili zinafanyika kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya www.brela.go.tz hivyo haina haja ya kufika katika ofisi za BRELA kwa ajili ya usajili.

Ili kukamilisha usajili, mwombaji atatakiwa kuwa na namba ya kitambulisho cha utaifa kutoka NIDA ambayo itakayomwezesha kufungua akaunti katika mfumo wa usajili na kisha kuandaa ombi la usajili na kuliwasilisha BRELA kwa njia ya mtandao.

Jumla ya gharama kwa ajili ya usajili ni Sh. 130,000 ambayo inalipwa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza mwombaji atalipa Sh. 65,000 ambayo ni ada ya ombi pamoja na kutangaza nembo kwa umma ili kujiridhisha kama nembo hiyo haina mmiliki mwingine.

Awamu ya pili mwombaji atalipia Sh. 65,000 ambayo ni ada kwa ajili ya cheti cha usajili baada ya ombi la usajili kukamilika. Muda wa usajili wa nembo ni miezi mitatu ambapo mwombaji atapata cheti cha usajili na kuimiliki nembo yake kisheria.

Katika hiyo miezi mitatu ya usajili kuna takwa la kisheria la kutangaza kwa siku sitini alama “nembo” hiyo kwenye jarida la BRELA linalotoka bure kila mwezi, jarida hilo linapatikana kwenye tovuti ya BRELA.

Kisheria alama ya biashara au huduma ukomo wake ni pale mmiliki wa alama “nembo” hiyo atakapoamua kuacha kuitumia kwa kuitaarifu BRELA kupitia kwa Msajili wa Alama za Biashara na Huduma. Sheria ina takwa la kuhuisha nembo hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka saba na baada ya hapo itakuwa kwa kipindi cha kila baada ya miaka kumi.

Alama ya Biashara na Huduma “nembo” ni mali kama zilivyo mali nyingine na zina thamani kubwa sana katika biashara, hivyo ni vema wafanyabiashara wa aina zote wakasajili alama zao za biashara ili kulinda “nembo” hizo zisichukuliwe na maharamia wa biashara.

Columnist: www.tanzaniaweb.live