Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Saa 36 kambini kwa Taifa Stars Ismailia

Stars Ismailia.jpeg Kikosi cha Taifa Stars kikiwa Kambini Misri

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nilisafiri kwenda Cairo, kisha Ismailia kwa ajili ya kuungana na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyocheza pambano lake la kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda. Tulishinda bao 1-0 kupitia kwa Simon Msuva.

Niligundua mambo mengi nikiwa Ismailia. Maisha yanachekesha sana. Kwanza kabisa mchezaji maarufu katika kikosi cha Stars pale Ismailia alikuwa Himid Mao. Kila Mwarabu alikuwa anamuulizia Himid. Kisa? Anacheza kwao.

Lakini zaidi ni kwamba Ismailia wana bahati mbaya na Himid. Anawafunga mara nyingi, ingawa yeye ni mchezaji wa kiungo. Siku moja kabla hajajiunga na kambi ya timu yake ilikuwa inacheza na Ismailia na alifunga bao. Mara kadhaa mashabiki wao walikuwa wanalalamika kwamba hawampendi Himid kwa sababu hiyo.

Katika kambi ya timu ya taifa pia, maisha yamekwenda kasi. Mbwana Samatta, Himid Mao na Simon Msuva sasa hivi ndio wachezaji wakongwe kikosini. Inawezekana sio wachezaji wenye umri mkubwa zaidi, lakini ndio wanaonekana wachezaji waliochezea Stars kwa muda mrefu.

Kweli maisha ya wanasoka ni mafupi. Katika miaka ya karibuni tangu tuhamasike tena na timu yetu ya taifa nimeshuhudia mabadiliko ya vizazi. Wakati ule wa Marcio Maximo tulikuwa na kina Juma Kaseja, Ivo Mapunda, Salum Swedi, Victor Costa, Said Maulid na wengineo wengi ambao sasa wameacha soka.

Halafu wakaja kina Mrisho Ngassa, Haruna Moshi, Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Athuman Idd ‘Chuji’ na wengineo. Leo tuna kina Msuva, Samatta, Bakari Mwamnyeto, Himid Mao, Dickson Job na wengineo. Na bado katika hao ungeweza kuona kina Samatta hawana maisha marefu katika kambi ya Stars. Kwa sasa wamezungwa na vijana wengi wadogo na wenye ari.

Lakini katika kambi ya Stars kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vijana wanaocheza nje ya nchi wakiongozwa na Samatta mwenyewe. Pale Ismailia tulikuwa na wachezaji 10 wanaocheza nje ya nchi na walikuwa na uwezo mkubwa, ingawa baadhi yao hawakupata nafasi.

Samatta na Kelvin John (Genk), Msuva (Al-Qadsiah ya Falme za Kiarabu), Novatus Dismas, Ramadhan Makame (Bodrumspor ya Uturuki), Alphonce Mabula (FK Spartak Subotica ya Serbia), Ben Starkie (Basford ya Uingereza), Ally Msengi (Moroka Swallows), Himid Mao (Ghazi El Mahalla ya Misri).

Ambao hawakucheza ni vijana wadogo ambao bahati nzuri kwao wamejikuta nje ya nchi bila ya kucheza Simba wala Yanga. Hatujui waliondoka vipi, lakini ukweli unaweza kuona wakishindana wakiwa mazoezini. Kinachochekesha ni mwaka 2007 nilikwenda Brazili na kikosi cha Stars chini ya kocha, Marcio Maximo lakini hakukuwa na wachezaji ambao walipitia katika ngazi za timu za taifa za vijana. Tungewezaje kupata mafanikio kutoka kwao?

Katika kikosi kilichokuwa kambini pale Ismailia wachezaji wote wamecheza katika timu za taifa za vijana. Kuanzia ile ya chini ya umri wa Miaka 17 hadi ile ya chini ya Miaka 20. Hata hawa wanaocheza nje ambao sio maarufu sana miongoni mwa mashabiki nchini nao wamecheza timu mbalimbali za vijana.

Kuhusu kocha? Adel Amrouche anaonekana kuwa Marcio Maximo mwingine. Nimeongea naye kwa muda mrefu na msingi wake mkubwa katika mafanikio ni nidhamu kutoka kwa wachezaji. mwenyewe anadai kwamba anaweza mbele zaidi kile anachokiona kwa mchezaji kuliko jina lake.

Kitu ambacho kitamsaidia ni ukweli kwamba wachezaji wake wengi wana nidhamu kwa sababu wamepita katika soka la vijana. Ni mavuno mazuri kwake na kwa taifa kwa ujumla na ndio maana tumekuwa tunasisitiza katika soka la vijana.

Vipi kuhusu kambi yenyewe? Daima Misri litakuwa taifa ambalo litasumbua sana kisoka kuanzia katika ngazi ya klabu hadi timu ya taifa. Kuna sharti la kwamba hoteli yoyote kubwa lazima iwe na Uwanja wa soka. Hoteli ya Tolip ambayo Stars ilifikia kulikuwa na viwanja viwili vikubwa vya soka.

Wachezaji walikuwa wanashuka chini ya hotelini na kuingiza mazoezini. inakuonyesha ni namna gani wenzetu wapo makini katika masuala ya michezo. Zaidi ya hapo ndani ya hoteli kulikuwa na gym ya kisasa mabyo iliwatosha wachezaji wote.

Waganda walikuwa wamefikia katika hoteli ya karibu na Stars iitwayo Mercury na wao walikuwa na uwanja wao wa mazoezi hapo hapo. Ni mara mbili tu Stars walitumia basi lao kwenda katika uwanja wa mechi. Siku moja kabla ya mechi ambapo kwa mujibu wa kanuni walipaswa kufanya mazoezi hapo, lakini katika siku ya mechi. Basi. Kwa Waganda nao ilikuwa hivi hivi tu.

Mitaani Ismailia pia kuna viwanja vizuri vya kisasa ambavyo vijana na watu wazima wanafanya mazoezi. Ni viwanja ambavyo vipo hali nzuri kuliko viwanja vingi vya Ligi Kuu ya Tanzania. Unapoona timu za Misri zinafanya vizuri katika michuano ya kimataifa basi ujue ni jambo ambalo wamewekeza mitaani katika miji yao yote.

Vipi kuhusu mechi? Ilikuwa mechi nzuri ya soka. Waganda walitawala kipindi cha kwanza wakati Stars walicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili. Inavyoonekana ni kwamba Waganda nao wameingia katika kizazi kipya cha soka baada ya kile cha awali kuwasumbua zaidi Stars. Hawa wa sasa hivi tunaweza kuwamudu.

Waliobaki ni wachache na ambao tunawatambua kwa haraka haraka kutoka katika kizazi cha zamani ni Emmanuel Okwi na Khalid Aucho. Sidhani kama kizazi chao kijacho kitakuwa kizuri kuliko kilichopita. Tuliwamudu vizuri hasa katika kipindi cha pili ambacho tulipata bao la ushindi.

Watu wamekuwa na maneno mengi kuhusu Mbwana Samatta hasa pale Msuva anapofunga. Inaonekana kama vile Msuva anakuwa shujaa kuliko Samatta. Ukweli ni kwamba wote wawili ni Watanzania na tunahitaji bao kutoka kwa mchezaji yeyote wa Stars na sio Samatta peke yake. Akifunga Msuva taifa bado linakuwa limeshinda.

Tofauti na klabuni kwake, akiwa na Stars, Samatta anafanya majukumu mengi uwanjani kwa sababu uwezo wa timu sio mkubwa sana. Analazimika kushuka chini na kucheza timu. Ni tofauti na anapokuwa katika timu zake za Ulaya anapolazimika kukaa mbele na kuvizia.

Columnist: Mwanaspoti