Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTIDOKTA: Utimamu wa akili ndo kila kitu

Aucho Moloko Utimamu wa akili ndo kila kitu

Fri, 19 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita tumeshuhudia Yanga ikitangazwa bingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa na mechi mbili mkononi baada ya kufikisha pointi 74 na huko Ulaya, Jumapili iliyopita Barcelona ya Hispania ilitangazwa bingwa wa La liga ikiwa imebakiza mechi nne.

Kule England katika Ligi Kuu timu ya Arsenal iliyoongoza kwa muda mrefu, Jumapili ilipokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Brighton na hivyo kuipa nafasi kubwa Manchester City kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ikihitaji pointi tatu tu.

Kibongobongo itazame Yanga ambayo jana ilikuwa na kibarua kizito nchini Afrika Kusini katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants.

Na kimataifa itazame Manchester City ambayo jana ikiwa nyumbani na kibarua kizito katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. Pia klabu hii ina jukumu la kushinda mechi za ligi zilizobaki ili kutangazwa bingwa wa Ligi Kuu England na wakati huohuo Juni 3 itakutana na Manchester United katika fainali ya Kombe la FA.

Ukitazama kwa jicho la kitabibu Manchester City na Yanga ni mfano wa timu zilizofikia hatua hizo kutokana na mafanikio ya utimamu wa miili ya mchezaji mmoja mmoja. Ni kweli soka lina benchi la ufundi na makocha wazuri wenye mbinu za kutosha, lakini utimamu wa miili wa wachezaji ndio kila kitu katika kufanikiwa.

Utimamu ndio unamwezesha mchezaji kucheza mashindano zaidi ya mawili kwa kiwango pasipo kuchoka na kutopata majeraha kirahisi.

UTIMAMU UKO HIVI

WataalamU wa sayansi ya fiziolojia ya michezo wanaeleza kuwa utimamu wa miili unahusisha utendaji wenye ufanisi usio na shaka wa moyo na mapafu pamoja na misuli na mifupa ya mwili.

Kila kinachofanyika mwilini kina athari pia kwa tunachoweza kufanya na akili zetu. Utimamu unachochea ubora wa akili na uimara wa hisia za mwili. Ndio maana mchezaji mwenye utimamu wa mwili anatakiwa pia kuwa na utimamu wa akili.

Ikitokea utimamu wa mwili ukayumba mtu anaweza pia kuteteresha afya ya akili na kumpa hisia hasi. Kuwa na utimamu ulio thabiti kunaweza kuboresha afya ya ubongo, kusaidia kudhibiti uzito, kupunguza hatari ya kupata magonjwa, kuimarisha afya ya mifupa na misuli na kuongeza uwezo wa kufanya majukumu au kazi za kila siku.

Mchezaji mwenye bidii na kujituma katika mafunzo na mazoezi ya kati mpaka yale makali anapata faida kubwa katika utimamu wa mwili ukilinganisha na mchezaji mvivu.

Hapa tunapata picha kuwa utimamu wa mwili kwa mwanasoka haupatikani tu kirahisi rahisi, bali inahitaji kuwa na nidhamu ya mazoezi ya kujenga afya ya mwili kwa ujumla.

VITU MUHIMU

Kuna mambo kadhaa katika utimamu wa mwili ambayo ni ustahimilivu wa moyo na mzunguko wa damu, uimara na ustahimilivu wa misuli na mifupa, unyumbulikaji na vitu vilivyomo ndani ya mwili.

Vilevile kuna kujimudu katika mhimili wa mwili, uratibu, kukimbia, nguvu, kasi na uamuzi pamoja na kutenda kwa wakati.

Moyo na mishipa ya damu yenye afya ndio inatuwezesha kuwa na utawanyaji wa damu yenye oksijeni na sukari kwa ufanisi katika misuli ambayo ndio inahitajika kwa mwanasoka kutumika kufanya kazi.

Misuli na mifupa ni lazima iwe imara na uwezo wa kufanya kazi kwa kipindi kirefu pasipo kuchoka kirahisi. Utimamu wa viungo hivi ndio pia unamfanya mchezaji kutopata majeraha kirahisi.

Unyumbulikaji yaani flexibility ni uwezo wa viungo wa mwili kufanya mijongeo mbalimbali katika uelekeo chanya kupitia maungio ya mwili ikiwamo ungio la goti, kifundo, nyonga, kiganja, kiwiko na bega.

Mfano uwezo wa mchezaji kupiga chenga kwa ufanisi na kuwatoka wapinzani ni lazima awe na utimamu wa maungio haya. Mchezaji anahitajika kuwa na mazoezi bora ya viungo ilia kunyumbulika.

Ndani ya mwili kuna vitu ambavyo lazima viwepo katika kiwango kinachotakiwa kitabibu ili kutimiza utimilifu wa mwili ikiwamo kiwango sahihi cha mrundikano wa mafuta.

Uwepo wa mrundikano mkubwa wa mafuta maana yake ni kuwa na uzito uliokithiri au unene. Mchezaji mwenye utimamu wa mwili huwa na kiwango cha mrundikano wa mafuta kinachokubalika.

Wachezaji hupimwa afya na kutathiminiwa kiwango cha mafuta ya mwili kwa kukokotoa uwiano wa uzito na urefu kitabibu hujulikana kama Body Mass index-BMI, kupimwa mzunguko wa tumbo na paja.

Uwezo wa kujimudu katika mhimili wa mwili dhidi ya kani ya uvutano. Utimamu wa mfumo wa fahamu na misuli na mifupa ndio unaweza kuutuliza mwili katika mhimili wake bila kuyumbayumba.

Mfano mchezaji mwenye utimamu wa mwili anatakiwa kusimama kwa mguu mmoja kwa sekunde 10 pasipo kuyumba yumba akiwa amefunga au amefumbua macho.

Uwezo wa kuratibu viungo vya mwili na matendo yake, mchezaji timamu anatumia ogani za fahamu kwa ufanisi ikiwamo macho na masikio hatimaye kutafsiri na kufanya vitendo sahihi.

Mfano mchezaji timamu atasikia mwito na kuona hatimaye kupiga au kutoa pasi mahali sahihi. Mfumo wa fahamu ndio unaratibu mambo haya.

Nguvu kwa mwanasoka ndio msingi wa kuweza kufanya matendo mbalimbali ikiwamo kukimbia kwa kasi kupiga mashuti na kukaba kwa nguvu.

Mchezaji mwenye utimamu anakuwa na nguvu za kutosha na hatimaye kuweza kutoa msukumo au shinikizo kubwa katika kukabana, kusukumana, kupiga au kukimbia kasi katika kukaba au kushambulia.

Kukimbia haraka kirahisi, ni uwezo wa mchezaji kuukimbiza mwili wake na huku pia akiwa katika uelekeo sahihi wakati wa kutii msisimko wa mwili wake.

Kuamua na kutenda kwa wakati, mchezaji mwenye utimamu wa mwili hufanya maamuzi kwa wakati na kutenda haraka kwa usahihi

Mfano mchezaji anapoondosha mpira unaokaribia kuingia golini kwao, ni kitendo kinachohitaji uamuzi wa haraka na sahihi pasipo kujifunga.

Kasi ni moja ya matokeo makubwa ya mwanasoka mwenye utimamu, ni hali ya kuweza kukimbia umbali fulani kwa muda mfupi. Mabeki wa pembeni na mawinga ndio mfano hali wa kasi.

CHUKUA HII

Utimamu wa mwili unaweza kuharibiwa na mambo mbalimbali kama vile ulaji holela wa vyakula, kutokulala na kupumzika, uvivu wa mazoezi au kutoushughulisha mwili, ulevi na majeruhi au kuumwa.

Vilevile matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya, umri mkubwa, mazoezi na mafunzo duni, kuishi mazingira duni na mtetereko wa afya ya akili inayoweza kuchangiwa na migoro ya familia, kazi na kimaisha.

Utimamu wa mwili ndio kila kitu katika mafaniko soka na yanayokana na nidhamu ya mchezaji na benchi bora la ufundi.

Columnist: Mwanaspoti