Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTIDOKTA: Kasi ya Vinicius Jr ni balaa

Vini Jr Real Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr

Fri, 12 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mchezo wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya UEFA kati ya Real Madrid na Manchester City uliochezwa usiku wa jumanne katika dimba la Madrid Santiago Bernabeu kasi ya winga wa kushoto wa Madrid Vinicius Junior ilikuwa ni balaa kwa Mabeki wa timu pinzani

Mchezaji huyu ambaye ndio alifunga goli la kwanza katka dakika ya 34 alionyesha kasi ya juu hasa katika upande wa kushoto akikwaaana na beki Kayle Walker ambayo muda wote alikuwa hatulii kumchunga winga huyo.

Kama vile haitoshi Vini Jr alionyesha uwezo wa kukaba kwa kasi pale anapopoteza mpira au pale beki wa kulia wa Man City K.Walker alipokuwa anapanda kushambulia.

Kila aliyeutazama mchezo huo hakuna aliyesita kumsifia Mshambuliji huyo mwenye umri wa miaka 22 hasa baada ya kufunga bao la kustukiza katika mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali waliotoka 1-1.

Kasi aliyonayo imechanganyika pia ana uwezo kunyumbulika kwa haraka ikiwamo kuwalamba chenga mabeki na kutoa pasi za uhakika.

Kwa upande wa kitabibu linatazama kasi ya mchezaji huyo toka nchini Brazil kama moja ya vitu ambavyo vinadhihirisha utimamu wa mwili wa mchezaji huyo.

Ukweli kuhusu kasi ya Vinicious Jr

Hakuna uchawi katika kasi anayochomoka nayo Vinicious bali ni uwezo binafsi unaochangiwa na vitu kadhaa ikiwamo umri, mwili, nidhamu, mazoezi, juhudi binafsi, mafunzo, vyakula anavyokula na pia mienendo na mitindo bora ya kimaisha.

Ikumbukwe kasi hiyo hajaionyesha kwa mara ya kwanza bali hata katika mechi zilizopita ikiwamo zile za ligi ya mabingwa Ulaya UEFA katika mechi wa robo fainali dhidi ya Chelsea na za ligi kuu ya la liga.

Lakini linapokuja suala la Madrid kucheza uwanja wao wa Santiago Bernabeu huku wakiwa na maelfu Ya washabiki kunampa ari na hamasa yakucheza kwa kasi.

Haishangazi mchezaji kama Vinicious kuwa na kasi katika mchezo wenye upinzani mkali hii ni inatokana na mashabiki, benchi la ufundi na wachezaji anaocheza nao wanamfanya kuwa na ari ya juu ya ushindi

Kukosa ari ya ushindi ni sawa na kuwa na nyumba bila paa, ari ya ushindi inaweza kumfanya mchezaji kuwa na hisia nzuri hivyo kuweza kujituma bila kuchoka na kusaka ushindi.

Umri wake ni miaka 22, umri ambao mchezaji huwa na misuli michanga ambayo bado haijachoka hivyo kuwa myepesi kupokea mazoezi na kujijenga vyema na kuwa na utimamu imara wa mwili.

Vini Jr ana uzito wa wastani hivyo kumfanya kuwa na uwezo wa kukimbia kasi bila kikwazo chochote.

Mwili wake unamfanya kuwa mchezaji mwepesi mwenye uwezo wa kupanda kushambulia na kurudi kasi kuwakaba maadui waliompokonya mpira.

Mwili wake umezoea mazoezi na kuwa sehemu ya maisha yake hivyo kushikamana mazoezi ya timu na yale binafsi kunampa matokeo makubwa katika utimamu wa mwili.

Kwa kumtazama tu akiwa uwanjani ni mchezaji mwenye juhudi binafsi anayejituma bila kuchoka, mtazame pale anapopoteza mpira huwa anapambana kuhakisha kuwa anaupata.

Na pia ni mchezaji ambaye anapenda kuleta hamasa na ari, mtakumbuka katika mchezo wa juzi alikuwa akiwapa ishara mashabiki kuwa tunashinda shangilieni.

Mwili wa mwanadamu una takribani zaidi ya misuli 650 ambayo kama ikijengwa vyema huweza kufanya mengi ikiwamo kuupeleka mwili kwa kasi kama ya Vinicious.

Lakini kila kitu mwili huratibiwa na ubongo, viungo vya mwili ikiwamo misuli huratibiwa na mfumo huu.

Nidhamu ya hali ya juu na tabia njema ni moja ya nyenzo kwa wanamichezo kufanikiwa kufanya mazoezi na kufuata maelekezo mbalimbali hivyo kucheza kwa kiwango cha hali ya juu.

Mwanasoka anahitaji kasi kwa sababu hizi

Wanasoka wote wanahitaji kuwa na kasi uwanjani, kadiri mchezaji anavyokuwa na kasi ndivyo pia anavyocheza vizuri. Ingawa kasi ya mpira wa miguu ni tofauti na michezo mingine.

Mara kwa mara Mchezaji soka anahitaji kukimbia na mpira na anaweza kuhitajika kukimbia kawaida au kufunguka kwa kasi yenye nguvu kama anavyofanya Vinicious.

Mara nyingi kasi katika soka huitajika mahala pasipotarajiwa, mfano mchezaji anaweza kuwa anakimbia kidogo kidogo lakini anaponyakua mpira anaweza kufunguka kwa kasi ili aweze kushambulia.

Vile vile mchezaji mkabaji atahitajika kufunguka ghafla kwa kasi ili kuweza kumzuia mshambuliaji ambaye si rahisi kukumkuta kama hakuna kasi ya kukimbia.

Hivyo ni kawaida kumwona mchezaji wa soka mara kwa mara kukumbana na mbio fupi fupiza kasi ambazo zinahitaji atumie nguvu kubwa kuweza kufanya hivyo.

Kasi ya mwanasoka inajengwa kwa mazoezi tangu akiwa kinda na anahitajika kutunza uwezo wake wa kuwa na kasi kwa kuzingatia programu nzima ya mazoezi anayopewa na wakufunzi.

Mazoezi ya kujenga kasi huwa na muda maalum, umbali maalum na mtindo wake lakini inahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa mchezaji kutekeleza yote haya.

Kwa sasa nidhahiri kuwa Mwili wa Vini Jr umeiva na amekomaa kiukamavu kitu ambacho kinamsaidia kukabiliana na ushindani na mazingira ya mechi ngumu zenye wachezaji wakali wa kiwango chake.

Unapokuwa na mwili mkakamavu ina maana kuwa mwili huo unaweza kudumu na kuvumilia mambo mengi ikiwamo kutopata majeraha ya mara kwa mara.

Vile vile mchezaji mkakamavu huweza kudumu na mwili wake na kiwango chake kwa muda mrefu zaidi.

Misuli ya mchezaji mkakamavu huwa imejengeka kimazoezi huku ukiwa ni mwili mwepesi kunyumbulika.

Stamina aliyonayo sasa anamfanya kuchez kwa kujiamini, stamina ni uwezo aliojifunza mtu na kunasika mwili mwake pamoja na kuzoeleka na kujengeka katika ubongo.

Baadaye mwili ukaweza kujijenga na kufanya mambo kwa matendo yenye kuonyesha uwezo mkubwa wa kutenda na hivyo mtu ukautumia mara kwa mara kwa kiwango kinachotakiwa kwa muda mrefu.

Hivyo stamina ni mchanganyiko wa uwezo wa mwili pamoja na ukakamavu wake kuweza kudumu kwa muda mrefu bila kuchoka katika mazingira magumu ya mwili ikiwemo kucheza mechi nyingi kwa kiwango cha juu kama anavyoonyesha Vinicious.

Misuli inapojengwa kwa mazoezi, akili nayo inajifunza na hayo mazoezi na aina ya mafunzo ya mchezo husika. Ili kuwa na stamina nzuri ni lazima kuwe na ushirikiano wa hali ya juu ya ubongo na viungo vya mwili

Ukakamavu wa mwili huweza kujengwa kwa mazoezi mbalimbali ikiwamo yale ya viungo, kunyanyua vitu vizito, mazoezi ya uchezaji soka, mbio na kuogelea.

Sababu kubwa ya mchezaji wa soka kuhitaji kasi ya kukimbia ni kuweza kufanya mambo mbali mbali ikiwamo kuwahi kukaba na kushambulia.

Kasi ya Vini Jr ni balaa kwa mabeki wa timu pinzani, tusubiri kuona kama ataiwezesha Madrid kushinda katika mchezo wa pili wa nusu fainali utakaochezwa jijini Manchester.

Columnist: Mwanaspoti