Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTIDOKTA: Jeraha la Neymar liko hivi...

Neymar Jr Injuryy Neymar akiugulia maumivu

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mshambuliaji wa soka wa AL Hilal na staa wa Timu ya Taifa ya Brazil, Neymar Jr amepata jeraha baya la goti wakati akitimiza majukumu ya timu ya taifa.

Staa huyu mwenye umri wa miaka 31 alipata majanga hayo katika mchezo ambao timu yake ilichapwa mabao 2-0 dhidi ya Uruguay. Neymar alitua vibaya aridhini katika nusu ya kwanza ya mchezo.

Imelelezwa mchezaji huyu amepata jeraha la kukwanyuka kwa nyuzi ngumu aina ya Ligamenti ijulikanayo kitabibu kama Anterior Cruciate Ligament (ACL) na kijifupa bapa plastiki kijulikanacho kama Meniscus katika ungio la goti la mguu wa kushoto.

Ugunduzi wa awali ulionyesha kuwa amepata jeraha la baya la nyuzi ngumu ya ligamenti ijulikanayo kama Anterior Cruciate ligament-ACL iliyopo katikati ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na ugoko.

Vipimo vya picha ya MRI ndio vilithibitisha kuwa mshambuliaji huyo aliyetua kutoka PSG kwa mamilioni ya dola amejeruhi nyuzi ya ACL na kifupa bapa cha katikati ya goti.

Jeraha baya la goti linakadiriwa kuwa huenda likamweka nje ya uwanja kwa muda wa miezi 8-10. Hii ni habari mbaya kwa klabu na timu ya taifa kwani ni mchezaji tegemezi pande zote mbili.

Leo nitawapa ufahamu wa nyuzi ya ligamenti ya ACL iliyokwanyuka na kifupa bapa cha katikati ya goti yaani meniscus.

LIGAMENTI ZA GOTI ZINA KAZI HIZI

Katika pitapita za kimaisha ni kawaida kukutana na maneno mawili ya kitabibu yaani sprain na strain, maneno haya yanaweza kukuchanganya na usijue tabibu amelenga nini.

Unaposikia sprain injury maana yake ni yale majeraha ya kuvutika kupita kiasi au kuchanika kwa nyuzi za ligament ambazo katika ungio (joint) huunganisha mfupa mmoja na mwingine.

Wakati kwa strain huwa ni majeraha yanayohusisha misuli na muushilio wake kitabibu tendon, aidha inaweza kuwa ni nyuzi ndogondogo za misuli kujeruhiwa au kuvutika au kukatika kwa tendon.

Kwa ujumla ligament zote huwa na kazi za kuunganisha mifupa inayotengeneza ungio na kuituliza katika eneo lake usiende uelekeo hasi na hatimaye uingio kuwa imara na kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Katika goti zipo ligament nne zinazounda ungio lijukanalo kitabibu kama knee joint.

Anterio Cruciate ligament-ACL ipo eneo la katikati ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na mfupa mkubwa goti. Kazi yake ni kuzuia uelekeo hasi wa mbele wa mfupa wa ugoko na kudhibiti kujizungusha.

ACL ndiyo kinara kwa kujeruhiwa mara kwa mara ukilinganisha na nyingine, dalili ya kipekee ya kujeruhiwa kwa ligament hii ni kutokea kwa mlio mara baada ya kujeruhiwa.

Posterior Cruciate Ligament-PCL ipo upande wa nyuma ikizuia uelekea hasi wa nyuma wa mfupa wa ugoko.

Medial Collateral Ligament-MCL ipo pembeni uelekeo wa nje ya mwili ikiwa na kazi ya kuimarisha mifupa usiende uelekeo hasi ndani ya goti.

Lateral Collateral Ligament-LCL ipo uelekeo wa ndani ya mwili ikitoa uimara nje ya goti.

Mara nyingi hupata majeraha pale mchezaji anapojipinda uelekeo hasi na kulazimisha nyuzi hizi kwenda uelekeo usio wake na kuvutika kupita kiasi na hata kukatika au kuchanika.

Taarifa za jumla za kifupa plastiki cha goti

Kifupa hiki hujulikana kitabibu kama Medial Meniscus kipo katikati ya goti kikiwa na ugumu kama plastiki na umbile la bapa, kazi yake ni kuzuia mfupa mkubwa wa paja na wa ugoko kugusana na kusuguana.

Kimeundwa na nyuzi ngumu ngumu zilizo mfano wa plastiki zilizoshikamana pamoja, aina ya vifupa hujulikana kitabibu kama Cartilage.

Uundaji wake na kuifanya kuwa kama plastiki ngumu na uwepo wake katika goti huwa na kazi ya kunyonya mawimbi ya shinikizo la uzito wa mwili, bila uwepo wake ina maana mifupa hiyo mikubwa ingelikakutokana na kugusana moja kwa moja.

Kifupa hiki kitabibu hujulikana pia kama ‘Shock Obsorber’ husaidia mjongeo laini bila msuguano wa mifupa mikubwa ya ungio la goti .

Kifupa hiki huweza kupata majeraha ikiwamo kupasuka au kuvunjika au kupata mchaniko. Matendo yanayosababisha haya ni pamoja na kujipinda kwa goti uelekeo hasi au kutua vibaya kwa shinikizo kubwa.

Kinaweza kuwekwa katika madaraja matatu ya majeraha ikiwamo la kwanza ni kutoka ufa tu, la pili ni kupasuka kusiko kamili na tatu kupasuka kamili pande mbili au zaidi.

Daraja la kwanza huweza kupona bila upasuaji na daraja la pili na tatu huitaji upasuaji kama ilivyokuwa kwa Neymar ambapo ni dhahiri amepata mpasuka wa daraja la pili.

Dalili na viashiria vya awali

Baada ya kupata majeraha hayo katika mechi iliyokuwa na upinzani Neymar alionekana akikaa chini huku akishikilia eneo la mbele la mguu wake wa kushoto.

Alionekana kutoa ishara ya kuumia sana na alipatiwa huduma ya kwanza lakini bado haikubadili kitu, hivyo alilazimika kutolewa nje kwa usaidizi wa machela.

Kwa kawaida dalili huwa ni maumivu katika eneo la mbele la goti, eneo la goti kuvimba, mara nyingine kutokea mlio usiokuwa wa kawaida wa msuguano, kushindwa kuutumia mguu uliojeruhiwa na kuchechemea.

UCHUNGUZI NA MATIBABU

Mara baada ya kutolewa Neymar alifanyiwa uchunguzi wa kina pamoja na picha za X-ray na skani ya MRI zilizobaini mvunjiko wa kifupa plastiki cha goti pamoja na kukwanyuka kwa nyuzi ngumu ya ACL Ligamenti.

Habari nzuri ni kuwa majeraha haya yanatibiwa kwa upasuaji wa kisasa wa matundu ambao unatoa matokeo makubwa katika majeraha haya yatokanayo na michezo

Kipimo cha Anthroscope ni kipimo cha kisasa chenye taa na kamera ambacho hupitishwa katika matundu yalichanwa katika goti na huweza kubaini na vile vile kukarabati ligament kama matibabu.

Zipo aina tatu za upasuaji wa magoti unaofanywa mara kwa mara ikiwamo Anrthroscopic Repair unaohusisha upasuaji wa kawaida, Partial meniscotomy unahusisha ukarabati wa kati na Total meniscotomy unaohusisha upasuaji mkubwa.

Aina ya tatu ya upasuaji ndiyo ambao ukifanyika huchukua muda mrefu kupona ikikadiriwa miezi 3-6. Kwa aina ya upasuaji wa kwanza mgonjwa anaweza kuchukua wiki 4-6 mjeruhiwa kupona kamili.

Kwa aina zote upasuaji kwa wastani huchukua saa 2-4 ingawaje pia itategemea kama kuna tishu za jirani zilizojeruhiwa katika tukio husika.

CHUKUA HII

Majeraha haya hayana njia ya moja kwa moja ya kuyazuia zaidi ni mchezaji kutakiwa kuepuka matendo yasiyo ya lazima ikiwamo kucheza kwa uangalifu na kuepuka mijongeo hasi ya ungio la goti.

Columnist: Mwanaspoti