Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTIDOKTA: Hisia inaweza kuathiri upigaji Penalti

Simba Shirikisho .png Wachezaji wa Simba

Fri, 5 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kutolewa kwa Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mikwaju ya penalti Ijumaa iliyopita na Wydad Casablanca nchini Morocco lilikuwa pigo lililoleta simanzi hapa nchini. Penalti zilizopigwa na Shomari Kapombe na ya mwisho ya Clatous Chama walizokosa ni dhahiri zilileta mpasuko wa hisia kwa wachezaji wa timu na mashabiki wa Simba hali ambayo ni ya kawaida kutokea.

Hali kama ile huku ukiwa ugenini ambako kuna mashabiki wajulikanao kama Ultra ambao hupiga kelele na kuimba mwanzo mpaka mwisho wa mechi haishangazi mchezaji kupata hofu na hatimaye kukosa umakini. Pamoja na kwamba Simba walikuwa ngangari katika mchezo huo wakacheza bila kujali kelele kiasi cha kumaliza dakika 90 za mchezo wakiwa wamefungwa bao 1-0 hivyo kulazimika kwenda hatua ya matuta.

Kurundikana kwa mpasuko wa hisia kwa mchezaji kunaweza kuathiri upigaji wake wa penalti kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kelele za mashabiki, mazingira mapya, woga au hofu ya kufungwa, kosa la awali, kulaumiwa na kucheza chini ya kiwango. Siku zote katika matokeo kama yale siyo tu yanaumiza wapenda soka, hata wachezaji wenyewe kiasi cha kuwapa kihisia hasi hapo baadaye, hivyo kuweza kuchangia kufanya vibaya katika mechi zijazo kama hatua za wataalamu wa kisaikolojia hazitachukuliwa.

Mpasuko wa hisia kwa wachezaji unaongeza hatari ya kufanya vibaya ikiwamo hata kuathiri umakini wakati wa upigaji penalti ikiwamo wale wachezaji wenye historia ya kutokosa mikwaju hiyo. Ndiyo maana klabu kubwa au timu za taifa huajiri wanasaoikolojia tiba kwa ajili ya kuwapa huduma ya tiba ya kisaikolojia wachezaji kabla na baada ya mechi.

Hawa wanakuwepo mpaka uwanjani kuzungumza nao wakati wa mapumziko au kama wakati wa mapumziko wakati wa kujiandaa na upigaji wa penalti. Wachezaji wengi mpira ni ajira inayowapa pesa. Jaribu kuvaa viatu vyao na fikiria kuwa ukitolewa unakosa bonasi na marupurupu na pia kuna zigo la Sh10 milioni 10 kwa kila goli kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mawazo yanaweza kumpa mchezaji hisia chanya au hasi na kuathiri umakini wake katika kupiga penalti na kupata au kukosa. Mfano mchezaji mwenye furaha sana (hisia chanya) au mwenye huzuni kali (hisia hasi) ni rahisi kukosa umakini kulinganisha na yule mwenye hisia ya kati. Hivyo kuyumba kwa hisia kunaweza kuathiri upigaji penalti ikiwamo kupata au kukosa.

UMUHIMU WA UTULIVU KIAKILI

Ikumbukwe kuwa mchezaji kucheza katika kiwango bora na kufanya vizuri zaidi anahitaji kuwa na utulivu wa kiakili ili kujiamini wakati wote wa mchezo mpaka hatua ya penalti. Mchezaji anaweza kuvurugwa kisaikolojia kabla, wakati na baada ya mechi na ndiyo maana ndani ya timu kuna wachezaji ambao huwa viongozi kuwatuliza wenzao wenye mihemko hasi uwanjani.

Nahodha wa timu, msaidizi wake na kipa ni watu ambao mara kwa mara wanatumika kuwatuliza wenzao waliovurugwa kihisia mara tu wanapofungwa kizembe au pasipo kutegemea. Ndio maana Kapombe alizungukwa na wenzake ili kumpoza na kumfariji na vilevile kupoza tukio ili wengine wasiweze kupata mpasuko wa hisia zaidi.

Kukabiliana na hali kama hizo wachezaji hupewa msaada wa kisakolojia kutoka kwa wataalam wa tiba, wanasaikolojia tiba, benchi la ufundi, kocha, wachezaji wa akiba na mashabiki. Sababu zinazochangia ufanisi hafifu wa wachezaji ni mjengo dhaifu wa kisaikolojia katika kupata ushindi. Inawezekana maandalizi ya kiufundi yakawa mazuri, lakini hisia zikavurugwa hivyo kushusha ari.

Mchezaji akishapata hitilafu ya kihisia anashindwa kucheza kwa umakini uwanjani ikiwamo kucheza fyongo kama vile kutoa pasi za ovyo au kushindwa kumalizia mabao ya wazi. Utulivu wa akili unajengwa kwa kuweka mawazo chanya na inawezekana tu endapo kuna mfumo uliowekwa ili kuwajengea wachezaji hisia nzuri zinazochochea ari ya ushindi.

Licha ya matayarisho kabambe ya mazoezi ya kila siku na kuwahi kufika ugenini na kuzoea mazingira ya mpinzani, bado wachezaji wanahitaji kujengewa hisia chanya ili wajione kuwa wanaweza kushinda popote. Simba walionyesha uimara kisaikolojia katika mechi licha ya kupigwa 1-0 hawakuruhusu bao la pili hatimaye kuifanya mechi kwenda hatua ya matuta.

Inapobainika kuwa kuna mchezaji ana hisia hasi anaweza kupewa muda kutuliza akili na kupewa maneno ya faraja ili kumuondolea hisia hasi. Ikumbukwe kuwa hisia hasi zikimganda mchezaji zina athari kubwa katika kufanya uamuzi hivyo kukosa umakini katika majukumu ya uwanjani ikiwamo kupiga penalti. Wataalam wa saikolojia ya michezo wanakubali kuwa hisia nzuri huleta matokeo mazuri.

Unapokuwa na hisia chanya inakupa nguvu ya kucheza wakati unapopoteza hamasa kunakufanya uchoke na kupata hasira kila mara hivyo kuhatarisha hisia na afya kiujumla.

JINSI YA KULETA HISIA CHANYA

Wataalamu wa saikolojia ya soka wanapendekeza hatua sita ambazo zinaweza kumuepusha mchezaji na mpasuko wa kihisia kabla, wakati akicheza na baada ya mechi kuelekeza mechi zijazo. Hatua ya kwanza wapewe hamasa ili kuwapa mjengo bora wa tabia na mwenendo unaoleta hisia chanya, hivyo kujiamini na kuwa na ari ya ushindi mechi zinazofuata.

Pili, kukubali makosa yanayojitokeza katika mechi bila kugadhabika na vilevile kulinda kusitokee madhara kwa wengine hivyo kushusha ari na hamasa ya ushindi. Mfano Kapombe na Chama walionyesha hali ya kukubaliana na makosa yaliyotokea ya kukosa penalti katika mchezo huo. Hii inawajenga kuwa na hisia chanya katika mechi zinazofuata.

Tatu na nne ni kujiweka katika viwango bora na kutengeneza nguvu ya sauti ya matumaini. Licha ya kufungwa mchezaji abaki na kauli za kutoshindwa. Wachezaji wakiwa ndani ya uwanja watoe kauli za kuleta hamasa mioyoni na kwa wengine ili kufanikisha au kulinda ushindi na vilevile kulinda hisia chanya kwa timu.

Tano, kila mchezaji achukue majukumu kamili na kuepuka kuwapa lawama au kuwanyooshea vidole wengine. Hii hutunza hamasa ya ushindi na kucheza zaidi. Sita, umakini na hisia kabla ya mechi ili kama kuna hisia hasi mchezaji asaidiwe ili kurudi katika hisia chanya.

MASHABIKI SIMBA

Katu mashabiki wa Simba wasiwashutumu wachezaji au bechi la ufundi kutokana kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika kwani kunaweza kufanya kukosa hamasa na ari ya ushindi katika mechi zijazo.

Mfano hai ni makosa ya mara kwa mara yanayofanywa na beki wa kati wa Manchester United, Harry Maguire yanaweza kuwa yanachangiwa na kuwa na hisia hasi kwani kila kona anatupiwa lawama. Wana Simba Wasamehe na kusahau ya Waydad na wagange ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwani ndiko walikobakiza kusaka mafanikio msimu huu.

Columnist: Mwanaspoti