Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Yanga vs Simba, sababu hizi mashabiki hawakuzimia

Mkapa Stadium Lupaso Yanga vs Simba, sababu hizi mashabiki hawakuzimia

Fri, 6 May 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki hii gumzo kubwa lililotawala ni mechi ya watani wa jadi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo uliochezwa saa 11 jioni huku baadhi ya mashabiki na wachezaji wakiwa katika mfungo wa mwezi mtukutu wa Ramadhani ulishuhudiwa timu hizo zikitoka suluhu na kugawana pointi moja moja. Mashabiki mitandaoni wanasema matokeo hayo yalileta utulivu pande zote, kwani hakuna aliyepatwa na maumivu wala furaha ya ushindi iliyopitiliza.

Ni kawaida kubeba hisia za maelfu ya mashabiki ndani na nje ya nchi ikiwamo wale wanaotazama mechi hiyo moja kwa moja au wanaofuatilia kwa njia ya redio na runinga. Burudani ya soka hubeba hisia za juu za mashabiki kiasi kwamba huwa ni kawaida wengine kuumia kihisia au kujikuta wakipoteza fahamu kutokana na mshtuko wa furaha au karaha.

Kutokuwepo kwa mabao na kutoka bila bila ni moja ya sababu mchezo huo kupungua kwa matukio ya mashabiki kuanguka na kuzimia uwanjani. Kwa utafiti wa kutazama tu utabaini michezo ya nyuma ya klabu hizi kulikuwa na matukio kadhaa ya mashabiki kuzimia au kupata mstuko uliokithiri pale mojawapo inapofungwa au kushinda.

MTAKUMBUKA TUKIO LA SHABIKI

Kupoteza maisha ni tukio la kusikitisha ni lile la wilayani Mpwapwa la kufariki ghafla kwa mtu mmoja wakati akitazama mechi hiyo katika runinga.

Tukio hilo lilitokea mwaka jana muda mfupi kabla ya Yanga kupata bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambapo Yanga walishinda 1-0 na kutwaa ngao hiyo.

SABABU KUTOZIMIA

Hali ya hewa katika mchezo wa majuzi ilikuwa rafiki. Siku ile kuchezwa mchezo ule nyakati za jioni ilikuwa na faida kiafya kwani miili ya mashabiki haikupoteza maji mengi kutokana na hali ya hewa ya jioni kuwa sio ya joto kali.

Mashabiki kufuata utaratibu uliowaepusha kuwa katika msongamano unaoweza kumhatarisha mtu kubanana na kukosa hewa safi.

Huduma mbalimbali za vinywaji na vyakula vilikuwa katika mazingira ya uwanja huo, hivyo mashabiki walipata maji, juisi, soda, ice cream na vitafunwa. Hii iliwasaidia kuepukana na kuzimia kutokana na upungufu wa maji mwilini na vilevile kuepuka kuzimia ambako kungetokana na sukari ya mwili kushuka kutokana na njaa.

Miundombinu ya uwanja na mazingira yanawezesha maelfu ya mashabiki kupata hewa safi ya kutosha kutoka pande zote za mzunguko wa nyuzi 360. Lakini pia, mashabiki walishikamana na maelekezo waliyokuwa wanapewa na wasimamizi wa uwanja.

KINACHOSABABISHA MTU KUZIMIA

Kuzimia ni hali ya mwili kuzima mawasiliano ya nje ghafla kwa muda mfupi na hatimaye huendelea kuwajibika na mawasiliano ya ndani ya mwili tu ili kusahihisha dosari inayoweza kutishia uhai.

Lakini wengi wanauliza kulikoni hali ile imempata mchezaji wa kulipwa ambaye suala la utimamu wa afya yake ni jambo muhimu.

Ieleweke kuwa unaweza kuwa timamu kiafya mara baada ya kupima lakini kumbe hapo baadaye matatizo ya kiafya huibuka ghafla wakati unafanya majukumu mbalimbali ikiwamo kucheza. Mara nyingi sababu kubwa inayochangia watu kuzimia ni ubongo kukosa hewa ya oksijeni kunakochangiwa na matatizo ya mapafu, moyo na mishipa ya damu na pia kuvuta hewa yenye sumu ya carbon monoxide.

Kwa upande wa matatizo ya moyo yanayoweza kusababisha mtu kuanguka ghafla na kuzimia ni pamoja na moyo kusimama ghafla au shambulizi la moyo ama matatizo ya mishipa ya damu.

Kuzimia ni moja ya njia za kujihami kwa mwili kutoa nafasi rasilimali zake ambazo ni damu na oksijeni kutumika katika maeneo nyeti ya mwili na kunyima zile ambazo hazina umuhimu kwa uhai wa mwili.

Maeneo nyeti ya mwili kwa ajili ya uhai ni pamoja na ubongo, moyo, mapafu, ini na figo.

Dalili ambazo mara kwa mara ni ishara ya kuzimia ni pamoja na hisia za uzito miguuni, kukosa nguvu, kuona giza, kizunguzungu, kupata hali ya kichefu chefu, kupiga miayo mara nyingi bila sababu, kuweweseka au kuchanganyikiwa na kuhisi joto au moto.

Yapo mambo mengine yanayosababisha mtu kuzimia ambayo ni pamoja na mwili kupata mstuko, sukari mwilini kushuka au kupanda sana, upungufu mkali wa maji, kunywa sumu au usugu wa vimelea, upungufu wa damu, vichochezi na dawa za matibabu.

KUMHUDUMIA ALIYEZIMIA

Ingawa hakuna njia ya moja kwa moja inayozuia mtu kuzimia, pale unapopata dalili za kuzimia ni vyema

kujisogeza eneo ambalo litakuwa salama endapo utazimia na kuanguka. Kwa mtu aliyezimia atahitaji kutathiminiwa kama anapumua au hapumui.

Inashauriwa kama upo jirani na mtu aliyezimia na atakuwa anapumua ni vyema haraka umlaze mahala salama, nyanyua miguu yake na uitikise tikise ili damu nyingi iende maeneo nyeti, mfungue mkanda au legeza mavazi aliyovaa na ondoa vizuizi vya mavazi na kisha mlaze ulalo wa uponaji.

Kama atakuwa anapumua vizuri, basi msikilizie kwa dakika moja na pata msaada wa watoa huduma au mkimbize katika huduma za afya. Ikiwa atakuwa hapumui, haraka tathmini upumuaji wake na tazama njia ya hewa kama ina mkwamo au kizuizi.

Kama atakuwa hapumui na hakuna mapigo ya moyo anza huduma ya ufufuaji wa moyo na upumuaji yaani CPR. Endelea kufanya CPR mpaka pale msaada utakapokuja.

USHAURI

Umuhimu wa CPR ndiyo unafanya elimu yake kutolewa tangu elimu ya msingi kwa lengo la kuikuza jamii iwe na ufahamu wa huduma hii inayoweza kuokoa maisha ya mgonjwa. Ni muhimu kushikamana na elimu hii na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kuzingatia taratibu na miongozo inayowekwa na wasimamizi wa viwanja wakati wa mechi kubwa za soka.

Columnist: Mwanaspoti