Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Tizi na misosi ndo mpango mzima kudhibiti ubonge

Lukaku Nyavu Straika wa Chelsea

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hivi karibuni tuliona straika wa Chelsea, Romelu Lukaku alivyokuwa bonge kiasi cha kukejeliwa, lakini akapambana na kufanikiwa kupata mwonekano mzuri tofauti na ule wa awali.

Licha ya kufanya mambo mbalimbali na kufanikiwa kupunguza uzito wa mwili kutokana mazoezi na udhibiti wa vyakula ambao ndiyo mpango mzima wa kukabiliana na mtu kuwa bonge, lakini Lukaku awali alikuwa bonge mtu.

Si Lukaku tu, lakini wachezaji wengi wamejikuta wakiwa vibonge kama ambavyo hivi karibuni, Ibrahim Ajibu alipokuwa Simba kabla ya kutua Azam, naye alionekana kuwa kibonge tofauti na alivyozoeleka.

Lakini nilikutana na swali linalohusu dawa za kupunguza uzito au unene ambazo nyingi zinatangazwa sana mitandaoni.

Bahati mbaya Fifa ilipiga marufuku dawa za kupunguza uzito kwani baadhi zinafanana kiutendaji na zile za kuongeza nguvu mchezoni.

Mtakumbuka mchezaji wa zamani wa Arsenal, Kolo Toure aliwahi kupimwa na kukutwa anatumia dawa za kuongeza nguvu mchezoni zilizopigwa marufuku, lakini baadaye alipunguziwa adhabu baada ya kubainika kuwa alizitumia kwa bahati mbaya kwani alimuona mkewe akitumia dawa za kupunguza uzito naye akaamua kuzitumia.

Hivyo hapa tunapata picha kuwa dawa za kupunguza uzito au kuongeza nguvu sio njia sahihi ya kukabiliana na uzito uliokithiri, bali imebaki mazoezi na udhibiti wa vyakula ndio mpango mzima.

Wachezaji hasa wanasoka vijana ni kawaida kujikuta wakivuta au kutumia dawa za kudhibiti uzito wa mwili kutokana na zama hizi za utandawazi.

Wengine wanajikuta wanatumia dawa hizo ambazo nyingi zina madhara na bahati mbaya au kukosa ufahamu wa kutosha juu ya matumizi ya dawa hizo.

Leo nitawapa ufahamu kuhusu dawa za kupunguza uzito uliokithiri au unene.

DAWA ZA KUPUNGUZA UZITO

Ni kweli upunguzaji uzito wa mwili kwa kutumia dawa ni moja ya tiba ambayo inawachanganya watu na hii ni kutokana na uwepo wa taarifa nyingi mitandaoni na matabibu wa kienyeji wanaotangaza kupunguza uzito wa mwili.

Kisayansi njia salama ya kukabiliana na unene ni mazoezi mepesi na ulaji sahihi wa vyakula kwa kuzingatia kanuni za afya. Njia hii hasa kwa mazoezi ya kila siku ndio inakubalika kama nyenzo inayoukabili unene ukilinganisha na dawa za kupunguza unene.

Katika huduma za afya hakuna dawa iliyoidhinishwa na ipo ndani ya miongozo ya matibabu ya kitaifa na kimataifa ikiwamo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo ni salama ili kupunguza uzito wa mwili. Zaidi miongozo mingi inasisitiza unene uliokithiri au uzito mkubwa huweza kudhibitiwa kwa mazoezi na vyakula.

Bado taasisi nyingi za chakula na dawa duniani zinatilia shaka usalama wa dawa za kupunguza uzito, ndio maana hazipo katika miongozo ya matibabu.

Vipo vidonge ambavyo vimekuwa vikitumiwa mara kwa mara duniani katika nchi zilizoendelea kukabiliana na uzito ambavyo ni pamoja na Orlistat, Belviq, Contrave, Sexenda, Phentermine na Qsymia.

Baadhi ya dawa hizo zinafanya kazi mwilini ikiwamo kuzuia unyonyaji wa mafuta na sukari katika mfumo wa chakula, huku nyingine huchochea homoni inayotaarifu ubongo kuwa tumbo limejaa chakula na kukunyima hamu ya kula.

Mtu anayeruhusiwa kuandika dawa za kupunguza uzito wa mwili ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) pekee na hii ni kutokana na ukweli kwamba dawa zina madhara makubwa ikiwamo kusababisha shambulizi la ghafla la moyo.

Vilevile hutoa dawa hizo kwa watu ambao zao la uwiano wa uzito wa mwili na urefu wa mwili (body mass index) ni zaidi ya 30 au pengine ni 27 na huku tayari wameanza kupata madhara ya unene ikiwamo kuugua kisukari aina ya pili. Pia, inapoonekana kuwa mbinu ya vyakula na mazoezi mepesi imeshindikana.

Sio kila mtu anaweza tu kutumia dawa hizo, ni lazima watalaamu wa afya wamfanyie uchunguzi wa kina kuona kwamba mwili wake utaweza kukabiliana na madhara yatokanayo na dawa hizo.

Madhara ya dawa za kupunguza unene wa mwili ni pamoja na kupata maumivu ya tumbo, choo chenye mafuta, kuumwa kichwa, kichefuchefu, kizunguzungu, sukari ya mwili kuwa chini, mapigo ya moyo kudunda bila mpangilio na kukosa usingizi.

Ieleweke kuwa kutumia dawa hizo holela bila kumuona daktari ni sawa na kuyaweka maisha yako hatarini. Sio salama kwa afya yako kutumia dawa za kupunguza unene.

FANYA HIVI

Mbadala sahihi wa dawa hizo ni mazoezi mepesi ya mara kwa mara ikiwamo kutembea umbali wa kilomita mbili kila siku kwa siku tano za wiki, kuruka kamba, kuendesha baiskeli, kuogelea, kucheza muziki uliochangamka na kufanya shughuli za kuushugulisha mwili.

Ukiacha wachezaji ambao hufanya mazoezi kila siku kwa watu wengine wanatakiwa angalau kufanya mazoezi mepesi kwa dakika 30-60 kwa siku kwa siku tano za wiki. Ni vizuri wachezaji na watu wa kawaida wakazingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kuepuka kutumia dawa holela.

Mbadala sahihi wa kukabiliana na uzito wa mwili ni mazoezi mepesi na udhibiti wa vyakula vya kunenepesha ikiwamo wanga, sukari na mafuta.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz