Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Sababu kifo cha pacha wa Ronaldo

Pacha Pic Data Ronaldo na Familia yake

Fri, 29 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wiki iliyopita mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Manchester United alitoa taarifa ya kujifungua kwa mchumba wake Georgina Rodriguez, lakini bahati mbaya pacha wa kiume alifariki dunia.

Aliandika katika kuta za ukurasa wa mtandao wa Instagram kuwa kwa masikitiko makubwa yeye na mchumba wake wameumizwa kutokana na kumpoteza ‘malaika’ mtoto pacha wa kiume, ila kuzaliwa salama kwa pacha wa kike kunawapa faraja kubwa.

Msiba huu ndio pia ulichangia kwa mshambuliaji huyu mwenye miaka 37 kutokuwepo katika mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) dhidi ya mahasimu wao Liverpool uliochezwa Jumapili wiki juzi. Mashabiki wa Liverpool wakiwa katika uwanja wao wa Anfield walionyesha uungwana kimchezo wa hali ya juu kwa kusimama na kuimba wakionyesha mabango ya kuifariji familia ya Ronaldo. Tukio hilo lilipokewa vyema na familia ya Ronaldo ikiwamo dada yake ambaye alisema kamwe hawezi kusahau tukio hilo kwani liliwapa faraja isiyoelezeka.

Akiwa ametoka katika tukio hilo, alijumuishwa katika mchezo wa EPL uliochezwa Jumamosi dhidi ya Arsenal na kufanikiwa kufunga bao la kufutia machozi. Itakumbukwa Oktoba, mwaka jana, Ranaldo alitangaza kuwa mchumba wake ana ujauzito wa watoto mapacha.

Kibinadamu kitendo cha kupata mimba pacha hupokewa kwa furaha kubwa, lakini kwa upande wa kitabibu aina hii ya mimba huwa na magumu mengi yanayojitokeza wakati wa ukuaji mimba na wakati wa kujifungua. Kutokana na umaarufu wake nguli huyu ambaye mpaka sasa ana mabao 15 Man United ni kawaida pia kujitokeza maswali kadhaa ikiwamo sababu za kifo na kama je shida hiyo ilitokana na uzembe wa matabibu? Maswali mengine yaliyoulizwa kutokana na tukio hilo ni pamoja na mimba pacha inatokea vipi? Je alipata mimba pacha kwa njia ya kawaida au ya kupandikiza. Hata wanaomfuatilia Ronaldo kupitia Instagram walikuwa na shauku ya kujua ni sababu gani zilichangia kifo cha pacha huyo wa kiume.

Taarifa iliyotolewa na familia ya Ronaldo haikueleza sababu zilizochangia kifo hicho na wala hospitali aliyojifungulia iliyopo nchini Ureno haiwezi kutoa taarifa kwa jamii bila ruhusa ya familia. Leo katika kona hii tutazitupia macho sababu zinazoweza kuchangia kifo kwa mmoja pacha katika ujauzito wa pacha na kupitia tukio hilo lipi la kujifunza.

SABABU NI HIZI

Kwa kawaida ujauzito pacha unatungwa mara baada ya vijiyai zaidi vya kike vilivyokomaa kuungana na mbegu ya kiume au kijiyai cha kike kuungana na mbegu ya kiume na hatimaye kugawanyika katika mimba changa mbili. Ujauzito pacha unaweza kutokea kwa njia ya asili au isiyo ya asili ya upandikizaji kwa maabara ijulikanayo kitabibu kama Invitro Fertilization maarufu kwa kifupi IVF. Kwa Ronaldo wakati akitangaza mchumba wake kuwa na ujauzito wa mapacha hakueleza ilikuwa ni wa njia gani. Ingawa ni furaha kupata mimba pacha, lakini upande mwingine ni aina ya ujauzito ambao huwa katika hatari kubwa ya kujitokeza kwa madhara mbalimbali - kwa pande zote mbili yaani mama na watoto.

Mama mwenye mapacha anakabiliwa na hatari ya kupata shinikizo la juu la damu mara tano zaidi, kujifungua kwa upasuaji kutokana na watoto kukaa vibaya, upungufu wa damu, kuwa na maji mengi au machache yanayomzunguka mtoto na kupoteza damu nyingi anapojifungua. Vilevile yupo katika hatari zaidi ya kujifungua njiti, mimba kuharibika mapema, kifafa cha mimba na matatizo ya mfumo wa damu wa kondo la nyuma kwa

watoto mapacha wanaotumia kondo moja. Ila hapa nitayalenga madhara mbalimbali yanayojitokeza na kuweza kuchangia kifo kwa mmoja wa mapacha kupoteza maisha.

Sababu zinazoweza kusababisha pacha mmoja kufariki dunaia zinaweza kuwa wakati wa ukuaji wa mimba katika nyumba ya uzazi, wakati wa kuzaliwa na muda mfupi baada ya kuzaliwa. Sababu za kufariki wakati wa ukuaji katika nyumba ya uzazi inaweza kuwa matatizo katika kondo la nyuma ikiwamo kukwanyuka au kujipachika vibaya kwa kondo la nyuma, ajali ya kitovu, sababu za kijenetiki au chembe za urithi.

Vilevile hitilafu ya kimaumbile ya pacha, kisukari cha ujauzito, maambukizi ya virusi wanaoharibu mimba na mama kuwa na upungufu mkubwa wa damu usiodhibitiwa.

Sababu za wakati wa kujifungua inaweza kusababisha kukwama katika tundu la pango la kiuno, kuishiwa nguvu wakati wa kupita, kitovu kukaba shingo na kujeruhiwa wakati wa kuzaliwa.

Kwa upande wa sababu za vifo mara baada ya kujifungua inaweza kuwa jeraha la ubongo, matatizo ya mfumo wa upumuaji, kuzaliwa na maumbile yasiyo timilifu, joto la mwili kushuka na sukari ya mwili kushuka. Ukiacha sababu hizo zipo pia zinazohusu makosa ya watoa huduma wakati wa kumsaidia mtoto kuzaliwa ambayo yakifanyika yanaweza kusababisha kifo cha pacha au mapacha wanaozaliwa.

FUNZO MUHIMU

Pamoja na kupata msiba huu, lakini Ranaldo alifarijika kwa kubakiwa na pacha wa kike. Alisimama imara kipindi hiki chote kiasi cha kurudi kuitumikia timu yake kama vile hakupata msiba. Pamoja na kwamba alikuwamo katika mchezo waliopoteza 3-1 dhidi ya Arsenal, Jumamosi katika mchezo wa EPL, lakini ndiye pekee aliyefunga bao kufutia machozi.

Hii dhahiri kuwa mchezaji huyu amepata watu wa kumpa faraja ambayo imesaidia kumpa tiba ya huzuni ambayo ni kawaida kumpata mtu ambaye amefiwa.

Jambo lingine la kujifunza kwa Ronaldo ni kutambua majukumu ya uwanjani na familia, aliporudi uwanjani alisahau shida zake na akaonyesha utayari wa kucheza kwa nguvu na kasi ili kuisaidia timu kushinda. Ingawa hawakushinda, lakini Ronaldo alifunga bao la kufutia machozi. Mshikamano wa kifamilia unamfanya Ronaldo kupata utulivu wa kiakili. Mara nyingi yupo karibu na mchumba wake na watoto. Vilevile mara kwa mara yupo pia karibu na mama na dada yake ambao hata tukio hili lilipotokea walikuwa naye bega kwa bega kumpa faraja. Ikumbukwe kuwa uwepo wa mifarakano ya kifamilia inaweza kumfanya mtu kuwa na matatizo ya kiakili ikiwamo msongo wa mawazo, sonona, hofu au wasiwasi.

Mchezaji anapokuwa na shida hizi na ikiongezeka nyingine anajikuta anaelemewa na mzigo wa matatizo ya akili, hivyo kumfanya kukosa utulivu wa kiakili na hatimaye kushindwa kutimiza majukumu ya klabu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz