Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Pele anahitaji faraja hizi

Pele2 Pele

Fri, 9 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar likingia katika hatua ya robo fainali hali ya gwiji wa soka wa duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ sio nzuri kiasi cha kuwa katika uangalizi maalumu, ICU nchini Brazil.

Pele ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 82 amekuwa katika wakati mgumu kiafya tangu mwaka 2020 kiasi cha kumfanya kushindwa kutoka hadharani kuhudhuria matukio mbalimbali ya kijamii.

Jumatatu ilitangazwa katika vyombo vya habari ikiwamo Reuters, Dailymail na The Mirror kuwa hali yake ilibadilika ghafla na kulazimika kuwekwa katika ungalizi maalumu katika Idara ya Tiba ya dharula mara baada ya matibabu ya moyo na mionzi kutompa nafuu.

Novemba 29, mkongwe huyo alikimbizwa katika huduma za afya kutokana na kusumbuliwa na uvimbe tumboni, moyo kushindwa kufanya kazi na saratani ya utumbo mpana.

Taarifa ya kuumwa iliwafanya mashabiki wa Brazil Jumatatu katika mechi dhidi ya Korea Kusini kubeba mabango yenye picha za mkongwe huyo na kuandika maneno ya faraja.

Hata wachezaji wa Brazil ambao waliibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya Korea Kusini baada ya mchezo walikusanyika na kufungua bango lenye picha ya gwiji huyo ambaye aliweza kuisaidia nchi yake kutwaa Kombe la Dunia mara tatu.

Vitendo hivi ilikuwa ni vya kiungwana sana kwani huleta faraja na kurudisha matumaini kwa mgonjwa ambaye yuko katika wakati mgumu kiafya. Inawezekana Pele asiweze kusikia, kuona au kujitambua lakini mwili wa binadamu ni sawa na mashine ya kustaajabisha, matibabu na madawa yanaweza kushindwa kumpa nafuu lakini faraja ikaweza.

Siyo Pele peke yake bali pia watoa huduma ya afya wa idara ya dharula wanaopishana pasipo kuchoka na jamaa wa karibu wa nyota huyo wa zamani ambao wanaweza kuwa katika hali ya hofu nao wanahitaji faraja. Kuwapa moyo watu hawa kwa sasa ndio kila kitu kwa afya ya Pele kwani kutawafanya kupata sura ya matumaini hatimaye mgonjwa anapowaona wakiwa hivyo hupata faraja na kuwa na matumaini makubwa.

Kwa hali aliyonayo sasa Pele kunamfanya kuwa katika hali ya kukata tamaa huku akiwa katika msongo wa mawazo au sonona kitabibu huitwa Depression hali ambayo ilimpata mwaka 2020. Ukiacha matibabu ya hospitalini, ni faraja pekee kutoka kwa watu wa karibu ndiyo inayoweza kumsaidia kuondoa matatizo kama haya ambayo ni ya kiakili zaidi lakini yanaweza kudhoofisha afya kwa haraka.

Jicho la kitabibu linaiona hali ya sasa ya Pele kuwa ni mbaya zaidi kuwahi kutokea, na pia ni matatizo ambayo ni magumu kupona na kuwa na afya timamu kama hapo awali.

Matatizo haya yanatishia moja kwa moja uhai wa mkongwe huyu wa soka ambaye kama angelikuwa timamu asingelikosa kutazama fainali hizi zinazofanyika Qatar.

HAYA YANATISHIA UHAI

Saratani ya utumbo mpana kitabibu hujulikana kama Colon Cancer, huwa inakua taratibu na huweza kubainika tu ikiwa katika hatua za juu.

Dalili ni pamoja na kujisaidia damu au choo chenye damu ambacho huwa cheusi. Mabadiliko yasiyokuwa ya kawaida ya mfumo wa chakula ikiwamo kupata haja mara kwa mara au kujisaidia na kuhisi haja haijaisha, uchovu, kudhoofika na kupungua uzito isivyo kawaida.

Matibabu ya saratani hutegemeana na hatua ya saratani hiyo. Kama ilivyo kwa Pele ambaye amepewa matibabu ya mionzi, ni dhahiri huenda saratani hiyo ipo hatua za mbele zaidi.

Kwa upande wa tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi ambalo kitabibu hujulikana kama Heart Failure ni tatizo ambalo linaweza kuwa sugu au la muda mfupi tu.

Tatizo hili huwa na dalili kama kupumua kwa shida na pumzi kukatika, kuchoka haraka hasa baada ya kutembea kwa muda mfupi, kuhisi kifua kuwa kizito, kukohoa, kuvimba miguu, kifundo na tumbo, kushindwa kulala chali, rangi ya midomo na kucha kubadilika na kukosa usingizi. Matibabu yatategemea na chanzo na madhara ambayo yameletwa na tatizo hili.

Kwa sasa matatizo haya ndiyo yanayotishia uhai wa mwanasoka huyu ambaye historia ya magonjwa yake inasikitisha sana.

HISTORIA YAKE YA KUUMWA

Tangu alipostaafu soka ameshafanyiwa upasuaji mara saba na huku akilazwa mara kwa mara kutokana na kuandamwa na magonjwa nyemelezi ikiwamo homa ya mapafu na uambukizi wa njia ya mkojo.

Mwaka 1970 ulikuwa ni mwaka mgumu kwa nguli huyu hii ni mara baada ya kudondoka vibaya katika mechi na kuvunjika mbavu ambayo ilijeruhi figo yake na madaktari kulazimika kuiondoa.

Hii ndio ajali ambayo ilisababisha gwiji huyu aliyeichezea Klabu ya Santos kuishi na figo moja maisha yake yote yaliyobakia. Majanga ya kuumwa yalimwandama kwani mwaka 2012 alifanyiwa upasuaji wa pili na wa tatu ambao ni upasuaji wa mfupa wa paja na tezi dume.

Mwaka 2015 alifanyiwa upasuaji wa nne wa mgongo hii ni baada ya kubainika chanzo cha maumivu makali aliyokuwa nayo yanasababishwa na pingili ya mgongo illiyohama.

Mwaka huohuo akafanyiwa upasuaji wa tano wa kuondoa vijiwe katika figo ambao nao ukalazimika kurudiwa ikiwa ni upasuaji wa sita mwaka 2016 mara baada ya kupata shambulizi la njia ya mkojo.

Mwaka 2020 alifanyiwa upasuaji wa saba na kuwekewa nyonga bandia. Upasuaji huu ndio ulimfanya tangu kipindi hicho kushindwa kutembea kwa kujitegemea.

Historia hii ya kuandamwa na magonjwa ndiyo kumemfanya kushindwa kutokea hadharani na kuhudhuria tuzo mbalimbali za FIFA tangu mwaka 2018.

KWANINI BADO ANADUNDA?

Uwekezaji aliofanya kupitia kipaji chake cha soka ulimfanya kuwa tajiri, hivyo kumudu gharama kubwa za matibabu na kulinda utimamu wa afya kwa pesa nyingi.

Ingawa umri alionao Pele hivi sasa unaweza kuwa kikwazo kupata matibabu haya kwani moja ya hatari ya kupata matatizo hayo ni kuwa na umri zaidi ya 50.

Ni kweli Pele anaumwa sana lakini faraja zinazomiminika kwa wadau wa soka duniani ni jambo zuri kwani ni sehemu ya tiba kwa wagonjwa wa hali kama yake.

Tuendelea kuburudika na hatua ya robo fainali Kombe la Dunia 2022 Qatar huku pia tukimwombea na kumtakia heri gwiji huyu aliyechaguliwa mwanamichezo bora wa karne ili apone haraka.

Columnist: Mwanaspoti