Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Ni upimaji afya tu kwa kwenda mbele

Dokta Pic SPOTI DOKTA: Ni upimaji afya tu kwa kwenda mbele

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi sasa kila kukicha ni habari za mitandaoni za hivi punde. Mara staa fulani anatua klabu ile, mara paap habari hiyohiyo inakanushwa kuwa staa huyo bado hajasaini mkataba.

Naam! Ndio soka la kisasa lilivyo. Limejaa habari za kweli na za upotoshaji. Kipindi hiki klabu zote ziko katika kusaka wanasoka ambao ndio mtaji wa mafaniko katika msimu ujao wa 2023/2024.

Hapa Bongo katika timu za Simba na Yanga tumeshuhudia wachezaji kadhaa wakipewa mkono wa kwaheri, huku wengine wapya wakitambulishwa kama usajili mpya wa msimu ujao. Kule kimataifa habari kubwa ya usajili ni ile inayomhusu nguli wa soka duniani wa kizazi hiki, Lionel Messi ambaye amesajiliwa na Inter Miami ya Marekani kwa mkataba wenye thamani ya kitita cha Dola 50 milioni kwa mwaka.

Unaambiwa Tangazo la utambulisho wa nguli huyu katika klabu hiyo ni moja ya utambulisho bora kuwahi kutokea katika medani ya soka.

Ukiona kipindi hiki hii tambulisha tambulisha ya wachezaji wapya waliosajiliwa huwa jua kuwa ni upimaji wa Afya kwa kwenda mbele kwa lengo la kujiridhisha utimamu wa wachezaji hao kabla ya kuwasainisha. Afya bora ndio mtaji wa mwanasoka wa soka la kulipwa kwani unapomuona katambulishwa hadharani jua kwamba kila kitu kimeiva.

Kwa kawaida kipindi hiki wachezaji wapya wanaponunuliwa katika klabu ni lazima wafaulu vipimo vya afya ili waweze kununuliwa. Mfano ni klabu kubwa za Ulaya ikiwamo Barcelona, Real Madrid, Manchester City na Manchester United wiki hizi ni kupimana afya kwa kwenda mbele kwa mastaa wapya na wale wa zamani.

SABABU ZA UPIMAJI AFYA

Mchakato wa upimaji wa afya kwa wachezaji wa soka ni maelekezo ya miongozo ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) likitambua vyema kuwa utimamu wa afya ya mchezaji ndio mtaji wake. Klabu za soka duniani hasa soka la kulipwa zinashikamana na miongozo hiyo ya Fifa, ndio maana unaona kwa sasa ni upimaji afya kwa kwenda mbele katika klabu mbalimbali.

Upimaji ndio unasaidia kujua ustahimilivu wa mwili wa mwanasoka kwani endapo atakua dhaifu huenda hayupo sawa kiafya ikiwamo kuwa na majeraha ya mara kwa mara au kuwa mgonjwa.

Upimaji ndio unaobaini uwepo wa majeraha ya ndani ya misuli na maungio ambayo kwa ndio yanaweza kuwa kikwazo kwa mchezaji kuweza kuwa na kasi, nguvu na kucheza kwa stamina. Vilevile upimaji hubaini uwepo wa matatizo makubwa ya kiafya ikiwamo magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na matatizo ya mfumo wa hewa.

Mchakato huu ni moja ya nyenzo ambayo inaweza kubaini udanganyifu wa umri wa mchezaji. Kwa wale waliosajili wachezaji kinda huitaji kutathimini umri wa mchezaji kwa kutumia njia za kitabibu ikiwamo inayojumuisha picha ya kiganja ya MRI.

Uchunguzi huweza kubaini uwapo wa majeraha ya mara kwa mara yasiyopona, hivyo kumpunguzia ufanisi na kiwango mchezaji. Ugunduzi wa hili unasaidia kumpa ushauri na matibabu ya majeraha yake.

Uchunguzi wa kiafya ndio huweza kubaini wachezaji kama ana uzito mkubwa au uzito na uimara wa misuli unapungua katika eneo flani mwili.

Matizo kama hayo yakibainika hupewa msaada wa ushauri ikiwamo mazoezi ya ‘gym’yakujenga mwili kwa wale ambao misuli imekuwa dhaifu huweza kupewa mazoezi maalum. Kwa wale wenye uzito mkubwa huweza kupewa ushauri namna ya kudhibitii uzito wa mwili ikiwamo kushauri kuacha kula vyakula vya mafuta mengi, wanga na sukari kwa wingi.

Uchunguzi huu huweza pia kubaini kasoro za kimaumbile ya mwilini ambazo zinaweza kumfanya mwanamichezo huyo kuwa wa kiwango wa kimataifa.

Wataalam wa afya huwa na uwezo wakugundua matatizo ya kisaikolojia na kitabia kwa wachezaji ikiwamo ulevi ulipindukia, uvutaji sigara na mifarakano ya kifamilia.

Hivyo wanapogundua hili huweza kuchukua hatua ikiwamo kuwapa tiba ya kurekebisha tabia hizo. Uchunguzi wa kiafya hubaini mchoko au uchovu mkali hasa baada ya mwanamichezo kutumika kupita kiasi katika mashindano zaidi ya moja.

MCHAKATO ULIVYO

Kwa kawaida uchunguzi hufanyika katika vituo maalumu vya kisasa vyenye vifaa vya kisasa na unaweza kuchukua saa 12-24 iwapo taratibu zitafuatwa. Uchunguzi huo hutegemeana na umri, afya kwa ujumla na historia ya familia, mienendo na mitindo ya maisha ikiwamo kama mwanamichezo anatumia tumbaku au kilevi chochote.

Uchunguzi hujikita kuangalia zaidi matatizo ya mfumo wa moyo na mzunguko wa damu, mfumo wa upumuaji, fahamu, mifupa na misuli na mingineyo.

Uchunguzi unaweza ukaanzia katika historia ya mwanamichezo kama ana dalili zozote au historia ya magonjwa sugu au ya kurithi katika familia yake.

Vile vile uchunguzi wa kimwili ikiwamo upimaji wa shinikizo la damu, kasi ya upumuaji, joto la mwili na unepaji wa kuta za mshipa wa damu.

Vipimo vya uzito, urefu, na upimaji wa ukubwa wa misuli mikubwa ya mwili pia hufanywa kubaini uzito mkubwa au mdogo.

Vipimo vya kisasa huweza kutumika kuweza kubaini matatizo ya kiafya ya tishu laini na tishu ngumu yaliyojikita kwa ndani kwa kutumia vipimo vya picha za CT na MRI.

Kwa upande wa uchunguzi wa mwili unaweza ukahusisha maabara na vipimo vya picha. Vipimo kama vya wingi wa damu na kundi lake, kipimo cha picha nzima ya damu, kiwango cha sukari ya mwili, vipimo vya maambukizi ya magonjwa ya kujamiana, VVU na homa ya ini. Vilevile uchunguzi wa picha za mwili ikiwamo ile ya kifua ya xray, vipimo vya uchunguzi wa moyo ikiwamo kile cha picha ya moyo na cha kuona ufanyaji kazi wa moyo.

Fifa iliamua kuweka mwongozo wa uchunguzi wa afya wa kina wa moyo hasa baada ya matukio ya wanasoka kuanguka na kufariki dunia viwanjani. Majaribio mbalimbali ambayo hufanyika katika maabara maalumu ambazo huwa na mashine za kukimbilia hubaini kasi ya mwanamichezo kama anakidhi kasi inayotakiwa.

Vilevile hufanyiwa majaribio ya mazoezi ya viungo kuona uimara wa mwili kiujumla, majaribio kuona uwezo wake wakuona, kutumia akili na kufanya maamuzi. Matokeo ya upimaji afya huweza kutathiminiwa na wataalam wa afya za michezo na kisha hutoa matokeo ya ujumla kama mchezaji ni timamu kiafya kucheza soka.

CHUKU HII

Unapoona hivi sasa ni upimaji afya kwa kwenda mbele tambua kuwa hayo ni maendeleo makubwa katika soka na idara za afya. Afya ni mtaji, klabu za hapa bongo zitumie miongozo hiyo kupima wachezaji.

Columnist: Mwanaspoti