Kiungo wa Manchester City, Kelvin De Bruyne ‘KDB’ huenda akawa nje ya uwanja kwa miezi mitatu au minne kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja aliyoyapata katika mchezo uliofanyika Ijumaa iliyopita.
Kiungo huyo tegemeo katika klabu hiyo alipatwa na majeraha hayo katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Burnley ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kulazimika kutolewa dakika ya 28. Itakumbukwa makala ya wiki iliyopita nililitaja jeraha la misuli ya paja ni moja ya majeraha ambayo yanatarajiwa kuwapata wanasoka wa ligi kama ya EPL.
Majeraha ya misuli ya nyuma ya paja aliyoyapata De Bruyne mwenye umri wa miaka 32 yamekuwa yakijirudia mara kwa mara sio tu msimu huu, bali hata misimu iliyopita alikuwa akipata aina hii ya majeraha.
Kwa mujibu wa Kocha Pep Gurdiola jeraha alilopata ni kubwa na huenda likahitaji kufanyiwa upasuaji kukarabati tishu za misuli hizo.
Majeraha haya ndio yalichangia kukosekana katika mchezo wa jana wa fainali ya Super Cup dhidi ya Sevilla ya Hispania. Aina hii ya majeraha ya misuli ya paja inawezekana ikawa ni mchaniko bunda la misuli au nyuzi ngumu za tendoni ambazo ndizo zinajipachika katika mifupa.
Na kama ni jeraha kubwa ina maana ni jeraha la misuli daraja la tatu ambayo huenda ni mchaniko wa misuli hii na kuachana pande mbili au zikashikana lakini ikiwa na mchaniko mkubwa.
Vilevile linaweza kuwa ni mvutiko uliopitiliza wa nyuzi ngumu za tendoni ambazo huwa ndizo mkia wa msuli unaojipachika katika mfupa. Nyuzi hizi zinaweza kuchomoka kutoka katika mfupa au kuchanika ama kukatika pande mbili.
Misuli hii inapata majeraha yanayojulikana kitabibu kama ‘strain’. Ni hali ya misuli kuvutika kupita kiwango au kupata shinikizo kubwa ama kujijeruhi kutokana na mijongeo hasi ya mwili. Haishangazi kwa De Bruyne kupata majeraha haya na hii ni kutokana na nafasi anayocheza eneo la katikati na kushambulia hali inayomfanya kukimbia sana, kupiga mashuti, kukumbana kimwili na wapinzani.
Vilevile eneo hili ndilo ambalo linamfanya mchezaji kukaba sana huku pia akishambulia kwa kasi na kutumia nguvu nyingi kucheza, hivyo kuwa katika hatari ya kupata majeraha haya.
MISULI NYUMA YA PAJA
Misuli ya nyuma ya paja inaundwa na misuli mikubwa mitatu ambayo ndio yenye kazi ya kulikunja goti na kulinyoosha, hivyo kuwezesha matendo kama vile kutembea, kukimbia, kuruka na kupanda.
Vilevile misuli hii ndio inamwezesha mchezaji kupiga mpira, kunyoosha paja, kupiga mpira na kukaba. Misuli hii inapojeruhiwa na kupata majeraha ya kawaida huchukua wiki sita kupona kabisa, ingawa kupona pia hutegemea na ukubwa wa jeraha na programu ya matibabu. Misuli hii iliyopo nyuma ya paja inaweza kujeruhiwa katika nyuzi mvutiko zilizo kama bunda na pia miishilio yake yaani nyuzi ngumu za tendoni.
HATUA ZA MATIBABU AWALI
Pale mchezaji anapopata majeraha ya misuli hii huhitajika kupewa huduma za awali kabla ya kwenda katika huduma za juu za matibabu za juu.
1. Kupumzika
Mchezaji atahitaji kutofanya shughuli zozote za kuushughulisha mwili zinazoweza kumletea maumivu ikiwamo kutembea au kukimbia. Hii inasaidia kupunguza hatari ya kuongeza ukubwa wa jeraha na kupata maumivu zaidi.
2. Barafu
Barafu iliyoviringishwa katika nailoni huwekwa nyuma ya paja katika misuli dakika 15-20 mara 2-3 kwa siku ili kupunguza maumivu.
3. bandeji mvutiko
Kufunga bandeji mvutiko au kifaa tiba cha kubana paja inasaidia kupunguza kuvimba na maumivu. Bandeji haitakiwi kubana sana wala kuwa legelege.
4. Kunyanyua mguu
Itahitajika mguu kunyanyuliwa kuzidi kifua wakati mtu akiwa amelala chali. Hii inasaidia damu chafu kushuka kirahisi na pia kupunguza uvimbe na maumivu.
Hatua hizi ni muhimu katika huduma ya matibabu ya awali wakati mchezaji akiandaliwa kwenda katika matibabu ya juu hospitalini au vituo maalumu vya matibabu ya majeraha ya michezo.
VINAVYOCHELEWA KUPONA
Kama ilivyo kwa De Bruyne majeraha haya ni yakujirudia rudia. Yanawapata zaidi wachezaji wale wanaotumika sana mara kwa mara kwa muda mrefu.
Ni kawaida majeraha kuchelewa kupona kutokana na mkao wa misuli yenyewe na maungio ya eneo hilo. Ila kuna mambo mengine yafuatayo yanayochelewesha kupona:
1. Udhaifu wa aina ya mazoezi au mafunzo anayopewa mchezaji na wakufunzi wa benchi la ufundi.
2. Kupewa mzigo mdogo sana au mkubwa zaidi wakati wa mazoezi tiba.
3. Eneo la chini ya mgongo linaweza kutuma maumivu chini ya misuli ya nyuma ya paja.
4. Mivunjiko shinikizo katika mifupa ya eneo hilo inaweza kuchangia kuwa na maumivu.
5. Maumivu yaliyotokana na shambulizi la nyuzi za tendoni za misuli ya makalio yanaweza kuchangia kupata maumivu zaidi katika misuli ya nyuma ya paja.
MATIBABU
Kipimo muhimu kinachofanyika kutazama ukubwa wa majeraha ya tishu laini ni kile cha MRI. Kipimo hiki kinaonyesha picha nzuri ya hali ya tishu. Matibabu yanategemeana na daraja la jeraha, mara nyingi daraja la tatu huwa ni upasuaji.
Tayari Guardiola imeelezwa kawasiliana na daktari anayemwamini ambaye ni nguli wa upasuaji wa majeraha ya michezo, Ramon Cugat.
Picha za MRI alizopigwa De Bruyne zimeshaonwa na Dk Cugat na ametoa ushauri wa matibabu.
Nguli huyu ndiye mara nyingi hutibu majeraha ya mastaa wa Ulaya ikiwamo Zlatan Ibrahimovich, Robert Lewandowsk na Leroy Sane.
CHUKUA HII
Ili kupunguza hatari ya majeraha ya nyuma ya misuli ya paja mchezaji anatakiwa kunyoosha viungo na kupasha mwili dakika 5-10 kabla ya kuingia, baada ya mechi au mazoezi.