Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Kilichomkosesha Ronaldo derby ni hiki

Cr Ronaldo Cristiano Ronaldo

Fri, 11 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Uamuzi wa Kocha Ralf Rangnick kutomjumuisha Cristiano Ronaldo katika mchezo wa Manchester Derby uliochezwa Jumapili uliwastua wengi ikiwamo wachezaji na mashabiki wa klabu hiyo.

Si unawajua tena mashabiki kindakindaki wa klabu hiyo wasipomwona Ronaldo tu katika mechi zao tayari wanakuwa na maswali lukuki kila kona mitandaoni!

Maswali hayo yalikuja mara baada ya supastaa huyo kuondoka kwenda nchini kwao Ureno wakati timu yake ya Man United ikikabiliwa na mechi ya derby dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja wa Etihad.

Kuhojihoji kuliongezeka baada ya miamba hiyo ya soka England kukumbana na kupigo cha kudhalilishwa cha mabao 4-1 katika mchezo wa EPL uliochezwa nyumbani kwa Man City siku ya Jumapili.

Katika taarifa fupi aliyotoa kocha Rangnick alithibitisha kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 37 ana majeraha ya misuli ya paja yajulikanayo kitabibu kama Hip flexors Muscles na si vinginevyo.

Ila bado kukawa na tuhuma kuwa Ronaldo alikuwa si majeruhi kama ilivyoelezwa na kocha huyo.

Alifafanua kuwa mchezaji huyo amepata tatizo la majeraha ya misuli jeraha ambalo liliwahi pia kumpata mwezi Januari mwaka huu na kumfanya kukosa mechi mbili.

Kocha huyo alimaliza ubishi ulioonekana katika kuta za mitandao ya kijamii kwa kueleza wazi kuwa nyota huyo hana tatizo naye isipokuwa anazingatia ushauri wa wataalam wa Afya.

Katika taarifa yake Ronaldo ameeleza kuwa aliondoka jijini London London kwenda Ureno kwa ajili ya matibabu na uuguzi wa majeraha ya misuli hiyo.

Hivyo uvumi uliovuma kuwa hakupa-ngwa kwa makusudi hazina ukweli wowote.

Jicho la tatu la Spoti Dokta linaona kuwa si jambo la kushangaza kwa mchezaji kama Ronaldo kupata aina hiyo ya majeraha kwani moja ya kihatarishi ni pamoja kucheza mchezo wa soka.

Ligi anayochezea na nafasi ya ushambuliaji anayocheza Ronaldo inamweka katika hatari ya kupata majeraha haya.

Mchezaji huyu kutokana na ubora wake anajikuta anatumika sana mara mara hali inayomfanya kukutana na faulu au kujijeruhi au kukumbana kimwili.

Vile vile kwa mchezaji anayependa kupiga mashuti makali ikiwamo Ronaldo wako katika hatari ya kupata majeraha ya misuli ya paja ya mbele yaani hip flexors Muscles.

Majeraha hayo yako hivi

Misuli ya Flexor iko mbele eno la juu ya paja ikiwa na kazi ya kusaidia mwili kutembea, kujipinda na kuleta goti kifuani.

Misuli hii inaweza kujeruhiwa kwa kuvutwa sana, kuchanika wastani na kuchanika pande mbili au muishilio wa msuli yaani tendoni kuchanika au kuchomoka katika mfupa.

Kwa asilimia kubwa ya wanasoka wanaonekana kupata majeraha ya misuli ya paja ambayo iko ya mbele na ya nyuma kutoka na mchezo wa soka kuhusisha zaidi miguu.

Tatizo la kuchanika misuli ya paja ni moja ya majeraha yanayoongoza kuwapata wachezaji wa soka hasa wale wanaocheza ligi za kulipwa zenye ushindani mkubwa.

Tatizo hili mara nyingi huwa si mpaka mchezaji achezewe faulo bali mwenyewe akiwa katika kasi hujikuta akipata maumivu ya kuchomwa kama na kitu chenye ncha kali nyuma ya paja.

Si jambo la kushangaza kwa wachezaji wa mpira wa miguu kupata tatizo hili mara kwa mara kwani wao wanatumia zaidi miguu kucheza ikiwamo kupiga mashuti, kukimbia, kuruka, kukwatuliwa na kukwatua.

Mambo haya yote yanafanyika katika eneo la miguuni na nguvu kubwa inatoka katika misuli iliyopo eneo hili ikiwamo misuli ya paja.

Misuli inapotumika sana au kuzidiwa uwezo wake huweza kupata mchoko mkali na kuwa dhaifu.

Wakati wa kucheza nako kuna kuchezewa faulo ambazo mara nyingi husababisha majeraha madogo mpaka makubwa. Wachezaji wa soka wanakumbana na faulo nyingi hasa kwa viungo na washambuliaji.

Mambo yote haya huweza kuchangia kujijeruhi ndani kwa ndani kwa misuli na kurundika vijeraha vidogo vidogo na kuifanya misuli hii kuwa dhaifu.

Baadaye ghafla unapotumia nguvu kupita kiasi ikiwamo kutaka kuchomoka kasi, misuli hii hupata shinikizo kubwa na huweza kusababisha kuchanika misuli hii.

Nyuzinyuzi ndogo za misuli zilizo kama raba band huweza kukunjuka kupita kiwango chake hivyo kukatika.

Wakati misuli hii ikifanya kazi hii hujikuta ikielemewa na uzito wote wa mwili, wakati huo huo huwa na kazi ya kujirefusha na kujifupisha ili kwenda kasi na hapo ndipo pia misuli hupata madhara.

Yapo mambo mbalimbali yanayoweza kumweka mwanamichezo katika hatari ya kupata tatizo la kuchanika misuli ya paja.

Misuli iliyojibana iko katika hatari ya kupata tatizo hili, hii inawakumba wanamichezo wasiopasha kabla ya mazoezi au mechi.

Kama misuli hii kiasili itakuwa ni dhaifu basi nayo inakuwa haina uwezo wa kuhimili mazoezi magumu hivyo inakuwa rahisi kujeruhi.

Uwepo wa mchoko hupunguza uwezo wa misuli kupata nishati na kuwa na nguvu hivyo nayo hukuweka katika hatari ya majeraha.

Wanamichezo ambao bado wanaendelea kukua kimwili wako katika hatari ya kuchanika kwa misuli kwani misuli yao na mifupa haikui katika uwiano sawa kwa muda na kasi.

Dalili ya mara kwa mara ni pamoja na mwanamichezo kujigundua kuwa na maumivu makali yanayochoma na kuuma nyuma ya paja hasa baada ya kuchomoka kwa kasi.

Hii itamfanya kusimama haraka na akiegemea mguu ulio mzima kiafya huku akishika nyuma ya paja baadaye maumivu yakizidi hukaa chini.

Yanapunguzwa kwa kufanya hivi

Ili kupunguza majeraha haya ya misuli ya paja ni vizuri wanasoka kuzingatia mazoezi mepesi ya viungo ikiwamo ya kunyoosha viungo vya mwili na kupasha moto mwili kabla na baada ya kushiriki michezo.

Usingaji (massage) wa misuli ya mapaja baada ya mechi au mazoezi magumu ni moja ya njia ambayo inatumiwa sana na wanasoka wa kimataifa kukabiliana na majeraha ya misuli.

Matumizi ya protini ya ziada na ulaji wa vyakula vyenye protini ni moja ya njia rahisi ili kukabiliana na majeraha ya misuli kwa wanamichezo.

Ukiacha ulaji protini, wachezaji wanatakiwa kunywa maji mengi angalau lita 2-3 kabla na baada ya mechi au mazoezi.

Wachezaji wanatakiwa kuepuka kucheza wakiwa wana mejaraha au kabla ya kupona vizuri. Tathmini ya kina ya kitabibu inahitajika kwa ajili wachezaji wanaopona baada ya kuwa majeruhi. Benchi la ufundi linatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz