Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Joto kali ni tishio kubwa kwa wachezaji

Joto Kali Vvv Joto kali ni tishio kubwa kwa wachezaji

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara kuna baadhi ya mechi zinachezwa kuanzia Saa 8 mchana, wakati mwingine jua likiwa la utosini.

Klabu zimewahi kulalamika juu ya mechi hizo kupigwa muda huo, hasa zikizihusisha zaidi timu ndogo, huku vigogo Simba na Yanga zikipangwa mechi zao kupigwa kuanzia jioni na mara nyingi usiku hasa zinapokuwa nyumbani, kipindi ambacho hali ya hewa huwa imetulia na joto kupungua.

Hata hivyo, Bodi ya Ligi (TPLB) imeshatoa ufafanuzi juu ya mechi hizo kwa nini zinapigwa muda huo kwa kueleza inatokana na matakwa ya ratiba kutoka kwa wadhamini wa matangazo ya ligi hiyo ambao mechi zote kwa siku ni lazima zionyeshwe kwenye runinga.

Pamoja na changamoto hizo za ratiba na kulazimisha mechi kupigwa mchana wa jua kali hasa kipindi cha joto huwa ni hatari zaidi kwa wachezaji.

Nani hajui ikiwa ni mchana ukiwa katikati ya jiji la Dar es Salaam na joto liko juu ukiwa katika msongamano pengine unatembea tu unajikuta ukitokwa jasho jingi na baadaye kukupa kiu kali ya maji. Kumbuka hapo unatembea tu unapata hali hiyo, jaribu kujilinganisha na mchezaji anayeshiriki ligi zenye ushindani au kucheza mchezo wenye ushindani nyakati za alasiri katika hali ya hewa ya sasa maeneo ya pwani atakuwa ana hali gani.

Ushiriki wa michezo kama vile Ligi Kuu Bara au mechi za kimataifa zinazochezwa jijini humo au kufanya mazoezi katika maeneo ambayo kwa sasa yana hali ya joto kali kunaweza kumuweka mchezaji katika hatari kiafya. Sababu kubwa ya hatari hiyo ni kutokana na mwili kupoteza maji na chumvi au madini mwilini kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida.

Endapo upotevu wa maji mwilini hautadhibitiwa ndivyo hatari ya athari hizo zinavyokuwa juu na pia kadri hali ya hewa ya joto inapozidi kuwa juu na ndivyo maji hupotea zaidi mwilini. Maeneo ya ukanda wa pwani ambayo sasa yanaonyesha kuwa na joto kali ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Unguja, Pemba, Mtwara na Lindi na Kanda ya Kaskazini ikiwamo Kilimajaro.

Joto hili katika mikoa hii ya Pwani na jirani yake ni tishio kwa wachezaji wa soka ambao mchezo huo unaohusisha kasi na nguvu. Ni vyema kujua athari au madhara yanayoweza kuwapata wachezaji wanaocheza katika mikoa yenye joto kali.

Iko hivi

Upungufu wa maji mwilini ni jambo ambalo linaweza kujitokeza kipindi cha joto kali na huku ikiwa hewa ni kavu isiyo na unyevu. Kwa kawaida mwili huhitaji maji na chumvichumvi kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi seli mbalimbali.

Wachezaji wanapokuwa katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali au kucheza mechi zenye ushindani hutokwa na jasho, hivyo hupoteza maji mengi na chumvi mwilini. Ikumbukwe kuwa kadri joto linavyozidi kuwa kali ndivyo mwili unavyotoa jasho zaidi, lengo ni kupunguza joto la ndani ya mwili lisizidi kiwango chake cha mwisho.

Kuvuja jasho sana huwa ni zaidi wakati wa kucheza katika joto kali na wakati huohuo kadri jasho linavyotoka kwa wingi na ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo tu mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kuvuja jasho.

Tatizo kiafya

Hali hii inaweza kuambatana na madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo kuuma na kubana kwa makundi ya misuli ikiwamo ile ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji kama wa soka.

Upungufu wa maji na chumvi mwilini usipokabiliwa kwa kuupoza mwili na kurudishia kiwango cha maji kilichopungua unaweza kuleta madhara makubwa kiafya.

Matatizo hayo ni pamoja na kupata mchoko mkali na kiharusi kitokanacho na joto kali pamoja na kupoteza fahamu. mMambo haya yanaweza hata kusababisha kifo kwa mchezaji. Madhara mengine yanayoweza kutokana na hali ya kutokwa sana na jasho na kupungiwa maji mwilini ni pamoja na kichwa kuuma, kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini mazoezini au mchezoni, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma na mwili kuuma.

Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango bora au akacheza lakini akachoka mapema. Hali hii ikiwatokea wachezaji wanaweza kudhaniwa kuwa wanafanya makusudi au kwa mazingira yetu ikadhaniwa wamehongwa kumbe wana upungufu wa maji miilini kutokana na kutoka jasho jingi.

Mara nyingi wachezaji ambao wanapata madhara haya kirahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha kabla ya mechi na vilevile kutokula vyakula vyenye maji na madini ikiwamo matunda na mboga.

Nini kifanyike

Wachezaji wanywe maji mengi siku mbili kabla ya mechi ikiwezekana lita 3-5 za maji kwa siku. Unywaji maji uwe ni utamaduni wa wakati wote kwa wachezaji na sio wakati wa joto pekee. Kwa watu wa kawaida glasi 8-10 kwa siku zinatosha kukabiliana na upungufu wa maji mwilini kipindi cha joto kali.

Usisubiri kiu ikubane ndipo unywe maji na yanywewe mara kwa mara au kunywa kidogo mpaka ufikie lengo linalotakiwa. Vilevile kula matunda kwa wingi kila baada ya mechi na katika mlo tumia mbogamboga kwa wingi. Matunda na mboga huwa na maji mengi na madini (chumvichumvi).

Ni muhimu mchezaji akatambua umuhimu wa kunywa maji ya kutosha kabla ya kuingia mazoezini au katika mechi na vilevile kunywa maji kila baada ya nusu saa au wakati wa mapumziko na baada ya kumaliza mazoezi au mechi. Sio vibaya kwa klabu zenye uwezo kutumia vinywaji maalumu kwa ajili ya wanamichezo ambapo ndani yake huwa na wanga na chumvichumvi. Vinywaji hivi kama vinavyojulikana sports drinks ni muhimu kutumia.

Kwa faida ya wote, vinywaji vya kuongeza nguvu na kusisimua au kuchangamsha mwili maarufu kama energy drinks sio sahihi kutumia kwa mtu kuongeza maji mwilini. Pia pombe, soda na kahawa sio mbadala wa maji yaliyopotea kwa njia ya jasho.

Kipindi hiki wachezaji waepuke kukaa au kutembelea maeneo yenye joto na msongamano, badala yake wakae maeneo ya wazi yenye vivuli hasa kabla ya mechi. Ni muhimu kuupumzisha mwili kwa kulala angalau saa nane kwa siku.

Kama joto litakuwa ni kali sana ni vizuri kucheza wakati wa joto au jua kali linapokuwa limepungua kuaepushia wachezaji matatizo.

Ni vizuri kutoa mapumziko ya katikati ya mechi ili kutoa nafasi kwa wachezaji kunywa kiasi kidogo cha maji ili kukabiliana na hali hiyo. Joto hili ni tishio kwa wachezaji, ni vizuri watoe taarifa mapema kwa madaktari wa timu mara tu wanapopata dalili na viashiria vya madhara ya joto.

Columnist: Mwanaspoti