Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Jeraha alilopata Neymar hili hapa

Neymar Pic Data Neymar akiugulia maumivu

Fri, 3 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mshambuliaji wa PSG ya Ufaransa, Mbrazil Neymar alipata majeraha mabaya ya kifundo cha mguu Jumapili katika mchezo wa ligi dhidi ya Saint Etienne.

Alipata jeraha hilo katika kifundo cha mguu wa kushoto dakika za mwisho za kipindi cha pili baada ya kuchewa faulu iliyokipindisha vibaya kifundo cha mguu.

Awali alidhaniwa huenda ikawa amepata mvunjiko wa mifupa ya kifundo lakini taarifa iliyotolewa hapo juzi na klabu hiyo umesema amepata majeraha ya nyuzi ngumu za ligamenti za kifundo. Imeelezwa vipimo vilivyofanyika vya picha za MRI ndizo zilizobaini kujeruhiwa kwa nyuzi hizo ambazo kazi yake ni kuunganisha mfupa mmoja na mwingine.

Jeraha hilo kitabibu hujulikana kama third degree ligament tear ni moja ya majeraha yanayotokea mara kwa mara katika eneo hilo. Katika kifundo nyuzi hizo zipo nyingi zikishika vifupa vya kifundo ikiwamo vifupa vidogo vidogo vilivyopo katika funiko la kifundo cha mguu.

Taarifa za klabu hiyo imeeleza jeraha hili litamweka nje kwa wiki 6-8, hii itamfanya kukosa mechi kadhaa katika kikosi hicho kinachofundishwa na Mauricio Pottechino.

Staa huyu (29) kwa dakika kadhaa alionekana kugaragara huku akishika kifundo na kupiga kelele hali iliyoashiria alikuwa katika maumivu makali yasiyo ya kawaida.

Kundi la watoa huduma ya kwanza pamoja na madaktari watimu waliona ishara ya mchezaji huyo kuashiria amepata jeraha baya.

Alipewa huduma kwa dakika kadhaa uwanjani na kisha baadaye alitolewa nje ya uwanja kwa machela. Alionekana akitolewa huku akilia kutokana na maumivu na huzuni aliyonayo. Ingawa habari njema kwake mpaka sasa ni hakuna mfupa uliovunjika ila kutokana na ukubwa wa jeraha hilo huenda upasuaji ukahitajika.

Jeraha hili liko hivi

Jeraha alilopata linahusisha majeraha makubwa yaani kujeruhiwa kwa tishu laini za kifundo cha miguu. Aina hii ya jeraha huenda likahitaji upasuaji ili kukarabati ligamenti hiyo iliyokatika au kuchanika.

Ingawa si tu ni ligamenti iliyojeruhiwa bali pia tishu laini zilizopo katika kifundo cha mguu ikiwamo nyuzi za miishulio ya misuli zinazounganisha msuli katika mfupa yaani Tendoni.

Vile vile mishipa ya damu na fahamu pamoja na tishu zingine laini zinazounda ungio la kifundo cha mguu.

Faulo hiyo aliyochezewa ilibeba shinikizo kubwa lililotua katika kifundo cha Neymar ambaye hakuwa ametarajia wala mwili wake haukua umejiandaa kujihami na shinikizo kubwa la aina hiyo.

Kawaida kuvunjika huwa ni mfupa kupata nyufa au kumeguka kipande au vipande au kuvunjika na kuachana pande mbili au kuvunjika huku ukiwa umeshikamana.

Wakati kuteguka huwa ni kuhama kwa mfupa au mifupa kutoka katika pango lake unapojizungushia na unaweza mfupa kuhama wote au ukahama kidogo lakini ukaendelea kuwepo katika pango lake.

Katika ungio la kifundo linajumuisha mfupa wa kisigino na mifupa miwili iliyoungana ya mguu. Eneo hili ni moja ya eneo ambalo wachezaji wa mpira wanapata majeraha sana kutokana na eneo hili kufanya mambo mengi wakati wanacheza au kukabwa kwani ni mpira wa miguu.

Kutokana na maumbile ya ungio la kifundo cha mguu kuwa na tishu laini kama vile ligamenti na tendoni pale linapojeruhiwa huweza kusababisha kuchelewa kupona.

Kwa Neymar hakupata mvunjiko wenye jeraha la wazi na wala damu haikuvuja nje ya mwili. Majeraha ya kifundo yanayotokea sana kwa wanasoka hujulikana kama Ankle Strain na Sprain ambayo mengi huwa yanakuwa si katika hali mbaya na hayahusishi kuvunjika bali ni kujeruhiwa kwa nyuzi za ligamenti na tendoni na misuli.

Jeraha la nyuzi ngumu za ligamenti alilopata kitabibu ni ankle sprain, na kamba hii inaweza kuvutika sana, kukatika kwa ligamenti pande mbili au kukwanyuka kutoka katika mfupa.

Nyuzi hizi zinaweza kupata majeraha baada ya kufinywa, kujipinda, kunepa, kuvutika kuliko pitiliza , kukwanyuka, kuchubuka, kuchanika kiasi au kukatika na kuachana pande mbili

Vile vile eneo hili likipatwa na shinikizo kubwa kama vile kugongwa na kitu kizito yanaweza kusababisha kuleta nyufa katika mifupa, kututumka kwa mfupa na kuvunjika vifupa vidogo vya kilindo.

Mara zingine nyuzi hizi za kifundo zinaweza kuvutika sana na kubanwa katikati ya mifupa ya kifundo cha mguu endapo zitapata shinikizo kubwa.

Nyuzi ngumu hizo zimejichimbia katika mifupa ya kifundo cha miguu ijulikanayo kama Talus na Tibia, pale zinapopata majeraha huweza kusababisha maumivu, mlipuko wa kinga ya mwili na kuvimba.

Majeraha haya hulikumba zaidi eneo la mbele la mguu wa chini yaani funiko la mguu ni kujeruhiwa kwa mfupa wa kifundo cha mguu (Talus) au mfupa wa ugoko (Tibia) katika eneo la mpaka katika ya kifundo na mguu wa juu.

Uwepo wa majeraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogo vidogo huweza kuleta majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu na kuleta maumivu makali na kuvimba.

Dalili na viashiria vya majeraha ya kifundo cha mguu ni pamoja na maumivu na kuuma pale panapominywa eneo hilo la kifundo, kupata maumivu pale unapojaribu kukukunja au kunyoosha kifundo.

Kuhisi kupata maumivu eneo la mbele yaani funiko wakati unapopiga mpira au unapokimbia.

Neymar hakuweza kuthubutu kunyanyuka na mguu huo zaidi wakati wote alionekana kugugumia kwa maumivu makali mpaka pale alipotolewa kwa machela.

Wakati wa utomasaji wa kifundo mfupa unaweza kugundua uwapo wa kichuguu katika mfupa wa mguu wa mguu (tibia) au sehemu ya juu ya mfupa wa kifundo (Talus).

Kama ilivyokuwa kwa Neymar ambaye alionekana kupata maumivu makali isivyo kawaida hivyo ilikuwa ni dhahiri kuwa amepata jeraha baya.

Kulia kwake na ishara zingine zilitosha kuwaaamsha madaktari kuwa si hali ya kawaida.

Inashauriwa wachezaji watoe ishara kama alivyofanya Neymar pale anapohisi maumivu makali ya pale anapofanyiwa faulu.

Kwa sasa Neymar anaendelea na uchunguzi zaidi akisubiri matibabu, tusubiri tuone nini kitaendelea katika matibabu yake.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz