Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Fahamu majeraha aliyopata Feitoto

Fei Toto Kiungo wa Yanga, Feisal Salum

Fri, 8 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Leo, Aprili 7 ni siku ya afya duniani. Siku hii ya kimataifa huadhimishwa kila mwaka. Mwaka huu ikiwa na kaulimbiu ya ìsayari yetu afya yetu.” Kwa upande wa kona yetu ya Spoti Dokta tutalipiga jicho tatizo la majeraha ya goti ambayo siku za karibuni limemkuta kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Alipata majeraha ya goti wiki iliyopita wakati akiwa kambini na Taifa Stars ambayo hivi karibuni ilikuwa na mechi za kimataifa dhidi ya Benin na Sudan. Fei Toto alipewa ruhusa kurudi nyumbani kwa ajili ya uuguzi wa jeraha hilo ambalo kwa taarifa iliyotolewa sio yale majeraha makubwa ya goti.

Majeraha ya goti ni tishio kwa wanasoka hasa linapoangukia kuwa la goti daraja la tatu kama alilowahi kupata beki wa Liverpool, Virgil Van Djik ambaye aliukosa msimu mzima wa Ligi Kuu England 2021. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ni kuwa jeraha alilopata litamuweka nje kwa wiki mbili, hii ina maana alikuwa mguu nje mguu ndani katika kikosi cha jana dhidi ya Azam FC.

Fei Toto ni kiungo muhimu kwa klabu na taifa, jeraha alilopata ni katika haraka ya kutimiza majukumu kwa taifa.

MAJERAHA YA GOTI

Mara nyingi majeraha ya ungio la goti ni zile nyuzi ngumu zinazoshikilia mifupa inayounda ungio la goti na kitabibu hujulikana kama ligament. Nyuzi hizi zinaweza kujivuta kuliko pitiliza kuliko kiwango chake cha kawaida kuchanika, kuchanika na kuachiana pande mbili au kuchomoka kutoka katika mfupa na kuondoka na kijipande cha mfupa.

Kwa kawaida kipimo kinachoweza kubaini kujeruhiwa nyuzi hizi ni kwa kufanyiwa kipimo cha CT Scan kinacholeta picha za tishu laini za mwili kwa ufasaha.

GOTI NA KAZI ZAKE

Goti ni moja ya ungio (joint) la mwili na ambalo ni rahisi kupata majeraha, limetengenezwa na sehemu ya chini ya mfupa wa paja ambayo hukutana na kujizungurusha kwa pamoja na muishilio wa mfupa mkubwa wa mguu wa chini.

Katikati ya mifupa miwili kuna kifupa kidogo. Kifupa hicho cha duara hujitelezesha na kushikizwa na nyuzi ngumu kutokea katika mfupa wa paja na wa chini ya goti.

Goti huwa na nyuzi za ligament zinazoshikilia mfupa mmoja kwenda mwingine, ina kazi ya kudhibiti mijongeo ya goti na kuzuia mijongeo isiyohitaji kufanyika na goti. Katikati ya mifupa mikubwa miwili huwa na kijifupa bapa kama plastic kiitwacho meniscus - kazi yake kubwa ni kama ëshock absorberí huwa na kazi ya kufyonza shinikizo la uzito wa mwili na hivyo kupunguza hali ya mifupa kusagika.

Goti lina nyuzi za ligament aina tatu - ipo ligament iitwayo anterior cruciate (ACL) yenye umbile kama X ndio ipo sehemu ya mbele ya goti na pia pembeni mwa goti ipo ligament nyingine iitwayo medial collateral ligament (MCL) ipo kulia na kushoto katika goti moja, huku nyuma ya goti pakiwa na ligament ambayo mara chache hupata majeraha inaitwa posterior cruciate ligament (PCL). Pia, ungio la goti limezungukwa kwa ndani na viji ngozi vyembamba vilivyochanganyika na nyuzi ndogo zingine vikitengeneza pango la goti ndani yake huwa na maji kama ute mzito unaolainisha ungio la goti. Goti lina mijongeo minne - hujikunja mbele na nyuma, kujizungusha kuelekea ndani ya mwili na nje ya mwili.

Hapa tunapata picha kwa mchezo kama wa soka goti linahitaji kufanya mambo yote haya hivyo kuliweka ungio hali kama eneo lililo katika hatari ya kupata majeraha

Wengi wa wanamichezo hupatwa na majeraha ya nyuzi nyuzi za gotini ambazo ni tishu laini. Zipo takriban aina nne za majeraha ya goti matatu ni nyuzi ngumu - ligaments ambazo ni majeraha ya nyuzi za mbele (ACL) na nyuzi za pembeni (MCL) ndizo zinazoongoza kwa kujeruhiwa michezoni na mara chache ligaments za nyuma ya goti (PCL) na aina ya mwisho ni kujeruhiwa kwa tishu ngumu ambazo ni mifupa au katileji.

MATIBABU MAJERAHA YA GOTI

Matibabu ya mwanamichezo huwa na lengo la kumsaidia kupona haraka na kulinda asipatwe na majeraha haya mara kwa mara ili kulinda kipaji na kiwango cha mchezo wake na huhusisha jopo la wataalamu wa afya. Wapo wataalamu wa afya za michezo ambao huona tukio zima la mchezaji alivyoumia na kuanza na matibabu ya msingi palepale uwanjani na baadaye hupewa rufaa kama itahitajika kufanya hivyo kupelekwa kwa wataalamu wa upasuaji wa mifupa. Katika matibabu ya msingi ya majeraha ya kawaida ya goti uwanjani ni kupumzika, barafu, kugandamiza/kuminya na kuunyanyua mguu kidogo kuzidi kifua.

Kwa kawaida majeraha mengi ya goti hutibiwa bila upasuaji, huku mengine yakihitaji upasuaji kurekebisha na kukarabati eneo la goti hasa kwa daraja la tatu. Kuruhusiwa kwa Fei Toto kurudi kujiuguza nyumbani ni sehemu ya matibabu ili kutoa nafasi eneo hilo kupona katika mazingira rafiki. Majeraha ya goti yanapopona mchezaji haingizwi kucheza moja kwa moja uwanjani ni lazima afanyiwe uchunguzi na kupewa majaribio kuona kama amepona.

VITU MUHIMU

Moja ya vitu ambavyo ni rafiki kwa mwili wa binadamu ni mazingira ya jua kwani mwanga wa jua unauwezesha mwili kuweza kuwa na ngozi imara na mifupa imara kutokana na mwili kujitengenezea vitamini D. Miili yetu hutengeneza vitamini D kwa kukaa katika jua dakika 15 kwa siku. Vitamini D inauwezesha mwili kulinda madini ya Kalisiamu na kuzuia mifupa kuwa dhaifu. Jua kwa sasa lipo la kutosha nchini ukilinganisha na maeneo mengi ambayo hakuna hali ya upepo wa bahari unaovuma eneo la nchi kavu lililozingukwa kwa maji.

Unywaji majisafi na salama katika mazingira ya joto unakupa kiu ya maji mengi ukilinganisha na aliyepo katika mazingira ya baridi. Mwili wenye maji mengi hupona kwa wakati. Kupumzika katika mazingira ya kuvutia hasa ya sehemu za fukwe husaidia kupeperusha matatizo ya akili ikiwamo msongo wa mawazo. Pia hali hii inaupa utulivu mwili kuweza kupona haraka jeraha.

Ikumbukwe matatizo ya akili yanachangia kinga ya mwili kushuka na kuwa dhaifu, hivyo ni hasara kwa jeraha kupona. Maeneo mengi ya pwani huwa ya wazi yakiwa na hewa safi ya kutosha jambo ambalo ni faida kwa mwili kwani hupata oksijeni nyingi hatimaye kuchangia jeraha kupona vizuri. Mchezaji akianza kupona na maumivu yakiisha yale mazoezi laini kwa aliyepona anayofanya ni rafiki na ni mepesi yanaweza kufanyika ufukweni mchangani. Aina hii ya mazoezi yanauwezesha mwili kuvuna utimamu pasipo kujijeruhi. Kumbuka sio kila zoezi ni rafiki wakati wa uuguzi wa jeraha.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz