Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SPOTI DOKTA: Fahamu haya kabla ya kutua Qatar

Magonjwa Qatar Fahamu haya kabla ya kutua Qatar

Fri, 18 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Zimebaki siku tatu tu mtanange wa Kombe la Dunia kufunguliwa rasmi nchini Qatar ambapo wenyeji wa mashindano wataminyana na timu ya Taifa ya Ecuador. Mchezo huo wa ufunguzi ni wa kundi A ambao kabla ya kuchezwa utatanguliwa na shamrashamra za kumwaga ikiwamo wanamuziki wa nchini humo na wa kutoka nchi zingine kutumbuiza.

Kwa mara ya kwanza dunia inashuhudia mashindano haya yakifanyika katika majira ya baridi katika nchi ambayo ni moja ya nchi zinazokuwa na hali ya joto kali kipindi cha majira ya joto. Wapo wananchi wa kutoka Afrika mashariki ambao tayari wameshika tiketi zao mkononi wakijiandaa kuelekea nchini Qatar kushuhudia siku 28 za mechi mbalimbali mpaka ile ya fainali. Nchi ya Qatar imejipanga vyema kila idara kuanzia ulinzi na usalama, malazi na makazi, sehemu za burudani na huduma za jamii kama vile vituo vyakutolea matibabu na maeneo ya wazi ya kupumzikia.

Tayari pia kuna miradi kadhaa ya Afya ambayo iko chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wakiwa na kampeni kubwa ya kuhakikisha kuwa watazamaji wote wanakuwa salama kiafya. Mradi huu wa WHO unaitaka jamii ishiriki katika mashindano hayo kuwa na mienendo na mitindo mizuri ya kimaisha ikiwamo kuepuka uvutaji wa tumbaku hadharani. Lakini kabla ya kufika huko kuna mambo ambayo ukiwa kama msafiri kuelekea nchini humo unapaswa kuyazingatiaa kwa lengo la kulinda afya ya mwili na akili.

CHUKUA HAYA

Tayari ilishatangazwa kuwa wasafiri wanaokwenda Qatar yale masharti magumu ya COVID-19 ikiwamo kutoingia nchini humo bila cheti kinachoonyesha umepima na uko salama yamelegezwa. Hivyo msafiri hatazuiwa kuingia nchini humo kwa kukosa cheti. Wamejidhatiti vyema kwa kuweka vituo vya kupima papo hapo katika viwanja vya ndege.

Kwa kawaida wasafiri wengi wanapotoka nchi moja kwenda nchi nyingine ambayo mwili wake haujachangamana na mazingira ni kawaida kukutana na tatizo la kuumwa tumbo na kuhara. Hali hii inajulikana kama food poison. Wanaipata sana wasafiri aidha ni kwa kula vyakula vya hotelini au migahawani. Tatizo hilo linatokea kwa nchi zote iwe ni tajiri au maskini. Taarifa njema ni kuwa ni tatizo ambalo linaweza kudhibitiwa na mtu akapona. Ukweli ni kuwa vijidudu vinavyoshikamana na vyakula aina ya bakteria wa E.Cole ndio mara nyingi wameonekana wakiwasababisha tatizo hili.

Muhimu kwa wasafiri ni kuhakikisha kuwa wanakula katika migahawa rasmi ambayo imezingatia kanuni za afya za uandaaji wa vyakula. Kumbuka vyakula vingi huwa ni vile vilivyotoka katika majokofu.

Habari njema ni kuwa Qatar ni nchi tajiri. Imejipanga katika kila eneo ikiwamo la afya. Wizara ya Afya ina watendaji kila mahali wanaohakikisha wageni wanakula vyakula vilivyoandaliwa kwa kuzingatia kanuni za afya pamoja na kunywa maji safi na salama. Unapokuwa umesafiri kwa saa nyingi katika ndege na kama sio msafiri wa mara kwa mara ni jambo la kawaida kukutana na hali ya kuvimba miguu.

Ni tatizo la kawaida ambalo linatokana na mrundikano wa maji miguuni kutokana na mzunguko wa damu kupata kikwazo kunakotokana na kukaa muda mrefu bila kutembea. Tatizo hilo linawapata zaidi watu wazima, wanene, wenye matatizo ya mishipa ya damu ya veini na wenye magonjwa ya moyo. Hupaswi kuwa na hofu tatizo hili linatoweka mara baada ya kutua na kuanza kutembea tembea huku na kule.

Uchovu wa mwili ni jambo ambalo haliepukiki kwa wale wasafiri wa saa zaidi ya tano. Hali hii inatokana na ukweli kuwa mwili unakuwa umetulia na pia viti vya ndege siyo vinavyonyooka kama vile kitanda. Uchovu kwa msafiri ni hali inayoweza kumpa hofu akidhani pengine ana tatizo kubwa la kiafya. Hoteli mbalimbali za nchini humo tayari zina huduma za usingaji yaani massage kwa ajili ya kukabiliana na hali kama ya uchovu. Ukiacha hoteli za nyota tano ambazo zipo za kila aina tena za kuvutia, lakini pia nchi hiyo imeweka meli kubwa za kisasa ambazo nazo zinatoa huduma za malazi na chakula.

Inaelezwa kuwa watu wenye uhitaji wa tiba ya magonjwa ya akili ikiwamo shinikizo la akili na sonona kitabibu depression sehemu ya kujipa utulivu wa akili ni katika mashindano haya. Maelfu ya watu kutoka Ulaya wanapenda kujipa utulivu wa akili kwa kufanya utalii na wakati huohuo wanajipa tiba ya matatizo ya akili.

Hivyo kwa yule anayekwenda katika mashindano hayo ajue kuwa anakwenda mahala sahihi kutakapoimarisha afya yake ya akili. Yapo maeneo ya wazi ambayo yamepewa ulinzi mkali ambayo watu wanaweza kuyatumia kupumzikia au kufanya mazoezi mepesi. Hii ni habari njema kwani maeneo haya yanaipa utimamu zaidi afya ya mwili na akili.

ZINGATIA HILI

Qatar ni nchi ya Kiislamu na imejikita katika tamaduni za dini ambayo ni moja ya dini zenye wafuasi wengi duniani na tayari imekwishaonya juu ya vitendo vinavyohusiana na mambo yanayokinzana na imani hiyo.

Columnist: Mwanaspoti