Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Ya Kenya, Zimbabwe yaweza kurudi Tanzania

Kenya Pic Ya Kenya, Zimbabwe yaweza kurudi Tanzania

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wiki iliyopita Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilitangaza kuzifungia Kenya na Zimbabwe kushiriki katika mchezo huo kimataifa baada ya serikali za nchi hizo kuingilia masuala ya mpira wa miguu.

Nchini Kenya, serikali imeuondoa uongozi wa kuchaguliwa na kuweka kamati ya muda kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi wa viongozi hao, na umma umekubaliana na kitendo hicho ukisema kwanza hakuna nchi inachopoteza kwa sasa; timu ya taifa haimo mashindanoni hali kadhalika klabu.

Nchini Zimbabwe hali ni kama hiyo. Viongozi wanatuhumiwa kwa ufisadi na unyanyasaji wa kijinsia na hivyo serikali imeona iusafishe mchezo huo. Nilipigiwa simu na redio kadhaa kuomba maoni yangu kuhusu uamuzi huo wa Fifa. Na jibu langu lilikuwa moja tu; hatuna vyombo imara vya soka vinavyoweza kuwawajibisha viongozi wanapokuwa na matatizo au tuhuma za ubadhilifu. Hali hiyo inapotawala, viongozi hujifanyia mambo wapendavyo kwa kuwa chombo pekee kinachoweza kuwawajibisha ni mkutano mkuu ambao idadi ikiwa ndogo kama wa TFF sasa, ni rahisi kucheza nao.

Wale viongozi wa Shirikisho la Soka Kenya (KFF) wamekuwa na tuhuma nyingi na ziliongezeka nguvu baada ya nchi hiyo kurudi kutoka fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika Misri.

Viongozi walichukua fedha serikalini wakidai za kwenda kuihudumia timu kwa ajili ya malazi na mambo mengine wakati ikiwa Misri. Baadaye zikapatikana taarifa timu ilihudumiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa malazi na mambo mengine.

Tangu wakati huo, si mkutano mkuu wa KFF wala chombo kingine chochote kilichohoji tuhuma hizo na viongozi wakaendelea kula bata.

Ilifikia wakati hadi vyombo vya habari vikaanza kuhoji sababu za Fifa au CAF kutoingilia kati na kuwawajibisha viongozi. Na hata fedha za rushwa za Ahmad Ahmad alizotoa kwa marais wa vyama vya soka walioandika barua ya kumuunga mkono katika uchaguzi hata kabla ya uchaguzi kutangazwa, hazikuhojiwa.

Inapofikia hali kama hiyo, ni lazima serikali iingilie kati na kuchukua hatua kwa kuwa wenye chombo hawaoni tatizo fedha zikiliwa ovyo; isitoshe na wao hula sehemu ya fedha hizo dharimu.

Hali ni tofauti kwa Fifa yenyewe kwa kuwa ina kamati ya maadili ambayo imegawanyika mara mbili. Moja ni kwa ajili ya uchunguzi na nyingine ni kwa ajili ya kuendesha mashtaka.

Ile inayofanya uchunguzi ndiyo iliyobaini kuwa rais wa zamani wa shirikisho hilo, Sepp Blatter aliidhinisha malipo ya dola milioni moja kwa rais wa Chama cha Soka Ulaya (Uefa), Michell Platini katika hali ya utata na ndipo aliposhtakiwa na kufungiwa miaka nane kujihusisha na soka. Tuhuma za Blatter zingewasilishwa kwenye mkutano mkuu wa Fifa, angepeta kilaini.

Sisi tuna Kamati ya Maadili lakini huioni ina nguvu hizo. Kila siku inaadhibu watu walio nje ya uongozi wa TFF. Ina maana hakuna kiongozi mwenye tuhuma mbaya? Hakuna mwamuzi mwenye tuhuma mbaya za rushwa? Hakuna kiongozi wa klabu mwenye tuhuma mbaya za rushwa? Hivi ni kweli ni watu tu wan je ndio wanaokosea kila siku?

Tunahitaji ustaarabu wa hali ya juu kufikia kiwango cha Kamati ya Maadili kuitisha shauri linalomuhusu rais wa TFF na kumuhoji kuhusu tuhuma Fulani za uvunjaji wa maadili. Lakini kwa sasa, tusitegemee kitu kama hicho. Labda tunachoweza kukitegemea ni serikali kuingilia kati kutakapozuka tuhuma za rushwa kama ilivyokuwa enzi za utawala uliopita ambao hatimaye uliishia lupango. Haya yanayotokea Zimbabwe na Kenya yalishatokea sana, lakini utawala wa Leodegar Tenga ukaweka misingi ambayo ilizuia serikali kuingilia kati masuala ya soka. Lakini naona dalili za misingi ile kuondolewa, hali inayoweza kusababisha nchi kurudi huko. Nimeona wazee wa Yanga wameanza kumuomba Rais Samia Suluhu aingilie kati, lakini baadhi wamewakejeli. Maumivu ya kichwa huanza taratibu!

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz