Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Waziri Mchengerwa ameanzisha safari ya 2030, twende naye

Mhengerwaaa Waziri Mchengerwa ameanzisha safari ya 2030, twende naye

Tue, 20 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa Mfalme wa Morocco, Mohamed Vll unaona dhahiri nia ya serikali kuendeleza michezo, hasa soka kutokana na uwekezaji mkubwa ambao serikali yake iliuweka.

Ni kwa sababu Mohamed wa Vll ni Mfalme na anachoamua ndio kinachotekelezwa, tofauti na sehemu nyingine ambako demokrasia imetamalaki kiasi cha wananchi, si tu kuwa na sauti kuhoji kila uamuzi, bali wana nguvu na njia nyingi za kuukwamisha.

Nia njema ni dhahiri na ingekuwa vigumu kwa mwananchi mwenye kutaka kutumia haki zake za kidemokrasia kumpinga Mfalme Mohamed Vll kuanza kuwekeza kwenye miundombinu na hatimaye mambo mengine ya msingi ambayo yameifanya Morocco leo kuwa mfano wa kuigwa hapa Afrika na duniani kwa ujumla.

Lakini nia yake iliendana na mipango madhubuti ya shirikisho la soka la Morocco, ambalo rais wake alikuwa na maono na kuyawekea misingi ya utekelezaji kiasi kwamba taifa hilo la Afrika Kaskazini leo linazungumziwa miongoni mwa mataifa manne kwa ubora duniani baada ya kufika nusu fainali na kushindwa na Croatia katika mechi ya mshindi wa tatu.

Hayo yalikuwa ni maono ya mfalme wa Morocco na Rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo ambayo yaligandamanishwa na kuibua mradi ambao leo umelifanya taifa hilo kuwa la kutisha katika soka duniani.

Na tayari Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limeipa uenyeji wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia baada ya mashabiki wake 40,000 kufurika uwanjani kushuhudia mechi ya nusu fainali dhidi ya Ufaransa ikiwa ni sehemu ya mashabiki 80,000.

Ndoto kama ya Mfalme Mohamed Vl wa Morocco pia inaonekana kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mchengerwa.

Mchenegerwa ameshakaririwa au kusikika katika hadhira nyingi akieleza nia ya Tanzania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030 ambazo bila shaka zitafanyika Marekani na Canada.

Amekuwa akieleza mengi kuhusu nia hiyo yake binafsi na ya serikali ya kuiwezesha Tanzania kufuzu kwa mara ya kwanza cheza fainali za Kombe la Dunia.

Ni kitu kizuri kwamba waziri amefikia uamuzi huo kwamba ni lazima tufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030 na hasa katika kipindi hiki ambacho tuna miaka minane ya kujiandaa, yaani tukiandaa kikosi cha wachezaji wenye umri wa miaka 12, maana yake ifikapo mwaka 2030 watakuwa na miaka kati ya 21 na zaidi, umri ambao ni muhimu kwa kushindana.

Nilipomsikiliza wiki iliyopita kuhusu hiyo ndoto yake nikapata wazo zaidi; kwamba anasema watakuwa na kocha ambaye hawatamuingilia na hatazuiwa kuteua wachezaji wa madaraja ya chini. Ni matumaini yangu kuwa Mchengerwa hataishia hapo, bali ataendelea kuweka miongozo ya maandalizi ya Tanzania kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia za 2030 ambazo zitapanua wigo wa idadi ya ushiriki kwa baadhi ya mabara.

Lakini ukimsikiliza kwa utulivu, Mchengerwa unaona kuwa amefanya vizuri kuliondoa basi kuelekea kwenye ndoto yake, inayomnyima haki hata rais kufikiria mara mbili kuhusu uamuzi wowote dhidi ya timu yake kufuzu kucheza fainali hizo katika soka. Ni kweli kwamba hata chama cha nchi hakiwezi kufikia mafanikio hayo kama msingi wake ni mtazamo wa mtu mmoja.

Kuwa na maono hayo ni kitu kizuri, lakini kuendelea kuwa nayo bila ya kutafuta wadau na kushirikiana kutengeneaa njia ya kufikia mafanikio hayo ni tatizo tena kubwa.

Wiki iliyopita nilimsikia Waziri Mchengerwa akizungumzia hata aina ya kocha atakayetuwezesha kufikia ndoto hiyo ya kushiriki fainali hizo kubwa katika mchezo wa soka.

Hapo ndipo nilipogutuka, kwamba safari ya Waziri Mchengerwa ya Tanzania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2030, zimeshafikia kiwango cha kuwa na aina ya kocha ambaye ataruhusiwa kuteua wachezaji kutoka daraja lolote lile? Maana yake hapo safari imeshaanza na imefika mbali.

Yaani bila ya kumuwahi kuzungumza naye, tunaweza kujikuta katika mazingira ambayo hatujui tufanye nini iwapo kutakuwa na vikwazo. Au tutafikia mahali ambapo tutasubiri ndoto ya Waziri Mchengerwa itimie hata kama vikwazo vitazidi uwezo wetu wa kukabiliana navyo.

Hapo juu nimeonyesha jinsi maono ya Mfalme Mohamad wa Vl yalivyooana na mkakati wa Rais wa Shirikisho la Soka la Morocco. Mmoja aliamua kutumia kila rasilimali ambazo serikali ingeweza kuzitoa, huku mwingine akiweka mazingira na mwongozo mzuri wa kuendeleza soka na ndio maana leo tunaimba mafanikio ya Morocco.

Hivyo ni muhimu sana Waziri Mchengerwa kuwa na maono hayo ya Tanzania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2030, lakini ni muhimu pia kumuwahi kuzungumza naye ili kuchora njia sahihi ya kufikia fainali hizo kwa kuzingatia majukumu tofauti ya wadau katika maendeleo ya soka.

Kama waziri ameshafikia kueleza aina ya kocha watakayemteua na mfumo wa kuteua wachezaji, maana yake Shirikisho la Soka (TFF) litawekwa kando katika mkakati huo na sijui kama hilo litawezekana. Ni vigumu!

Kwa hiyo nia njema ya Waziri Mchengerwa kuiwezesha Tanzania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2030, haina budi kuwasilishwa mbele ya kikao cha wadau wote wa soka na michezo kwa ujumla na kupanga njia ya kuelekea huko ili kusiwepo na chochote ambacho kitasahaulika na hata kama hatutafuzu, tuwe tumetumia fursa hiyo kuukuza mchezo wetu kutoka hatua moja hadi nyingine.

Hamu ya kucheza fainali za Kombe la Dunia ni ya kila mdau; mchezaji, klabu, nchi, viongozi wa soka, serikali, wafanyabiashara, na wengine wengi. Kwanini basi hawa wasitengeneze njia moja ambayo itasaidia kila upande?

Kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia hakuji kwa bahati nasibu, hata kama wakati huo Fifa itakuwa imeongeza idadi ya nchi kutoka Afrika. Ni lazima kuwe na mikakati mikubwa na inayoangalia kila sehemu muhimu; kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hivyo ndoto ya kufikia hilo haiwezi kuwepo wizarani pekee; ni lazima kila mdau ashirikishwe kutengeneza mkakati mmoja.

Na TFF haitakiwi kukaa pembeni kusubiri kuona jinsi Waziri Mchengerwa atakavyofeli, bali kumuwahi mapema na kumueleza jinsi mikakati ya kufika huko inavyotakiwa itengenezwe. Vivyo hivyo kwa wadau wengine wote wa michezo, ili mradi tu waziri ameshaonyesha matamanio yake na mpango wa serikali kufikia mafanikio ya juu kimichezo.

Wakati huu ambao Waziri Mchengerwa anaendelea kutangaza maono yake, na bila shaka ya serikali kuhusu fainali za Kombe la Dunia za 2030, ni muhimu kumuwahi na kumuweka chini kujadili mpango kabambe zaidi na shirikishi wa kufanikisha ndoto hiyo. Hatuhitaji kumuonyesha kwamba amepatia au amekosea, bali kumuonyesha njia ambayo tunadhani ni sahihi kimfumo kufikia huko anakotaka na ambako wote tunataka kufika.

Kama Waziri Mchengerwa ameshaanza safari ya Kombe la Dunia 2030, tumuwahi kabla hajafika mbali na kutengeneza mkakati jumuishi na shirikishi wa kufikia huko tutakako. La sivyo tutasubiri mwishoni kutafuta nani alikosea na nani alipatia, kitu ambacho hakitatusaidia zaidi ya kupoteza muda.

Columnist: Mwanaspoti