Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Utani wa jadi unatumika kupumbaza wengi

Simba Yanga Caf Utani wa jadi unatumika kupumbaza wengi

Wed, 10 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwishoni mwa wiki iliyopita niliangalia video za baadhi ya wazungumzaji kwenye mkutano wa Simba uliolenga kuzungumzia shughuli za msimu huu.

Video zilizosambazwa sana zilikuwa ni zile zinazowakebehi wapinzani wao, yaani Yanga, hasa kile walichofanya kwenye usajili huku matarajio ya Simba msimu huu yakionyeshwa kuwa yatakuwa somo kwa majirani zao wa Kariakoo.

Kila aliyepewa nafasi alijaribu kuchambua kilichosemwa na viongozi wa Yanga ili ufurahishe wajumbe. Ndivyo ilivyo hata kwa wapinzani wao wanapokuwa na mikutano yao. Mzungumzaji mzuri ni yule anayeweza kuwakejeli Simba kwa kila neno bovu, halafu wajumbe kucheka sana kana kwamba wamemaliza tatizo kuu walilolizungumza kwenye kikao hicho.

Kwa hiyo, inapofikia suala la taarifa za fedha au ripoti ya utendaji, huwa ni kama maluelue. Ni wachache wanaoelewa au kusikiliza kwa makini. Na wale waliosikiliza kwa makini wenye nia ya kudadisi huonekana wametumwa na hawana jingine lolote zaidi ya kutaka kuwapotezea muda. Ilifikia wakati mkutano Yanga ulionekana kuwachelewesha watu kwenda uwanjani kuiona timu yao, na wakati mwingine hata kuchelewa kwenda kula pilau lililoandaliwa na kiongozi.

Hata mikutano ya maofisa habari wa klabu hizo sasa imegeuka kuwa ya umbea. Ofisa Habari hawezi kuzungumzia zuri la timu yake kwa maelezo mazuri. Uzuri wa taarifa yake unakuja pale anapoifananisha na jambo la timu pinzani. Hapo huonekana ametumia akili sana na hata kuonekana anafaa kupata tuzo yoyote ya kijinga inayoweza kuan zishwa mitandaoni.

Huko ndiko tulikofikia. Hakuna tena mambo muhimu tunayoweza kujadili kwa kina. Linapokuja jambo muhimu, linarahisishwa na kushushwa ili lilingane na upuuzi na hivyo kuwa na uwanja mpana wa kulijadili katika viwango vya chini visivyolingana na jambo lenyewe.

Ukijaribu kulichambua hasa linapokuwa suala la fedha au uongozi, huwa kuna majibu mepesi kama mpira unataka pesa‚ au huko ndiko mpira unakoelekea. Ukimzuia huyo mtu asiongeze neno na kumwambia hebu tufafanulie hilo la mpira unataka pesa kulihusisha na hili, ni lazima atahangaika sana asijue alitoa wapi maneno hayo.

Bado kuna matatizo makubwa na ya msingi katika klabu zetu. Hizo siasa za utani wa jadi zinatumika kupumbaza watu wasijikite kujadili mambo muhimu kwa kina.

Hivi tangu klabu hizi zituambie zinafanya mageuzi, tumeweza kuona mabadiliko yenyewe? Tunaona kuna mambo ya msingi yamebadilika au kuna sura ndio zimebadilika? Je, uendeshaji umekuwa wa kisasa? Je, watendaji sasa wanapatikana kwa sifa? Je, menejimenti inaweza kufanya kazi kwa uhuru bila ya vikao vya kamati za utendaji kukutana mara kwa mara kuamua kile ambacho kingeamuliwa na ofisa mtendaji mkuu? Hivi wanachama wanaweza kutofautisha kati ya mwekezaji na mdhamini? Tofauti hizo zinaonekana dhahiri katika shughuli, taarifa na utendaji wa viongozi?

Lakini leo, ukisikia Yanga imemsajili Aziz Ki, basi utaambiwa ni kwa sababu ya mageuzi kwa kuwa mpira wa sasa unataka fedha! Ukiambiwa Simba imeingia mkataba wa kihistoria wa udhamini, utaambiwa ni kwa sababu ya uwekezaji na wengine watakwambia ni uhodari wa CEO, hata wasijue alifanya nini.

Yaani kuna majibu mepesi sana ili kukatisha mjadala wowote unaoweza kukuna kichwa. Mjadala mrefu utakuwa ni ule wa kudhihaki upande mwingine.

Tukiona Vipers wanashinda, tunashangaa! Kosi kubwa limeshindwaje? Hatuna majibu magumu kwa sababu tumejikita katika hoja nyepesi.

Columnist: Mwanaspoti