Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Tulimtimua Kim Poulsen kwa dharura!

Kim 1140x640 Kim Poulsen

Tue, 13 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Safari yetu kuelekea fainali za michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) ilikoma wiki iliyopita baada ya Taifa Stars kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda The Cranes, hivyo kutupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-0.

Katika mchezo wa kwanza wa nyumbani Kwa Mkapa, tulilala kwa bao 1-0 na kusababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen kuondolewa kwa maelezo atapangiwa kazi nyingine na kumteua Mzambia Hanour Janza kushika nafasi yake kwa muda.

Mabao yote manne ni mepesi yakitokana na uzembe wa mabeki na kipa. Dar es Salaam, beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alishindwa kuulinda mpira uliokuwa hauna madhara. Bao la kwanza la mechi ya marudiano jijini Entebbe lilitokana na Jonas Mkude kuufuata mguu wa Mganda baada ya kushindwa kuufikia mpira na kusababisha penalti.

Mabao mengine mawili yalitokana na mabeki kushindwa kujipanga kwa mipira ya juu na kuruhusu Waganda kufunga kirahisi kwa kichwa.

Siwezi kusema kuwa Poulsen asingefukuzwa, Stars isingeondolewa na Waganda, lakini naona kama staili ya kumtimua iliiga zile za dharura za klabu. Klabu humtimua kocha katikati ya mashindano na kocha mpya hulazimika kuhangaika na wachezaji anaowakuta kupata matokeo mazuri.

Kwa timu za taifa ni tofauti. Kocha huwa na wigo mpana wa kuchagua wachezaji kulingana na mahitaji yake. Lakini lisingewezekana kwa kocha mpya wa Tanzania kwa kuwa tayari timu ilikuwa katikati ya raundi moja ya mashindano na mechi ya marudiano ilikuwa ndani ya wiki moja.

Asingeweza kuanza kusaka wachezaji wanaoendana na mahitaji yake. Hakuwahi kufikiria kuwa angeteuliwa au kutaarifiwa mapema kuwa angeteuliwa na hivyo kupata wasaa wa kufuatilia wachezaji ambao angewaita iwapo angeteuliwa.

Kilichosubiriwa kutoka kwake ni miujiza; kwamba atumie wachezaji walioitwa na Kim kupata matokeo tofauti na yale ya Kwa Mkapa! Cha ajabu ni kwamba alikubali kuwa angeweza kufanya maajabu hayo.

Sidhani kama dharura ni njia nzuri ya kubadili makocha wa timu za taifa. Kim alistahili kuachiwa amalizie mechi ya marudiano baada ya kupata wasaa mzuri wa kuwasoma Waganda kwenye mechi ya kwanza na hivyo kufanya marekebisho kulingana na yaliyotokea na pia kuwapa fursa wachezaji wampiganie.

Pengine kumtimua ilikuwa ni kufunika makosa ambayo shirikisho liliyafanya.

Kim alilalamika sana kuhusu maandalizi, hasa muda wa kutosha na mechi za majaribio. Ajabu Waganda walikuja kucheza mechi ya majaribio hapahapa kwetu na timu ambayo hatukuwahi kuifikiria, lakini kwao ilitosha kuwapa sehemu ya picha ya kikosi chao.

Michuano ya CHAN huwa ni kipimo kizuri cha maendeleo ya ndani ya nchi, sera na kanuni zetu kuhusu wachezaji wageni, mikakati yetu ya maendeleo na mambo mengine.

Kwa vyovyote vile, nguvu kubwa ilitakiwa iwekwe huku CHAN kwa kuwa ndio kunatupa picha nzuri ya wapi tumefikia katika program zetu za kukuza wachezaji. Lakini pamoja na ukweli kuwa TFF walikuwa wameandaa mambo yao, bado mechi ya Waganda inaonekana ilikuja kama dharura ambayo tuliishughulikia kidharura! Hutegemei makubwa kwenye dharura labda uwe mzuri katika mikakati ya kukabiliana na majanga.

Kwa kuwa sisi si wazuri kukabiliana na majanga, tulifanya kile tulichoweza wakati huo. Kwamba Tanzania imefungwa nyumbani, tumuondoe Kim na tuungane na gumzo la mtaani kwamba ‘eti’ kocha huyo ni mzuri kwa soka la vijana hivyo tumrudishe hukohuko.

Halafu tumteue kocha mwingine ‘wa matokeo’ ili tuvuke hapa, halafu tuanze kutafuta kocha mpya baadaye. Dharura!

Tumeshafikia kiwango ambacho hakihitaji dharura. Kinahitaji mikakati ya muda mrefu na kushughulikia mambo kwa utulivu na si kwa dharura.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz