Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Tukerwe, tusizoee ubora wa waamuzi

Waamuzi Waamuzi TFF yaendesha Semina kwa waamuzi

Tue, 15 Feb 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna video mbili zinazotembea hivi sasa kuhalalisha makosa ya waamuzi wa Ligi Kuu. Mpya ni ile inayoonyesha refa wa mechi baina ya Simba na Prisons akitoa uamuzi wa adhabu ya penati kwa tukio ambalo alikuwa mbali karibu hatua 18.

Video ya pili ni ile iliyoibuliwa baada ya tukio hilo la katikati ya wiki. Video hiyo inamuonyesha refa aliyetoa adhabu ya penati kwa Yanga kwa tukio ambalo linaonekana kuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele aliunawa mpira wakati akijaribu kufunga kwa pigo la mkasi.

Na baada ya mechi ya Jumamosi baina ya Yanga na Mbeya City, video nyingi Zaidi za makosa ya waamuzi zitaibuka, hasa wakati huu ambao Ligi Kuu ya soka ya Bara inaingia katika duru la mwisho.

Ni matukio ambayo hayajaanza leo. Kila mara refa anapokosea katika mechi ya Yanga, basi itatafutwa video ya makosa kama hayo katika mechi ya Simba na baada ya hapo mchezo unakuwa umekwisha.

Ni kama tunajifunza kuzoea makosa ya waamuzi na kuyaona kwamba si kitu kikubwa kwa sababu yapo. Na hilo lilidhihirika baada ya kiongozi mmoja wa juu kueleza kuwa maneno mengi husemwa inapotokea makosa ya waamuzi katika mechi za vigogo hao, akithibitisha kuwa kuna makosa mengi Zaidi katika mechi zisizohusu klabu hizo mbili.

Maana yake ni kwamba tuzoee hayo makosa na wala tusiingie kulaumu kwa sababu yapo!

Ajabu sana. Na pengine kwa kauli kama hiyo, Kamati ya Waamuzi nayo inabidi ikae kimya, Isifikirie njia za kupunguza makosa hayo ambayo kuna uwezekano mkubwa hugharimu klabu kiuchumi kwa kuwa si rahisi wadhamini waendelee kuwa na Imani na timu ambazo hazipati ushindi kwa sababu ambazo hazielezeki.

Kwa hiyo chombo pekee kinachoshughulika na waamuzi ni ile Kamati ya Masaa 72, ambayo kazi yake kuu ni kuwaadhibu waamuzi wanaonekana kuvurunda. Watajirekebisha vipi si jukumu lao.

Tatizo ni kwamba hao wanaoadhibu wanatumia picha za marudio za video kuona kosa, wakati pale uwanjani refa hana hiyo fursa ya kuangalia tukio kwa mara ya pili. Wapo vijana wadogo waliofungiwa mwaka mmoja kwa kufanya makosa kwenye ligi ambayo hawakutakiwa hata wachezeshe. Watajifunza wapi baada ya kukosea, si jukumu la Kamati ya Masaa 72!

Wakati fulani mwenyekiti wa zamani wa waamuzi, Nampunde alikuwa na mpango wa kuanzisha kundi la marefa wa ubora wa juu (elite group of referees) kwa ajili ya kuwa na waamuzi wachache, wanaowezekana kuwamudu kwa mafunzo na marekebisho kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu.

Yaani kwa ligi ambayo ina timu 16, unahitaji marefa angalau 12 wa kati na wengine 20 wasaidizi kwa ajili ya Ligi Kuu na pengine mechi muhimu za Kombe la Shirikisho.

Kwa Uingereza, Select Groiup 1 lina waamuzi 22 wa kati ambao huteuliwa na Professional Game Match Officials Limited (PGMOL). Pia PGMOL ina waamuzi wasaidizi na jumla yao ni zaidi ya 70. Miongoni mwao wamo wa kulipwa na wale wa dei waka.

Lakini PGMOL ina jukumu la kuboresha viwango vya waamuzi hao, pia kila mechi huchambuliwa na mwamuzi wa zamani, ambaye huangalia kwa makini kila uamuzi kwa kutumia video za mchezo huo na taarifa za matukio kupima kiwango cha mwamzi. Wachezaji wateule wa zamani (Match Delegates) pia hupima kiwango cha usahihi wa uamuzi na jinsi waamuzi walivyomudu mechi.

Kabla ya kuteuliwa kuingia kwenye Select Group, waamuzi hufuatiliwa uchezeshaji wao na baadaye kuingia kambi ya siku mbili ambayo huhusisha mazoezi ya kimwili na kiufundi na baadaye kuchambua video za mechi na wanaofaulu ndio wanaingia kundi hilo.

Columnist: Mwanaspoti