Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Tuache udhamini kizamani, Barbara ametufikirisha

CEO Babra CEO wa Simba ,Babra Gonzalez

Tue, 14 Dec 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita ilitawaliwa na tukio la kampuni ya GSM kuingia kwenye kapu la udhamini wa Ligi Kuu na hivyo kuibua mzozo hasa kwa klabu ya Simba ambayo imeweka bayana kuwa kuna kasoro zinazotia shaka na kuugomea.

Simba ilifikirisha wengi kutokana na ukweli kwamba klabu washiriki wa Ligi Kuu ndio hasa wenye mali hiyo na hivyo, kama klabu nyingine zote walitakiwa kuwa na taarifa za kutosha kabla ya kuambiwa watavaa nembo ya mdhamini mpya. Kibaya zaidi ni kwamba mkataba huo uliingiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) badala ya Bodi ya Ligi ambayo ndiyo mwendeshaji wa Ligi Kuu.

Kituko kinakuja kwamba TFF inaingia mkataba halafu inauambia upande wa tatu—yaani wa pili ni Bodi ya Ligi atekeleze masharti ya mkataba uliosainiwa na TFF.

Ni kituko kwa kweli na Simba ina hoja tena za msingi kabisa katika hilo hivyo ni muhimu kwa TFF na Bodi ya Ligi kutotumia nguvu kulazimisha udhamini huo kwa sababu katika mazingira ya uwazi kabisa wadau wote walitakiwa wahusishwe kwa kiwango kikubwa kujua kwa kina manufaa na mgawanyo wa mapato ya udhamini huo.

Nimeshangaa kusoma kwamba eti kiongozi wa klabu ya Biashara anasema anachojali “ni fedha, na hayo mambo mengine hayawahusu”. Hicho ni kiwango kikubwa cha kutojua wajibu wake kama kiongozi wa klabu ya Ligi Kuu, haki za klabu hiyo na vyanzo vya mapato.

Kwa kiongozi kama huyo unaona dhahiri ni kwa sababu gani Biashara ilishindwa kwenda Libya kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda 2-0 nyumbani. Na unaona dhahiri sababu za timu hiyo kwenda kwa mbinde Djibout kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho.

Hawa si aina ya viongozi wanaotakiwa kuongoza klabu za Ligi Kuu kama upeo wake wa masuala ya udhamini, uwazi na haki za klabu ni mdogo kiasi hicho. Lakini ni muhimu pia kwa Bodi ya Ligi kuanza kukuza chapa ya Ligi Kuu kama bidhaa yake kubwa badala ya kung’ang’ania mfumo wa zamani wa udhamini. Haiwezekani Ligi Kuu ikawa na wadhamini wakuu wawili, mmoja akiwa amedandia gari wakati safari imeshaanza. Ni kituko kingine hicho.

Cha msingi ni kwa TPLB kuchukua mifumo inayotumiwa na nchi nyingine kama England, ambako kuna Premier League, Italia (Serie A), Hispania (La Liga), Ufaransa (Ligue 1) na Ujerumani (Bundesliga). Nchi hizo zimekuza chapa ya bidhaa zao kuu ambazo ni Ligi Kuu na kuzipa majina hayo. Hakuna tena udhamini wa haki peke (exclusive rights) wa ligi nzima kama ambao tumekuwa tukiipa Vodacom kwa muda mrefu. Udhamini huo wa jina la ligi sasa haupo tena, badala yake wenzetu wametengeneza vufurushi tofauti kwa ajili ya kuviuza kwa washirika kulingana na nyanja wanazofanyia biashara zao.

Mshirika mkuu wa Ligi Kuu ya England ni EA Sport, mshirika wa huduma za kibenki ni Barclays, wa bia ni Budweiser, wa muda ni Hublot, mpira maalum ni Nike na cloud ni Oracle. Pia wapo Avery Dennison na Panini kama licensees wakati wa utangazaji ni Sky, BT Sport, Prime Video na BBC Sport wakati redio ni BBC na Talk Sport.

Hawa wote ndio huweka fedha zinazoifanya Ligi Kuu ya England kuwa moja ya ligi bora duniani. Huu unatakiwa uwe mwelekeo badala ya huu uliosababisha usumbufu na Simba kiasi kwamba GSM anaweza kuona alipotea njia. Msimamo wa Simba umehusishwa na kitendo cha watu wa mlangoni kumzuia mtendaji mkuu wao, Barbara Gonzalez kuingia uwanjani kushuhudia pambano dhidi ya Yanga, Jumamosi, kutokana na kiongozi huyo kuwa mstari wa mbele kuhoji udhamini wa GSM.

Walimzuia kwa sababu aliambatana na watoto ambao ‘hawaruhusiwi kuingia eneo la VIP’ nay eye alikataa kuwaacha, akitaka aingie nao.

TFF na Bodi ya Ligi wanaweza kuwa sahihi, lakini Barbara ametufikirisha kuhusu nafasi ya familia katika kuburudika na mechi za ligi, hasa kipindi hiki ambacho ripoti ya mahudhurio ya mashabiki viwanjani msimu uliopita ilionyesha tatizo kubwa.

Mtu mwenye hadhi ya VIP anayetaka kwenda kushuhudia mechi na watoto wake afanyeje. Kama Barbara angekubali kutengana na watoto alioenda nao, wangewekwa sehemu gani salama hata kama angewalipia? Kuna sehemu maalum kwa ajili ya watoto wanaokuja na wazazi wao ambao ni VIP?

Kama ilivyo kwa wenzetu England, ripoti ya Lord Taylor kuhusu janga la Hillsborough lililoua mashabiki 95 wa Liverpoo, ndio lilileta usalama unaowezesha mashabiki kwenda viwanjani na wake na watoto wao.

Hili la Barbara tunalichukuliaje. Au ndio tunabakia kutolea matamko kuwa eti ‘alionyesha jeuri’ badala ya kuangalia changamoto iliyoibuliwa na kitendo chake cha kukataa kutengana na watoto ambao hawaruhusiwi VIP?

Columnist: Mwanaspoti