Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Tahadhari, 'ile kwa Mkapa hatoki mtu' hubadilika

Air Manula Tahadhari, 'ile kwa Mkapa hatoki mtu' hubadilika

Tue, 29 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya klabu, Simba, watakamilisha mechi za raundi ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa kuvaana na vigogo wa Niger, Union Sportive Gendarmerie (USGN).

Simba ina pointi saba, sawa na RS Berkane ya Morocco iliyopo nafasi ya pili, USGN ikishika mkia (4) na Asec Mimosas ya Ivory Coast ikiwa kileleni na pointi tisa.

Ni kama Simba inasubiri mechi hiyo ya Aprili 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kukamilisha safari ya nusu fainali kwa kuwa Wabotswana hawaonekani kuwa kikwazo.

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Niger, Simba ililazimisha sare ya bao 1-1, Bernard Morrison akiingia kipindi cha pili na kusawazisha mambo.

Lakini historia haituambii kuwa mechi hiyo ni rahisi kama mechi nyingine za makundi ambazo huwa si ya kuamua hatima ya timu mashindanoni. Kwa hiyo hata ile kauli ya “Kwa Mkapa Hatoki Mtu” haiendani na mazingira ya mchezo huo.

Ni mechi chache ambazo Simba ilitumia vizuri uwanja wa nyumbani kuamua hatima yake mashindano, hasa katika hatua za juu. Katika mechi dhidi ya Nkana Red Devils, bao lililofungwa dakika za mwisho baada ya Simba kuanzisha mpira wa haraka, liliipeleka Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ziko mechi nyingine kadhaa ambazo Simba iliamua hatima yake jijini Dar es Salaam, lakini zile za hatua ya juu zimekuwa changamoto kwa mabingwa hao watetezi.

Mwaka 1993, Simba ililazimisha sare ya bila kufungana na Stella Abidjan nchini Ivory Coast, hivyo kuwa na uhakika kutwaa Kombe la CAF jijini Dar es Salaam.

Lakini Boli Zozo aliharibu kila kitu. Alifunga mabao mawili yaliyozima maandalizi yote ya sherehe za ubingwa yaliyokuwa yamefanywa na baadhi kutangazwa uwanjani.

Hali kama hiyo iliitokea Simba katika mechi ya mtoano dhidi ya Ismailia ya Misri jijini Dar es Salaam. Simba ilikuwa inahitaji matokeo mazuri kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) ili kulipa kiasi cha kufungwa mabao 2-0 ugenini.

Joseph Kaniki alifunga mabao mawili, lakini mechi hiyo ikavunjwa kutokana na mvua kubwa. Iliporudiwa siku iliyofuata, matokeo yakawa ni ushindi wa bao 1-0 na Simba kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.

Simba ilikutana na hali kama hiyo katika michuano ya CAF baada ya kupata bao la ugenini jijini Abidjan dhidi ya Asec Mimosas ilipofungwa mabao 2-1. Ilitegemea kuwa ingepata angalau bao moja Dar ili isonge mbele. Lakini Sekou Bamba akatibua mipango hiyo.

Bamba alifunga bao la kwanza na katika kipindi cha pili akatoa pasi ya bao kuipa Asec ushindi wa mabao 2-0 na kuzima ndoto za Simba.

Katika mechi dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, Simba ilifanikiwa kulazimisha sare ya bila kufungana jijini Maputo na hivyo ushindi wa aina yoyote jijini Dar es Salaam ungeipa tiketi ya kuvuka raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa. Lakini Luis Miquissone akaifungia UD Songo bao la kuongoza dakika ya 14 kwenye Uwanja wa Mkapa na bao la penalti lililofungwa na Erasto Nyoni katika dakika ya mwisho halikuweza kuizuia UD Songo kusonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.

Na mwaka huu ambao Simba ilishindwa tena kuutumia Uwanja wa Mkapa kuamua hatima yake katika Ligi ya Mabingwa. Iliishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy nchini Botswana na katika mechi ya marudiano ilitangulia kufunga na hivyo kuonekana imesafisha njia jijini Dar es Salaam.

Lakini Galaxy walizinduka na kufunga mabao matatu yaliyowapa ushindi wa sheria ya bao la ugenini, kwani matokeo ya mwisho yalikuwa ni mabao 3-3.

Nimetumia rekodi hizo chache kuikumbusha Simba kuwa inapofikia mazingira ambayo yanaonekana mepesi, hali huwa tofauti na matokeo kuigharimu. Kwanza viongozi huanza kutoa kauli ambazo zinaonekana kama wameshavuka hata kabla ya timu kushuka uwanjani.

Ni lazima kauli kama hizo huvuruga saikolojia ya wachezaji na kuwapa mashabiki matumaini yasiyo halisi na wanapoona mambo tofauti uwanjani, hupoteza hata ile ari ya kushangilia.

Ni muhimu Simba kujiandaa kwa mechi ya Gendarmerie ikiwa na kumbukumbu hizo na hivyo kufanya mambo sahihi kwa kuwa hata wapinzani wao wanajipanga tofauti.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz